MTU WA MPIRA: Simba hii tumwachie Mungu

SIMBA imeanza kutema bungo huko Ligi Kuu. Vijana wa kisasa wanasema imelowa.

Majuzi imeacha alama pale Mbeya. Lakini huu ni mwendelezo wa kushindwa kufanya vizuri katika mechi muhimu.

Msimu huu imepoteza mchezo mmoja tu dhidi ya Azam FC. Lakini ilipata sare dhidi ya KMC, Singida Big Stars na sasa Mbeya City. Zilikuwa mechi muhimu sana kwa Simba kushinda, lakini hawakuweza kufanya hivyo.

Bahati mbaya ni kwamba wakati Simba inadondosha alama, wapinzani wao Yanga wanashinda mechi zao. Hii sasa inatengeneza wigo mkubwa wa alama kileleni.

Sare anazopata Simba zinamuweka katika hali ngumu ya kurejesha ubingwa pale Msimbazi. Mpaka sasa inabidi Yanga ipoteze angalau michezo miwili ndipo Simba ipate ahueni. Inawezekana kweli? Sijui.

Lakini pamoja na yote, swali la Msingi ni kwamba Simba imefikaje katika hali hii? Hapa ndipo kwenye tatizo la msingi. Simba kuna mahali walikwama ndio sababu leo wako hapa.

Kwanza walifeli katika usajili. Kati ya wachezaji saba waliosajiliwa Simba ni Augustine Okrah na Moses Phiri tu wameweza kujihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza.

Bahati mbaya zaidi ni kwamba hao wengine licha ya kukosa nafasi katika kikosi cha kwanza hawana hata msaada wakitokea benchi. Inashangaza sana.

Yule Mzungu Dejan baada ya kiwango duni mwanzoni mwa msimu, alikimbia mapema. Na wala hakuna aliyejali. Unajua kwanini? Ni kwa sababu hakuwa na maajabu yoyote.

Sasa matokeo yake Simba imekuwa na kikosi cha kwanza imara, lakini nje hakuna mtu wa maana. Tutamlaumu sana Juma Mgunda kwa kuendelea kumpanga Kibu Denis. Kama siyo Kibu ni nani?

Benchi la Simba ni jeupe sana. Hasa katika eneo la ushambuliaji. Matokeo yake akitoka John Bocco ataingia Kibu Denis. Mchezaji fulani wa mchongo.

Mshambuliaji ambaye anasifika zaidi katika kukaba. Wakati kina Ayoub Lyanga, Sixtus Sabilo wakisifika kufunga na kutoa pasi za mwisho, Kibu anasifika kukaba. Inachekesha sana.

Vipi asipokuwepo Sadio Kanoute. Nafasi yake atacheza Jonas Mkude ama Victor Akpan. Huyu Akpan ni mchezaji mzuri wa kawaida. Simba walihadaika na zile pasi zake pale Coastal Union, lakini ukweli mchungu ni kuwa siyo mchezaji wa daraja lao.

Mkude amechoka. Nadhani pengine sababu ya kucheza mfululizo kwa miaka mingi ama umri umeanza kumtupa mkono. Yupo unga kwelikweli. Anajitengea kieneo chake na kucheza anavyojisikia yeye.

Hayupo fiti tena kucheza kwa dakika 90. Lakini sasa kama Kanoute hayupo ungetaka acheze nani mwingine. Yupo Mkude na ndiye chaguo lililobaki kwa Mgunda.

Kwa upande wa mastraika Simba ndio imefeli zaidi. John Bocco siyo mchezaji wa kumtegemea sana. Naye amecheza muda mrefu. Pia ana majeraha ya mara kwa mara.

Tangu msimu uliopita Bocco amefunga mabao sita tu. Ni pungufu ya mabao aliyofunga Mayele msimu huu peke yake. Sasa utawezaje kushindana na Yanga.

Mchezaji pekee hatari pale mbele ni Moses Phiri. Bahati mbaya naye amepoteza fomu yake hapa karibuni. Ukame wa mabao unamwandama kama mgawo wa umeme unavyoiandama nchi.

Matokeo yake Simba sasa inahangaika kufunga. Nje yupo nani? Habibu Kyombo. Ni mchezaji mzuri, lakini bado hapaswi kuwa tegemeo.

Wachezaji aina ya Kyombo pale Yanga wapo wengi na hawapati hata nafasi. Kina Yusuph Athuman, Crispin Ngushi na wengineo. Lakini pale Simba watu wanataka Kyombo acheze na afunge. Ni ajabu sana.

Hivyo lazima Simba ikubali kuwa ilifeli sokoni. Imeshindwa kupata wachezaji mahiri wa kuifanya timu kuwa hatari zaidi.

Tumeona hili zaidi alipokosekana Clatous Chama. Timu ilikosa ubunifu kabisa. Hakuna mchezaji wa angalau kufanania kile anachofanya Chama. Timu ikawa katika hali mbaya.

Tutamlaumu sana Mgunda lakini kwa kikosi kile hata akaroge Kwamsisi hakuna maajabu makubwa yatapatikana. Simba ikikutana na mechi ngumu itadondosha tu alama. Hasa hizi mechi za mikoani.

Simba pia ilifeli katika benchi la ufundi. Haikuwa bahati mbaya wakaangukia kwa Juma Mgunda. Walikwama na hawakuwa na chaguo zaidi.

Mapema hapa walimleta Zoran Maki. Ni kocha mzuri, lakini hakuwa anaendana na falsafa ya Simba. Uamuzi wake ulikuwa mgumu mno. Unawezaje kukaa na kocha ambaye ana wasiwasi hadi na kiwango cha Chama.

Bahati mbaya huyu ndiye alishiriki kuandaa timu mwanzo wa msimu. Akaondoka wakati mashindano ndiyo yameanza tu. Iliwavuruga Simba hapa. Wangefanya nini?

Kimbilio la haraka likawa Juma Mgunda. Walimchukua kwa ajili ya mashindano ya CAF. Akafanya vizuri wakamwachia na ligi. Sasa unajiuliza Mgunda amewahi kushinda nini hadi utegemee kuwa ataipa Simba ubingwa?