Namba hazijamsaidia Depu pale Yanga
Muktasari:
- Jamaa alishuka nchini akitokea Poland alikokuwa akiichezea Radomiak Radon inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
MIONGONI mwa sajili za dirisha dogo ambazo zilitikisa hapa kijiweni ni wa mshambuliaji Laurindo Dilson Maria Aurelio 'Depu'.
Jamaa alishuka nchini akitokea Poland alikokuwa akiichezea Radomiak Radon inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.
Katika siku zake za mwanzo Yanga, Depu alionekana kufanya vizuri kiasi ambacho alitufanya wengi tuamini balaa jipya limetinga Ligi Kuu Bara na hasa akichagizwa na historia yake wakati akiwa Angola.
Ndani ya kipindi hicho cha mwanzo, jamaa akatupia mabao sita na kupiga pasi mbili za mwisho katika mechi zake saba za mwanzo za ligi ikimaanisha alihusika na mabao manane katika mechi saba.
Kwa tathmini ya harakaharaka, takwimu hizo za Depu sio mbaya tena kwa mshambuliaji ambaye ndio kwanza amenaswa dirisha dogo la usajili na hakuwa na uzoefu wa ligi yetu wala mazingira ya Tanzania.
Pamoja na hayo, aliyofanya katika hizo mechi za mwanzo alizocheza baada ya dirisha dogo la usajili na takwimu zake, maisha ya Depu Yanga yapo mtegoni na kuna uwezekano mkubwa akaachwa dirisha kubwa lijalo la usajili.
Inasemekana pamoja na kukiri uwezo wa Depu katika kufumania nyavu, wazito Yanga wanaamini mchezaji huyo raia wa Angola sio mshambuliaji wa kisasa anayeweza kushiriki katika mechi tofauti na kufunga tu.
Kama Depu akiachwa, itadhihirisha wakati mwingine namba siyo kila kitu katika maisha ya mchezaji na hazitoshi kumlinda ndani ya timu.
Ingekuwa soka la zamani, Depu angelindwa kwa wivu mkubwa lakini kwa sasa ni tofauti. Watu wanaangalia zaidi ya kufunga mabao.