MZEE WA UPUPU: Super League ni zaidi ya Ligi

KWA mara ya kwanza katika historia ya hatua ya makundi na kuendelea kwa klabu ya Simba, mwiko umevunjwa nyumbani.
Simba haikuwahi kufungwa kwenye uwanja wa nyumbani katika hatua ya makundi ya mashindano ya Afrika, tangu ianze kufika hatua hiyo mwaka 2003.
Katika kipindi hicho Simba imecheza mechi 15 nyumbani na kutoka salama zote.
2003 - mechi 3
Simba 0 - 0 Ismailia
Simba 1 - 0 Asec Mimosas
Simba 2 - 1 Enyimba
2018/19 - mechi 4
Simba 3-0 Smouha
Simba 1-0 Al Ahly
Simba 2-1 AS Vita
Simba 0-0 TP Mazembe
2020/21 - mechi 4
Simba 1-0 Al Ahly
Simba 4-1 AS Vita
Simba 3-0 El Merreikh
Simba 3-0 Kaizer Chiefs
2021/22 - mechi 4
Simba 3-1 Asec Mimosas
Simba 1-0 RS Berkane
Simba 4-0 US Gendarmerie
Simba 1-0 Orlando Pirates
Katika mechi hizo 15, Simba iliruhusu mabao 4 tu kwenye uwanja wa nyumbani. Lakini katika mechi hii moja tu dhidi ya Raja Casablanca, Simba imeruhusu mabao matatu.
Sasa kiwango ambacho Raja Casablanca wamekionyesha dhidi ya Simba kwa Mkapa, ndicho kitakachoonyeshwa na wapinzani kwenye mashindano mapya ya African Super League.
Super League ni mashindano yatakayokutanisha timu za daraja la Raja tu, yaani wao Simba ni kati ya klabu ndogo zaidi huko.
SUPER LEAGUE NI NINI?
Ni mashindano mapya ya klabu barani Afrika yanayoandaliwa na shirikisho la soka barani humu, CAF, kwa baraka za shirikisho la soka duniani, FIFA.
Mashindano haya yanalenga kuleta mapinduzi kwenye soka la Afrika na kuyafanya kuwa mashindano yenye pesa nyingi zaidi barani humu.
Awali, yalipangwa kuwa na timu 24 zitazogawanywa kwenye makundi matatu ya timu nane nane.
Lakini sasa inasemekana kutakuwa na kundi moja tu, la timu nane zitakazocheza nyumbani na ugenini. Mashindano hayo yamepagwa kuanza Agosti mwaka huu.
MASHINDANO YA PESA NYINGI
Hiki ndicho kipengele kitakachozitoa roho timu za Afrika.
CAF imepanga kuweka pesa ndefu kuyafanya mashindano haya yawe na heshima kubwa.
Julai 3, 2022, CAF ilitangaza kwamba jumla ya dola milioni 100 zitatolewa kama zawadi huku bingwa akipata dola milioni 11.5.
Shirikisho la soka la kila nchi litapata mgao wa dola milioni moja (zaidi ya shilingi bilioni mbili) kutoka kwenye Super League.
Kila klabu itakayoshiriki itapata dola milioni 2.5 (zaidi ya bilioni tano) za maandalizi tu.
BALAA KWA SIMBA
Simba inatajwa kama moja ya klabu zitakazoshi-
riki mashindano hayo na hivi karibuni wajumbe wa CAF walitembelea ofisi za klabu hiyo kama sehemu ya maandalizi ya kuzijua timu shiriki.
Kwa pesa hizo ambazo CAF imeziweka mezani, klabu kubwa zitatoa siyo tu macho bali viungo vyote kuhakikisha zinaenda kwao.
Hapo ndipo kiwango kama cha Raja kitaonekana kwa Mkapa kila wakati.
Kwa kawaida, timu kubwa za Afrika kama Al Ahly zina tabia ya kutegea ugenini na kwenda kushinda nyumbani.
Lakini katika mashindano haya ambayo wanaume wanakukazia kamba za viatu hata kwako, ni hatari kulegea ugenini kwa sababu unaweza kutoka kapa nyumbani na ukalowa!
Kwa hiyo hata Al Ahly atakuja kwa Mkapa na kutoa kiwango kama cha Raja. Na hapo bado kuna wengine kama kina Esperance na Wydad ambayo soka lao siku zote ni la mwendo kasi....yaani wanakupelekea moto tu, uwe kwako au kwao.
Kwa hiyo Simba wanatakiwa kujitathmini kuona kama wako tayari kiufundi kushiriki mashindano hayo.
Agosti bado mbali kidogo na mwezi Julai kutakuwa na dirisha jingine la usajili...wajipange sawasawa na wahakikishe wanapata kocha mwenye kiwango cha Super League ili kuijenga timu itakayopunguza aibu kama hii ya Raja. Maana Raja siyo tu waliifunga Simba bali waliifundisha mpira.
Kasi ya mchezo, uhakika wa pasi, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja na hata uwezo wa timu kwa ujumla ulikuwa wa hali ya juu sana. Wakipoteza mpira wanajua kurudi na kufunga njia. Wakiupata mpira wanajua kutoka na kukaa kwenye nafasi wapasiane.
Simba hawajawahi kukutana na timu inayocheza namna hii katika mechi zote 15 zilizopita kwenye mashindano ya Afrika.
Hata walipofungwa 3-0 na Enyimba 2003 haikuwa kwa sababu ya uwezo kama huu, au walipofungwa 4-0 na Kaizer Chiefs mwaka 2021, haikuwa kwa sababu ya uwezo mkubwa namna hii bali makosa zaidi ya mchezaji mmoja mmoja.
Lakini kwa Raja, ni uwezo ambao Simba walishindwa kabisa kuufikia. Raja ni kielelezo tu hali itakavyokuwa kwenye Super League...kutoka kapa kwa Mkapa kwa Simba inaweza kuwa hadithi ya kawaida.