Nyota Azam FC wafungiwa darasani

Muktasari:

  • Daktari wa timu hiyo, Mwanandi Mwankemwa alisema moja ya somo ambalo wachezaji wamepewa juzi na jana ni pamoja na namna ya kuokoa maisha ya mchezaji mwenzake uwanjani.

WACHEZAJI wa Azam FC tayari wameingia kambini kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara huku kazi ya kwanza ilikuwa kupima afya zao.

Baada ya kupima afya wachezaji hao walikuwa wakipewa elimu mbalimbali ikiwa mchezaji anahitaji msaada haraka uwanjani kabla daktari hajafika.

Daktari wa timu hiyo, Mwanandi Mwankemwa alisema moja ya somo ambalo wachezaji wamepewa juzi na jana ni pamoja na namna ya kuokoa maisha ya mchezaji mwenzake uwanjani.
Alisema wachezaji wa ligi zilizoendelea mchezaji anapoanguka mtu wa kwanza kumpa huduma ya kwanza anakuwa mchezaji mwenzake aliyekuwa karibu na hii ni sababu wanapewa elimu.

"Uwanjani ni eneo la kazi kama ilivyo sehemu nyingine hivyo kunaweza kutokea mchezaji akajigonga sehemu na akahitaji msaada wa haraka hivyo lazima wawe na elimu hiyo.

"Mfano mchezaji anapoanguka mtu anayehitaji kuwa wa kwanza kumsaidia ni mwenzake hivyo kama hana elimu ya huduma ya kwanza haitasaidia kitu ndio maana hawa wetu tunawafundisha," alisema Mwankemwa.

Mwankemwa aliongeza wachezaji wa Azam FC lazima wafanyiwe vipimo kabla ya kuanza kwa ligi ikiwa pamoja na kusisitiza uwepo wa bima kwa kila mchezaji.
Alisema pamoja na vipimo wachezaji watapewa mafunzo maalumu ya kufanya pale inapotokea dharula uwanjani kama mchezaji ameumia au kazimia ghafla.

"Pia wachezaji wetu tunawafundisha namna ya kunyanyua mapigo ya moyo 'Cardio Pulmonary Resuscitation (CPR) kabla dokta hajafika uwanjani inapotokea tatizo lazima uweze kumsaidia mwenzako haraka kwa kumpa huduma ya kwanza."

Azam FC imemaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu iliyomalizika hivi karibuni na ni miongoni mwa timu nne zitakazoshiriki michuano ya kimataifa, Simba na Yanga Ligi ya

Mabingwa wakati Azam na Singida Kombe la Shirikisho.
Katika kuimarisha kikosi chake Azam imeachana na wachezaji zaidi ya 10 huku tayari ikiongeza nyota kadhaa akiwemo, Feisal Salum 'Fei Toto' akitokea Yanga.