Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau watoa mbinu upatikanaji bima kwa wachezaji - 3

Muktasari:

  • Vilevile, wanapendekeza kutolewa elimu kuhusu afya, mikataba na haki za wachezaji.

WADAU wa soka nchini wanapendekeza uwepo ushirikiano wa vilabu na kampuni za bima na hospitali ili kuwawezesha wachezaji kuwa na bima za afya kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Vilevile, wanapendekeza kutolewa elimu kuhusu afya, mikataba na haki za wachezaji.

Mkurugenzi wa Sheria na Masoko wa TFF, Boniface Wambura anasema vyama vinavyosimamia haki za wachezaji vinapaswa kuongeza nguvu ya kuwatetea wanamichezo kwa kuhakikisha hakuna mchezaji anayesajiliwa bila kuwa na uhakika wa matibabu pamoja na huduma za afya.

Mbali ya hayo, Wambura anasema: “Kuna umuhimu wa kuanzishwa mfuko maalumu wa afya kwa wachezaji ambao unaweza kusaidia wale wanaopata majeraha makubwa hasa katika timu zenye uwezo mdogo kifedha,” anasema.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, anasisitiza kuwa bima ni haki ya msingi kwa wanamichezo wote.

Anasema Serikali pamoja na vyombo vya michezo vinapaswa kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bima kwa wachezaji, huku elimu juu ya afya, mikataba pamoja na haki za wachezaji ikitolewa kuanzia ngazi za chini kabisa za soka.

“Wapo wengi wanaingia kwenye soka wakiwa na ndoto za kucheza pekee bila kufahamu hatari zinazoweza kuwapata wanapopata majeraha,” anasema.

Anasema wapo wachezaji wengi wanasaini mikataba bila hata kuuliza kama wanapatiwa bima au la.

“Mwisho wa siku wanapopata matatizo ndipo wanatambua kuwa walipaswa kusimamia haki zao mapema.”

Abeid Kasabalala, Katibu Msaidizi wa taasisi inayosimamia haki za wachezaji (Spata), anasema timu kubwa zinapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuhakikisha wachezaji pamoja na familia zao wanakuwa salama kiafya muda wote. “Hii itasaidia timu ndogo kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye afya za wachezaji. Mchezaji mwenye afya bora ndio msingi wa mafanikio ya timu,” anasema. Maoni ya vilabu, mwanasheria

Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC FC, Daniel Madenyeka, anasema ni muhimu kwa klabu kushirikiana na kampuni za bima pamoja na hospitali ili kupata vifurushi rafiki vitakavyoweza kuwasaidia wachezaji kupata matibabu ya kawaida na makubwa kama vile upasuaji.

“Kwa sasa baadhi ya bima zinazotolewa kwa wachezaji haziwezi hata kugharimia majeraha makubwa jambo linalowafanya wachezaji wengi kuendelea kutumia fedha zao binafsi wanapoumia,” anasema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate FC, Kelvin Herry katika hilo anasema: “Mchezaji anapoumia na kushindwa kupata matibabu ya haraka, klabu yenyewe hupoteza uwezo wake ndani ya uwanja. Lakini kuna madhara makubwa kwa maisha ya mchezaji baada ya soka, hasa pale anaposhindwa kuendelea na taaluma kutokana na majeraha.”

Monday Iddy, mwanasheria wa michezo anasema klabu haidhuriki kuliko mchezaji husika, hivyo wanaotakiwa kupigania haki zao ni wachezaji wenyewe.

“Sehemu kama TFF na Spata huko ndiko wachezaji wanatakiwa kupeleka malalamiko dhidi ya klabu ili hao wenye mamlaka waweze kusimamia na kuhakikisha klabu inatekeleza kile ambacho sheria inasema kwa upande wa michezo,” anasema.


MTAZAMO WA WANASOKA

Ni mtazamo wa mchezaji Gerald Mdamu, kuwa, wachezaji wanapaswa kupewa elimu kuhusu umuhimu wa bima kwa sababu wengi hawajui.

Anaeleza kuwa soka linaweza kuisha kwa dakika moja kutokana na jeraha, lakini maisha ya mchezaji yanaendelea hata baada ya kutoka uwanjani.

“Kulinda afya kunapaswa kuwa jambo la lazima kwa kila klabu inayotaka kuonekana ya kisasa na yenye kuthamini rasilimaliwatu wake,” anasema.

Mdamu aliyevitumikia vilabu vya Mwadui FC na Police Tanzania FC akiwa mshambuliaji ni mmoja wa waathirika wa kutokuwa na bima baada ya maisha yake kisoka kukatishwa alipopata ajali ya gari.

“Vyombo vya habari wasaidieni wachezaji wapate haki, lakini wapewe elimu kwa sababu wengi hawajui umuhimu wa bima. Wanachojali ni kusajiliwa na kucheza lakini kuna maisha nje ya hayo,” anasema.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Dua Said anasema maisha yamebadilika akieleza miaka ya nyuma hapakuwa na bima na madhara yalikuwa makubwa kwani wapo walioacha soka kutokana na majeraha.

“Kwa wanaocheza kipindi hiki huduma nyingi za muhimu wanazipata na sheria za kuwalinda pia zipo, wakati wetu tulipoteza wengi kwa sababu tu ya majeraha, kwa sasa ukiwa na bima ni rahisi kusaidika,” anasema.

Anashauri sheria na kanuni kutekelezwa kwa ukamilifu ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa kwenye mikono salama.

“Matatizo hayana hodi, unaweza kupata majeraha wakati ambao huna pesa ila bima ikaokoa,” anasema.

Mkongwe katika soka, Abdallah Kibadeni anasema kitu cha kwanza kwa mchezaji ni afya kabla ya kiwango chake, hivyo hatarajii kusikia klabu ikisema haitoi bima kwa kuwa ni jambo la lazima.