Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MTU WA MPIRA: Waamuzi wanakosea makusudi au hawajui?

LIGI Kuu Bara ni namba tano kwa ubora Afrika nzima. Ni heshima kubwa sana. Ni historia kubwa kwa nyakati hizi.

Haijalishi nani alitoa takwimu hizi, ila ukweli ni kwamba kwa sasa Ligi ya Tanzania Bara iko juu. Imepiga hatua kubwa sana kufika hapa.

Kuna watu wengi wametoa machozi, jasho na damu kuifikisha hapa. Kila mmoja kwa wakati wake.

Timu zilianza kununua wachezaji wakubwa. Azam TV wakanunua haki za Matangazo ya Televisheni. Wadhamini wakajitokeza. Kwanini tusipige hatua?

Moja ya hatua kubwa ilikua kuanzishwa kwa Bodi ya Ligi (TPLB). Ilikua ni mwanzo mzuri sana.

Changamoto ni kwamba mwanzo kulikuwa na shida ya mamlaka. Bodi ya Ligi ikawepo lakini maamuzi yote bado yalibaki pale Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Maamuzi ambayo yangefanywa na bodi yakabaki kuwa madogo madogo tu. Kazi ikawa ngumu.

Hata hivyo kuingia kwa Rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia kukabadili mambo mengi. Wakamuweka Almas Kasongo kama Mtendaji Mkuu wa Bodi. Wakaipa mamlaka kubwa Bodi.

Ikaanza kwa kuhamishia ofisi yao sehemu yenye hadhi zaidi. Bodi ikaajiri wafanyakazi wengi zaidi. Ikawa na usimamizi mkubwa.

Ikaanza kuweka mipango ya kuboresha Ligi yetu. Wakaweka mkazo kwenye ubora wa viwanja vya soka. Kila timu ikatakiwa kuwa na uwanja wenye hadhi na eneo la kuchezea. Viwanja vikafungiwa. Timu zikaamka usingizini na kuona ulazima wa kusimamia hilo.

Bodi ikasimamia masuala mengi ya msingi ya uendeshaji wa timu. Nidhamu ya timu ikapanda na kila mmoja akafuata usimamizi wa Bodi.

Pili, Azam TV wakaongeza uwekezaji wao. Wakaamua kuonyesha mechi zote za Ligi. Wakapata ushirikiano wa Bodi kwa kuwapangia ratiba rafiki kwa TV.  Hadi sasa Tanzania ni moja ya nchi chache Afrika ambazo mechi zote zipo kwenye televisheni. Inafurahisha sana.

Katika kuhakikisha jambo hilo linakwenda vizuri, Azam TV wakajitolea kufunga taa kwenye viwanja vinne nchini ili kuongeza idadi ya mechi za usiku.

Wakafunga taa pale Kaitaba, Majaliwa, Jamhuri na Mkwakwani. Sasa Ligi imekuwa na mechi za kutosha za usiku.

Katika viwanja 16 vinavyotumika kwenye Ligi, sita vina taa. Ni hatua kubwa sana.

Pia, Azam TV ikaongeza fedha kwenye haki za matangazo. Kila timu inapata zaidi ya Sh 500 milioni kwa kila msimu. Fedha hizi zikaelekezwa kwenda kulipa wachezaji mishahara. Hii ikasaidia kuondoa yale madai ya wachezaji kuwa wamekaa miezi kadhaa bila kulipwa. Uzuri wa pesa za Azam TV huwa zinatoka kwa wakati.

Wakaongeza pia zawadi kwa washindi. Leo hii bingwa anapata zaidi ya Sh 500 milioni. Timu inayoshika nafasi ya nne inapata zaidi ya Sh 200 milioni. Inafurahisha sana.

Mabadiliko haya yameongeza ubora wa Ligi sana. Timu zina uhakika wa maisha.

Pamoja na ubora wote, bado eneo la Waamuzi limekuwa changamoto sana. Timu nyingi zimekuwa zikilalamikia eneo hili.

Mapema tu msimu huu kumeanza kuwa na maamuzi ya utata. Unatazama tukio hadi unajiuliza kama mwamuzi anafahamu sheria vizuri ama anafanya makusudi.

Mfano ile faulo aliyochezewa Joyce Lomalisa pale Azam Complex, Chamazi. Kwanini mwamuzi hakutoa kadi nyekundu? Anajua mwenyewe.

Ilikuwa faulo mbaya sana. Lomalisa akaumia vibaya. Mwisho wa siku ikatoka kadi ya njano tu.

Zipo timu zimepewa penalti za ovyo msimu huu. Sitaki kuzitaja hapa, lakini wenyewe mmejionea.

Kuna muda off-side za wazi tu zinaachwa. Wapinzani wanalalamika na hakuna kinachotokea. Inaumiza sana.

Wakati tukiendelea kujivunia ubora wa Ligi yetu, ipo haja ya kuendelea kuboresha eneo la waamuzi. Kama haki hakuna, ushindani unapungua.

Hakuna kitu kinaumiza kama timu imesajili wachezaji mahiri, inawalipa vizuri. Inaajiri makocha wazuri halafu uwanjani refa anakwenda kuwaumiza uwanjani. Inasikitisha sana.

Timu zishinde kwa haki. Timu zifungwe kwa haki. Hapo soka letu litapiga hatua zaidi.

Ifike mahala wachezaji wa kila timu waone ushindani ni wa haki. Watapambana zaidi. Sio kuona kama wakicheza na timu fulani wataonewa.

Pia, waamuzi lazima wawalinde wachezaji mahiri. Tuliona kilichotokea kwa Henock Inonga. Ilibaki kidogo tu avunjike mguu pale Uwanja wa Uhuru.

Mchezaji anacheza faulo za makusudi akijua refa hatafanya chochote. Angalau kwa Inonga mwamuzi Ahmed Arajiga alitoa kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Usalama wa wachezaji ni kitu muhimu sana. Lazima wacheze kwa kulindana. Lazima waamuzi wawalinde.