Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwalimu kunyakuliwa na Yanga ni pigo kisaikolojia

Muktasari:

  • Wakati huohuo, jana usiku kulikuwa na Dabi ya Kariakoo katika Ngao ya Jamii iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan Abeid Karume, visiwani Zanzibar, Unguja. Katika mchezo huo, ndipo ilipotazamiwa kupatikana picha ya nani hasa amesajili kikosi kikali zaidi ya mtani wake.

HARAKATI za kutambulisha nyota wapya wakati wa Siku ya Simba iliyofanyika Jumamosi na Siku ya Yanga zilinoga sana, hii ni baada ya mshambuliaji Selemani Mwalimu, aliyetajwa kuwa ni mchezaji wa Simba, kunyakuliwa kwa mkopo na klabu ya Yanga.

Wakati huohuo, jana usiku kulikuwa na Dabi ya Kariakoo katika Ngao ya Jamii iliyochezwa kwenye Uwanja wa Amaan Abeid Karume, visiwani Zanzibar, Unguja. Katika mchezo huo, ndipo ilipotazamiwa kupatikana picha ya nani hasa amesajili kikosi kikali zaidi ya mtani wake.

Sakata la kunyakuliwa kwa mshambuliaji Mtanzania kutoka Zanzibar, Mwalimu, ambaye alikuwa akikpiga nchini Morocco katika klabu ya Wydad Athletic, lilibadili saikolojia ya soka. Magazetini, mitaani na mitandaoni, mashabiki wa Simba walionekana kuumizwa kihisia, kwani siku moja kabla walitangaziwa kuwa mchezaji huyo anatua Msimbazi.

Baada ya siku chache, juzi Jumatatu, mchezaji huyo alionekana akitambulishwa katika klabu ya Jangwani na Rais wa Yanga, Said Hersi.

Shangwe lilikuwa kubwa sana kwa mashabiki wa Jangwani, wakionekana kuupokea usajili huo kwa furaha na matumaini makubwa. Kunyakuliwa kwa Mwalimu ni pigo kubwa kisaikolojia kwa uongozi wa klabu ya Simba na wachezaji, kwani inaweza kuwapa hofu au wasiwasi wa kulaumiwa. Vilevile, tukio hilo linaweza kuwafanya kukosa kujiamini mbele ya mashabiki wao ambao walimtangaza kuwa mchezaji huyo ni wao.

Mbinu iliyotumiwa na Yanga kumnyakua Mwalimu siyo tu pigo la mbinu za kiufundi, bali pia ni pigo la kisaikolojia ambalo linaweza kuwapa hofu ya kushindwa kwa Simba.


WANAIPOKELEAJE HII KISAIKOLOJIA?

Mtakumbuka Yanga tayari ina washambuliaji wanne ambao wako vizuri katika kiwango cha uchezaji. Kutua kwa Mwalimu tayari kunaweza kuwapa hofu washambuliaji wengine.

Kutua kwa Mwalimu kunaweza kuwafanya washambuliaji hao kisaikolojia kujituma zaidi uwanjani kwa hofu ya kupokonywa namba au kusugua benchi.


FAIDA DHIDI YA MAJERAHA

Kutua kwa Mwalimu kunaleta ahueni kubwa sana katika safu ya ushambuliaji ya Yanga, hii ni kwa sababu kocha ana washambuliaji wanne. Hivyo, anakuwa na uhuru wa kuwabadilisha mara kwa mara, kadiri anavyotaka na kulingana na uhitaji wa mechi na umuhimu wake.

Kitendo cha kuwa na washambuliaji wengi kina maana kuwa Yanga inaweza kuepukana na majeraha yatokanayo na kutumika sana bila kupumzishwa. Mtindo wa kubadilisha washambuliaji una msukumo mkubwa kisaikolojia kwa washambuliaji kujiamini na kutumia mbinu za kuepuka majeraha.

Utakumbuka kuwa washambuliaji ndio ambao mara kwa mara hufanyiwa sana faulo, hivyo kuwa katika hatari ya kupata majeraha.

Wingi wa washambuliaji na kubadilishwa mara kwa mara unawapa nafasi ya kupata mapumziko, hii ina faida ya kuwaepusha na majeraha, lakini pia kuupa nafasi mwili kupona majeraha ya ndani kwa ndani.


KUONGEZEKA KIWANGO CHA WACHEZAJI

Faida ya kuwa na wingi wa washambuliaji inalinda utendaji kazi na utimamu wa mchezaji, hii ni kwa sababu hana mzigo mkubwa wa kazi peke yake, bali wanagawana.

Mchezaji anayepata mapumziko huku akiwa anatumika kwa wastani anaweza kuwa na utendaji kazi bora uwanjani, huku akiboresha utimamu wake wa mwili kwa ujumla. Eneo la ushambuliaji linapokuwa na wachezaji wengi linasababisha saikolojia nzima ya timu kuwa bora, hii ni kwa sababu wanacheza wakijiamini kuwa wana silaha za kumsambaratisha adui.

Hali kama hii inaleta utulivu mkubwa kiakili kwa timu nzima, hivyo kuweza kuwa na mshikamano mkubwa na hatimaye kucheza kwa kiwango cha juu kwa muda mrefu bila kuchoka. Vitu hivi vitampa ubora zaidi Mwalimu na wengine.


JUHUDI BINAFSI NA NIDHAMU

Wachezaji wengi mastaa waliofanikiwa duniani walikuwa na juhudi binafsi, ikiwamo kufanya mazoezi binafsi na kujituma katika kila jukumu analopewa. Nidhamu ni msingi wa kufanya majukumu mbalimbali ya mafunzo na mazoezi bila kusukumwa au kushurutishwa. Nidhamu ndiyo inayomfanya mchezaji kuhudhuria mafunzo na mazoezi kwa wakati, kula chakula kwa kuzingatia ratiba, na kupumzika na kulala kwa muda uliopendekezwa.

Juhudi binafsi zinahusisha pia kujiongeza kwa kuufanyia mwili mazoezi tiba na yale ya uponaji baada ya mechi au mazoezi makali. Hapa mchezaji anayejiongeza kwa kujipa huduma za kuongeza na kulinda utimamu, ikiwamo mazoezi lainishi ya viungo, usingaji, yaani masaji, uogaji katika mabafu ya maji baridi na mvuke au katika mabwawa ya kuogelea na mazoezi ya gym.

Vilevile, lishe binafsi ya wanamichezo iliyopendekezwa na mtaalamu wa lishe za wanamichezo, ikiwamo unywaji wa maji na vinywaji maalum vya wanamichezo, ulaji wa matunda, mboga mboga na minofu ya protini.


ZINGATIA MIIKO YA MWANASOKA

Mchezaji mzuri na mwenye kuhitaji kufika mbali ni lazima ashikamane na miiko ya mwanasoka, ikiwamo kutotumia vilevi kama pombe na dawa za kulevya, kutotumia tumbaku na bidhaa zake kama vile viper na shisha, na kushiriki tendo la ndoa kwa ratiba bila kuingilia ratiba na mipango ya mechi na mazoezi. Vilevile, kujiburudisha na vitu visivyochosha akili, mfano kutumia kwa wastani TV, simu au mitandao ya kijamii, kupumzika mahali tulivu na kulala saa 8-10, na kutokula vyakula kiholela.


SOMA, JIPE MAARIFA NA MBINU MPYA

Soka la kisasa linahitaji ufahamu mpya na ubunifu mpya kila mara. Huwezi kuwa bora kama husomi vitabu vya soka, hutazami wachezaji waliokuzidi au wale wa zamani waliofanya vyema.

Kusoma na kujifunza mbinu ni lazima usome, uelewe, ujijengee uwezo wa kutenda, hatimaye kutenda kwa upekee na kukupa matokeo makubwa uwanjani. Ili kufanikiwa kusoma na kujifunza, ni lazima uwe na utulivu wa kiakili na lazima kuishi katika mazingira yanayokupa utulivu. Ndio maana mchezaji hatakiwi kuwa na migogoro isiyo ya lazima, na kama ipo, basi hatua za kuwaona wanasaikolojia au washauri nasaha zifanyike.


LINDA AFYA KWA WIVU MKUBWA

Mchezaji hatakiwi kujilinda pekee na majeraha yatokanayo na michezo, bali pia kuwa na mienendo na mitindo bora ya kimaisha ambayo itamlinda kutokupata magonjwa mengine.Ikumbukwe kuwa afya ni mtaji kwa mwanasoka. Kuumwa ugonjwa wowote ule tayari inavuruga utimamu wa mwili, hivyo na lazima atashindwa kucheza kwa kiwango.


WAPI NA NANI ANAKUTIBU?

Wachezaji mastaa wanaolipwa huwa wanajiongeza, ikiwamo kuwa na mikataba na vituo vya tiba na madaktari wa majeraha ya michezo pale wanapopata majeraha na kuumwa.

Kuwa na daktari binafsi ambaye anaweza kuwa mshauri sahihi wakati wa changamoto za kiafya na pia kukushauri kituo gani ni sahihi kutibiwa. Vilevile, mchezaji kujiongeza na kuwa na bima ya afya ni jambo la msingi. Hii inasaidia kupunguza gharama kubwa pale wanapopata changamoto za kiafya.