Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MTU WA MPIRA: Kocha Azam FC anajichimbia kaburi lake mwenyewe

AZAM FC imeamua kujiimarisha vilivyo kuelekea msimu mpya wa mashindano. Huhitaji kuwa na elimu ya Chuo Kikuu kuweza kuona hili kwani matajiri wa Chamazi wameamua.
Walianza kama utani kwa kumsajili Feisal Salum 'Fei Toto' muda mchache tu baada ya Yanga kukubali kumuuza. Wakavunja benki na kulipa mamilioni ya fedha kumchukua.

Nani alifikiria hili? Hakuna. Ilionekana kama Azam FC isingeweza kumnunua mchezaji tegemeo wa Yanga lakini wamefanya hivyo kwa Fei Toto tena akiwa katika kiwango bora kabisa.
Haya ndiyo maboresho tunayozungumza. Wakarejea mezani na kusafisha benchi lao la ufundi. Wakawatoa hadi watu walioaminika kuwa ni vigumu kuwang'oa kwenye viunga vya Chamazi. Wakamtoa rafiki yao, Kally Ongala baada ya kushindwa kuwa na msimu bora.

Ongala ni rafiki yao mkubwa. Wana historia kubwa pamoja nje ya soka, lakini wamempa mkono wa kwaheri. Nani alidhani kama Aggrey Morris angeweza kupewa mkono wa kwaheri baada ya miaka 14 klabuni hapo? Ni ngumu, lakini Azam wamemwambia akatafute maisha mengine nje ya Chamazi.

Ni hivyo hivyo walivyofanya kwa watendaji wengine wa benchi la ufundi. Lakini kabla ya hapo miezi miwili nyuma walishamtangaza Yusuf Dabo kuwa kocha wao mpya kuanzia msimu huu mpya wa mashindano. Walijipanga mapema.
Dabo ametaka kuja na watu wake na Azam FC wamempa.

Ameleta Wasenegali kadhaa wa kumsaidia pale Chamazi. Ameleta wachezaji pia kutoka Senegal. Wamempa na wachezaji wengine aliowataka.
Kocha wa makipa, Khalifa Abubakar anatoka Senegal. Mtaalamu wa video anatoka Senegal. Wamemleta kocha msaidizi mwenye uzoefu mkubwa, Bruno Ferry raia wa Ufaransa pia wakampa kocha wa viungo, Jean Laurent kutoka huko huko Ufaransa.
Benchi la ufundi kwa Azam FC sasa lina watendaji 14, lakini saba kati ya hao wanahusika moja kwa moja na masuala ya ufundi. Ni wengi sana kwa timu za Afrika.

Timu nyingi kwenye Ligi yetu zina makocha watatu tu. Ni kocha mkuu, msaidizi wake pamoja na kocha wa makipa. Katika timu nyingine kocha wa makipa ndiye msaidizi wa kocha mkuu.
Timu zinakwenda kwa kuungaunga. Hata hivyo pale Chamazi mambo ni tofauti. Kocha wa makipa naye ana msaidizi wake. Inavutia sana.

Uzuri wa Dabo ni kocha wa kisasa na anajua anachokifanya, ametaka wachezaji wengi waletwe kwa mapendekezo yake, na wameletwa. Ni kama huyu straika, Diao. Ni mwili jumba. Ni ngumu sana kumpa dhamana kama anaweza kuwa mchezaji hatari kwenye Ligi yetu.

Lakini Azam FC wamekubali matakwa ya Dabo, amewaambia anapenda washambuliaji wenye nguvu na ndiyo sababu amependekeza Idris Mbombo abaki na wamlete huyo Diao. Wakampa.

Akamtaka Gibril Sillah ambaye wamewahi kufanya kazi pamoja huko Senegal kabla hajauzwa kwenda Raja Casablanca. Azam FC wamemleta pale. Watu wameshangaa Azam FC inawezaje kusajili mchezaji Raja? Ila wameweza.
Ametaka kambi katika eneo tulivu na wamempeleka huko Tunisia, wanakwenda kukaa huko kwa wiki tatu. Atapewa kila kitu anachotaka, Azam FC wameamua kufungua moyo na kumwamini Dabo. Ni kocha mzuri na anajiamini.
Wasiwasi wangu ni kwamba Dabo ameamua kujitwisha mzigo mzito peke yake. Amejenga imani kubwa kwa mabosi kuwa msimu ujao anakwenda kushindania ubingwa na kupambana kwenye mashindano ya Kimataifa. Nao wameweka imani kubwa kwake.

Ni ngumu kusema chochote kwa sasa ila wengi tunaamini kuwa matatizo ya Azam FC ni zaidi ya hivi vinavyoonekana. Kama ni makocha walishakuja wazuri kuliko Dabo. Kama ni wachezaji walishakuja wazuri kuliko Diao. Nini kilitokea? Ni majanga.
Kama ni maandalizi makubwa Azam FC mwaka jana waliweka kambi kwenye mji wa Kitalii wa El Gouna pale Misri. Hata hivyo walimtimua kocha wao wiki chache tu baada ya kurejea. Hakuwa na jipya na walimpa pia kila kitu kama Dabo.
Nadhani Dabo alipaswa kuchunguza tatizo la msingi zaidi pale

Chamazi. Kwanini wachezaji wa Azam FC hawajitumi kama wa Simba na Yanga? Kwanini Azam FC inapata shinda kwenye mechi za mikoani? Ni matatizo ambayo yamekuwa yakiitafuna timu yao kila siku.

Fiston Mayele alisema wachezaji wa Azam FC wanakamia mechi kubwa lakini mechi ndogo wanacheza kawaida. Alitolea mfano namna walivyocheza hovyo dhidi ya Namungo. Huyu ni mchezaji wa Yanga lakini ameona tatizo pale Chamazi.
Wachezaji wa timu kubwa wanatakiwa kucheza kwa ubora ule ule kila siku. Hii haipo pale Chamazi, leo watacheza vizuri, kesho watakuangusha. Ni kwanini? Wanajua wenyewe.

Bahati mbaya Dabo amechagua njia yake. Anaamini kuwa akipewa kila kitu ni rahisi kufanikiwa. Ni vizuri kama itakuwa hivyo, lakini mambo yakienda tofauti kidogo tu ajira yake itakuwa shakani. Lawama zote zitakwenda kwake moja kwa moja.

Ubaya wa soka la Tanzania watu wanataka vitu viwili. Wanataka timu icheze soka safi na ishinde mechi. Ikitokea unashinda tu bila soka safi, bado watalalamika. Ndivyo Watanzania tulivyo. Ni wakati sasa wakusubiri jipya atakalokuja nalo Dabo.