Hizi ndizo mechi za Wiki ya Mwananchi
Muktasari:
- Tamasha hilo huchagizwa na wasanii mbalimbali ambao hujitokeza kwenye Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kutoa burudani zaidi kwa mashabiki, huku pia hutumika kucheza mechi ya kirafiki, kwa ajili ya kuangalia nyota wapya kwa msimu wa 2026-2027.
BAADA ya kushuhudia jana burudani ya tamasha la Simba Day kwa klabu ya Simba, leo ni zamu ya watani zao wakuwa wa jadi, Yanga ambao wanafanya pia kilele cha 'Wiki ya Mwananchi', itakayofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini, Dar es Salaam.
Tamasha hilo huchagizwa na wasanii mbalimbali ambao hujitokeza kwenye Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kutoa burudani zaidi kwa mashabiki, huku pia hutumika kucheza mechi ya kirafiki, kwa ajili ya kuangalia nyota wapya kwa msimu wa 2026-2027.
Mwanaspoti linakuletea orodha na matokeo ya mechi zote saba za nyuma ambazo Yanga imecheza tangu tamasha hilo kubwa na la kuvutia nchini lilipoasisiwa rasmi mwaka 2019 chini ya uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mshindo Msolla.
Katika mechi hizo saba, Yanga imeshinda nne, ikitoka sare moja na kupoteza mbili, huku ikifunga mabao manane na kuruhusu sita.
YANGA 1-1 KARIOBANGI SHARKS FC (2019)
Hii ni mechi ya kwanza ya kilele cha tamasha la 'Wiki ya Mwananchi', tangu lilipoasisiwa mwaka 2019, chini ya uongozi wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla na ilicheza dhidi ya Kariobangi Sharks FC ya Kenya, Agosti 4, 2019.
Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Kariobangi ilipata bao la utangulizi dakika ya 49 kupitia kwa Patrick Otieno, kisha dakika ya 57, Patrick Sibomana aliisawazishia Yanga kwa penalti na kuisha sare ya 1-1.
YANGA 2-0 AIGLE NOIR FC (2020)
Mechi hii ya kuvutia iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini, Dar es Salaam, Agosti 30, 2020, Yanga iliifunga Aigle Noir FC ya Burundi mabao 2-0, huku ikionyesha soka nzuri chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mserbia Zlatko Krmpotic.
Mabao hayo yalifungwa na Tuisila Kisinda 'TK Master', dakika ya 39, akimaliza pasi ya Feisal Salum 'Fei Toto' anayecheza kwa sasa Azam FC na Mghana Michael Sarpong dakika ya 51, kwa kichwa akitumia vizuri krosi iliyopigwa na Ditram Nchimbi.
YANGA 1-2 ZANACO (2021)
Baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Aigle Noir ya Burundi, msimu uliofuatia Yanga ikaduwazwa kwa kuchapwa 2-1, dhidi ya Zanaco FC ya Zambia, katika mechi kali na ya kusisimua iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Agosti 29, 2021.
Mshambuliaji Mkongomani Heritier Makambo aliifungia Yanga bao la utangulizi dakika ya 30 ya mechi hiyo baada ya kuwapiga chenga za fedheha mabeki wa Zanaco FC, akipokea pasi nzuri ya aliyekuwa kiungo wa kikosi hicho, Feisal Salum 'Fei Toto'.
Baada ya bao hilo, Zanaco ilijibu mapigo ambapo winga wa timu hiyo, Ackim Mumba alisawazisha dakika ya 60, kisha kiungo Kelvin Kapumbu kufunga la ushindi dakika ya 76 na kuzima kabisa shangwe la maelfu ya mashabiki wa Yanga waliofurika kwa Mkapa.
YANGA 0-2 VIPERS (2022)
Agosti 6, 2022, Yanga ilifanya vibaya tena katika sherehe hizo baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Vipers ya Uganda.
Mechi hiyo iliyoshuhudiwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, mabao ya Vipers yalifungwa na kiungo, Milton Karisa dakika ya kwanza tu na Anukani Bright akafunga la pili dakika ya 64.
Vipers iliyokuwa mabingwa wa Ligi Kuu Uganda ilikuwa chini ya kocha mkuu raia wa Brazili, Roberto Oliveira 'Robertinho' na baada ya kuipa mafanikio hayo, aliondoka na kujiunga na Simba Januari 3, 2023, ingawa alitimuliwa Novemba 7, 2023.
YANGA 1-0 KAIZER CHIEFS (2023)
Katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa Yanga ikiwa na benchi jipya la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Muagentina Miguel Gamondi, iliifunga Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini bao 1-0, Julai 22, 2023, lililofungwa na mshambuliaji, Mzambia Kennedy Musonda.
Musonda alifunga bao hilo dakika ya 45+1, akimalizia pasi ya Maxi Mpia Nzengeli, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ikiwa ni ushindi wa pili kwa Yanga, baada ya ule wa mabao 2-0, dhidi ya Aigle Noir ya Burundi, Agosti 30, 2020.
Tamasha hili lilinogeshwa na mastaa wengi huku aliyeteka hisia za wengi ni aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mahlatsi Makudubela 'Skudu' ambaye alisajiliwa na kikosi hicho akitokea Klabu ya Marumo Gallants ya kwao Afrika Kusini.
YANGA 2-1 RED ARROWS (2024)
Safari hii Yanga iliialika Klabu ya Red Arrows iliyotoka kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Zambia (MTN Super League) msimu wa 2023–2024, ikiwa na pointi 71, baada ya kushinda mechi 21, kati ya 34 iliyocheza, sare minane na kupoteza mitano tu.
Red Arrows ilichukua Kombe la ABSA 2024 huko kwao Zambia, huku ikichukua pia ubingwa wa Michuano ya Kombe la Kagame 2024 jijini, Dar es Salaam, baada ya kuifunga APR ya Rwanda kwa penalti 10-9, baada ya sare ya bao 1-1, ndani ya dakika 120.
Katika mechi hiyo, Red Arrows ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji, Ricky Banda dakika ya sita, kisha Mudathir Yahya akaifungia Yanga dakika ya 64 na Stephane Aziz KI akafunga la pili la ushindi kwa penalti dakika ya 90.
YANGA 1-0 BANDARI FC (2025)
Tamasha hili lililofanyika Septemba 12, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda tena kwa bao 1-0, dhidi ya Bandari FC kutokea Kenya, lililofungwa dakika ya pili tu na nyota wa kikosi hicho, Celestin Ecua.
Ecua raia wa Ivory Coast, alijiunga na timu hiyo kwa ajili ya msimu wa 2025-2026, akitokea Zoman FC na alionyesha kiwango kizuri katika tamasha hilo na kuwavutia mashabiki wa kikosi hicho zaidi ya 60,000, waliojitokeza uwanjani hapo.
Kabla ya kujiunga na Yanga kwa ajili ya msimu wa 2025-2026, Ecua alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa msimu (MVP) wa 2024-2025 wa Ligi Kuu ya Ivory Coast, baada ya kuchangia mabao 27 ya Zoman FC, akifunga mabao 15 na kuasisti pia mengine 12.
Licha ya kiwango bora alichokionyesha akiwa na Zoman FC na katika tamasha la kilele cha 'Wiki ya Mwananchi', ila Ecua alishindwa kutamba na kikosi hicho, ambapo dirisha dogo la Januari 2026, alijiunga na JS Kabylie ya Algeria kwa mkopo.
YANGA Vs FC LES AIGLES DU CONGO (2026)
Licha ya kushuhudiwa burudani zitakazotolewa leo na wasanii mbalimbali, ila hitimisho la mwisho litakuwa pamoja na mechi ya kirafiki, ambapo mwaka huu wa 2026, Yanga itacheza dhidi ya kikosi cha FC Les Aigles du Congo kutoka nchini DR Congo.
Mashabiki wa Yanga wana hamu ya kuwaona nyota wapya waliosajiliwa na kikosi hicho kwa ajili ya msimu wa 2026-2027, ambao ni Juma Issa Abushiri aliyetokea Fountain Gate, Erick Mwijage akitokea KMC FC na Suleiman Mbarouk 'Mpemba D' (JKU FC).
Wengine ni Abdulnasir Assa 'Gamal', Mohamed Mussa, Hussein Juma Mihambo wa Mashujaa, Housseine Zakouani (Al-Zulfi SFC), Albert Kangwanda (Red Arrows FC), Oumar Farouk Comara (Golden Arrows FC) na Cheikh Ibrahima Toure (Al-Jabalain FC).
Pia, wamo kiungo mkabaji, Fred Duval Ngoma aliyetokea Olympique de Safi ya Morocco, huku miongoni kati ya sajili hizo zinazosubiriwa kwa hamu ni ya mshambuliaji nyota, Peter Shalulile aliyeachana na Mamelodi Sundowns FC ya Afrika Kusini.