Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Komara atapenya kwa Bacca na Mwamnyeto Yanga?

KUJILI 05

Muktasari:

  • Uwepo wa mabeki hao wazawa ambao pia ni tegemeo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars umekuwa mwiba kwa mabeki wa kati wa kigeni kwa takribani msimu wa nne sasa.

Komara karibu jangwani.. lakini nafasi yako ina mlango mgumu sana! Hivyo ndivyo ambavyo Farouk Komara anavyoweza kuambiwa baada ya Yanga kumtambulisha beki huyo wa kati kutoka Golden Arrows ya Afrika Kusini, akitua kwenye eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa na utawala wa wazawa watatu Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ na Dickson Job.

Hapa ndipo penye kazi kubwa kwa Komara. Si kwamba Yanga haina nafasi ya kuongeza beki wa kati, bali tatizo ni mabeki hao watatu wamekuwa na kiwango na kuaminika kiasi ambacho hata wageni waliowahi kufika Jangwani wakiwa na CV nzuri walijikuta wakitumia muda mwingi kuangalia mechi kutoka nje.

Uwepo wa mabeki hao wazawa ambao pia ni tegemeo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars umekuwa mwiba kwa mabeki wa kati wa kigeni kwa takribani msimu wa nne sasa.

KOMA 05

HISTORIA YA WAGENI

Historia inawakataa mabeki wa kigeni kwenye nafasi hiyo, ipo mifano ya mabeki ambao walikotoka walikuwa na kiwango kizuri lakini baada ya kufika Yanga walishindwa kuonyesha ubora wao kutokana na utatu wa wazawa.

Miongoni mwa mifano hiyo ni Gift Fred ambaye alikuwa na kiwango bora alipokuwa Sports Club Villa ya Uganda lakini alipofika Tanzania alikuwa kama mtazamaji tu mbele ya mabeki hao.

Mamadou Doumbia alifika Jangwani akiwa ametoka kuonyesha kiwango kizuri kwenye michuano ya CHAN na akapewa matumaini makubwa, lakini akashindwa kuwatoa kwenye nafasi zao.

Hata Frank Assinki, aliyesajiliwa baada ya kuonyesha kiwango Singida Black Stars, alikumbana na mtihani huohuo ingawa kidogo alikuwa anapata nafasi ya kuanza.

Kwa hiyo Komara anatakiwa kuelewa mapema kusajiliwa Yanga si sawa na kupewa jezi ya kikosi cha kwanza. Atalazimika kuonyesha kwenye mazoezi. Kila siku atakuwa anapimwa katika namna anavyokabiliana na washambuliaji, mipira ya juu, mipira ya chini, kujenga mashambulizi kutoka nyuma na zaidi ya yote uwezo wa kuwa na utulivu wakati timu ikiwa kwenye presha. Kama ataonyesha ubora unaomfanya kocha kuona tofauti kati yake na waliopo anaweza kupata nafasi.

KOMA 02

JOB

Hata hivyo, Komara anaweza kuwa na nafasi ambayo mabeki waliopita hawakuipata. Dickson Job bado hajarejea kikamilifu baada ya jeraha lililomuweka nje, hivyo mwanzo wa msimu unaweza kumpa Komara nafasi ya kuonyesha kile alichonacho.

Hii haimaanishi nafasi ni yake moja kwa moja maana kama Job atarejea na kiwango chake, Komara atahitaji kuendelea kuonyesha ubora ili asiishie kuwa suluhisho la muda. Lakini akitumia vizuri kipindi hiki, anaweza kujitengenezea nafasi ya kuwa sehemu ya pacha mpya ya ulinzi.

KOMA 04

CHAGUO LA KOCHA

Kocha Manqoba Mngqithi ambaye ni raia wa Afrika Kusini si mgeni wa Komara kwani kabla ya kuhamia Yanga alikuwa akiifundisha Golden Arrows, ambako alimaliza msimu wa 2025/26 akiwa kwenye nafasi ya sita ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Hiyo inaweza kuwa faida kidogo kwa Komara kwa sababu kocha anamjua mazingira ya soka la Afrika Kusini, ingawa haimaanishi atapewa nafasi kwa upendeleo. Mngqithi mwenyewe atataka kuona kile ambacho beki huyo anaweza kukifanya ndani ya mfumo wake.

KOMA 03

Kiufundi Komara ana mitihani miwili: kwanza kuivunja himaya ya Mwamnyeto, Bacca na Job; pili, kumshawishi Mngqithi yeye ni sehemu ya suluhisho la Yanga, si kuongeza tu idadi ya mabeki.

Hili ni eneo ambalo Yanga imekuwa ikilinda kwa ubora mkubwa. Utatu huo umecheza pia katika kikosi cha Taifa Stars, hivyo wamezoeana kwa muda mrefu na wana uelewa mkubwa wa kucheza pamoja. Hapo ndipo Komara anatakiwa kwenda hatua moja zaidi; si kuwa mzuri peke yake, bali kuonyesha akiwa na mmoja wao, Yanga inaweza kupata pacha yenye ubora zaidi.

Kama atafanya hivyo, Yanga inaweza kupata faida kubwa. Badala ya kuwa na mabeki watatu wanaogombea nafasi, Komara anaweza kuongeza ushindani na hata kulazimisha kocha kufanya maamuzi magumu mechi baada ya mechi.

Lakini kama atakuja na kiwango cha kawaida, historia ya Doumbia, Gift Fred na Assinki inaweza kujirudia. Hivyo, Komara anaingia Jangwani akiwa na jina jipya, lakini mtihani wake ni ule ule uliowashinda wengi waliomtangulia kuvunja ufalme wa mabeki wazawa na kujifanya sehemu ya kwanza ya mipango ya Yanga.