Msiwape presha wachezaji mechi za Yanga na Simba
Muktasari:
Si muda mrefu sana ulipita, Yanga ilifungwa na Simba mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
KUMBUKUMBU mara zote huwa na umuhimu wa kipekee. Wiki iliyopita, Yanga walifungwa na watani wao wa jadi Simba bao 1-0.
Si muda mrefu sana ulipita, Yanga ilifungwa na Simba mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
Simba kwa siku za karibuni imekuwa ikiifunga sana Yanga, ndugu zanguni mtaniwia radhi kwa haya makala ya leo, nitawarudisha nyuma kiasi.
Ni makala ambayo yatawagusa watu hapa na pale, lakini kwa sababu ni mafundisho pia kwa vijana ambao ni chipukizi, wazazi na viongozi pia, natumaini itaweza kuwapa somo.
Mimi, Boniface Ambani mwandishi wa makala haya niliwasili Tanzania nikitokea India nilikokuwa nikisakata soka katika Klabu ya Salgaocar.
Wakati nasajiliwa, Yanga ilikuwa imepitisha miaka mingi bila ya kuifunga Simba.
Hayo yote hayakunitisha, nilikuwa na uzoefu wa mechi kama hizo, Kenya nishawahi kukipiga katika mechi kati ya watani wa jadi, AFC Leopards na Gor Mahia, timu hizi za Kenya nazo zina uhasama kama Simba na Yanga. India nako kuna East Bengal na Mohun Bagan.
Kwa hivyo kwangu halikuwa jambo geni, nakumbuka baadhi ya magazeti yalianza kuikashifu Yanga na kuhoji ni vipi wanachukua mchezaji kutoka India.
Wakati huo Simba ilikuwa imewanasa wachezaji kutoka Nigeria kina Emeh Ezechukwu na Orgi Obinna. Kwa hiyo kusajiliwa kwangu hakukuwa na mbwembwe. Hata hivyo, nilimwomba Mungu anipe nguvu na hekima ya kuweza kufanya kazi zangu vyema.
Historia ya Yanga na Simba nilikuwa naifahamu kwa hiyo halikuwa tatizo kwangu. Ligi Kuu ya Vodacom Bara ilipoanza nakumbuka mechi yangu ya kwanza ilikuwa dhidi ya Prisons ambayo tulishinda kwa mabao 4-0 mimi nikifunga mawili, mengine yalifungwa na Ben Mwalala na Shamte Ali.
Baada ya hapo nikajitangazia rasmi kuanza kufukuzia kiatu cha dhahabu, nilifunga mechi saba mfululizo, waliokuwa wakiikashifu Yanga imesajili mchezaji kutoka India wakatii amri.
Mechi na Mtibwa Sugar sikucheza, nilikuwa na jeraha, tukatoka sare ya 0-0 mjini Morogoro, mechi iliyofuata ilikuwa ya Simba na Yanga.
Hapo sasa nikatambua umuhimu wa mechi hiyo, Yanga kukawekwa ulinzi mkali katika Hosteli ya Lamada, haikuchukua muda tukaenda Pemba na Simba wakaenda Unguja, kila timu ililikimbia jiji.
Nilipouliza nikaambiwa mababu wamedai tufanye hivyo, ulinzi ulikuwa mkali kila mahali, mara tukarudi jijini na kuwekwa kwenye hoteli ya kifahari ya New Africa.
Kwangu hayo yote niliona kama nikuwatia presha wachezaji, sikuona maana ya kuwazungusha wachezaji hivyo.
Kumbuka mechi ya aina hiyo inahitaji utulivu, wakati wakihangaika mimi akili zangu zote nilikuwa nimezielekeza kwenye mechi, sikuwa na presha zozote.
Nikajaribu niwezavyo kujiondoa katika presha, matayarisho yangu ya hiyo mechi yakawa ya kawaida tu ingawa nilijua umuhimu wa kupata ushindi.
Viongozi ndio wanaowafanya wachezaji kuwa na presha, mara hoteli hii kesho nyingine mara babu kasema, kibaya zaidi ni kwamba na wachezaji wanaingia katika mambo hayo ya ushirikina na kusahau kwamba mechi huchezwa kwa bidii ya mchezaji mwenyewe.
Kama mchezaji, akili zako ni kuwa bila kutumia nguvu za giza, nguvu za mababu hauwezi kushinda basi hapo ni tatizo lako.
Cha pili kwa viongozi wao, wameshazoea ushirikina, timu ikishinda inakuwa ni mababu ndio wamefanya ikashinda na si juhudi za wachezaji.
Hii inaudhi sana, timu ikikosa ushindi inakuwa ni wachezaji ndio wabaya, ni kwa nini msiwalaumu mababu kwa kupoteza mechi.
Nikirejea mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza kwangu dhidi ya Simba, mengi yalifanyika nikishuhudia na mwisho wa yote tuliifunga Simba bao 1-0, bao lililofungwa na Ben Mwalala baada ya kupata pande la uhakika kutoka kwangu katika dakika ya 11.
Sikumaliza mechi hiyo, niliumia dakika ya 43, jeraha lililonifanya nisiendelee lakini tulipata ushindi uliotokana na bidii za wachezaji waliojitolea.
Jambo kubwa uwanjani ni kujitolea si kutegemea babu akusaidie kupata ushindi, wakati nikiwa Yanga nilikuwa na muda wa kuwafahamisha wachezaji wenzangu kuwa ushirikina hauna nafasi katika soka.
Soka ni bidii yako na akili itakayokuokoa ingawa ilikuwa vigumu lakini nilijaribu niwezavyo kuwafahamisha kuwa unapoondoka Tanzania kwenda kufanya majaribio Ulaya au Arabuni hautaenda na babu ili akupigie ramli.
Nikirejea upande wa viongozi, tafadhali punguzeni presha kwa wachezaji mechi hizi zinapokaribia.
Kwangu haya naona ni mambo yaliyopitwa na wakati, acheni kuwapa presha wachezaji, waacheni mechi hiyo waichukulie kama mechi nyingine ya kawaida na hatimaye ushindi utakuja tu.
Wakati yote yakiendelea mimi sikuwahi kujiweka katika presha, pia pamoja nami Yanga tulikuwa na kikosi cha wachezaji mahiri kina Nurdin Bakari, Shadrack Nsajigwa, Godfrey Bonny, Shamte Ali, Mrisho Ngasa, George Owino, Athuman Idd Chuji, Ben Mwalala, Cannavaro na Obren.
Ni wachezaji waliokomaa kisoka, misimu miwili nilicheza Yanga, kati ya mechi nne tulizocheza dhidi ya Simba, tulishinda mbili, tukapoteza moja na sare moja. Viongozi punguzeni presha kwa wachezaji mechi za Yanga na Simba zinapokaribia.