Moshi wakarabati Uwanja wa Ushirika
Muktasari:
- Lazima ipo namna na taarifa zilizotua hapa kijiweni ni kwamba Uwanja wa Ushirika kule Kilimanjaro haukidhi vigezo vya kutumika kwa Ligi Kuu.
TUMEKAA hapa mtaani tunashangaa kuona Polisi Tanzania wanachezea mechi zao za nyumbani za Ligi Kuu katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha badala ya Ushirika uliopo Moshi.
Lazima ipo namna na taarifa zilizotua hapa kijiweni ni kwamba Uwanja wa Ushirika kule Kilimanjaro haukidhi vigezo vya kutumika kwa Ligi Kuu.
Hii sio sawa jamani. Nyie jamaa zetu Wachaga hapa kijiweni waambieni basi wenzenu kule wakarabati huo uwanja ili Polisi Tanzania irudi Moshi badala ya kuchezea mechi zake Arusha.
Majamaa ya Arusha yanafaidi ligi kupitia Polisi Tanzania pasipo kuvuja jasho la kuipandisha kama mlivyofanya nyie watu wa Moshi sasa hili lisiendelee wanangu changamkeni basi.
Kama mliweza kupambana kwa muda mrefu katika Ligi ya Championship na mkaingia gharama kubwa za muda na fedha kuhakikisha timu inapanda Ligi Kuu, hili la kukarabati uwanja haliwezi kuwashinda ndugu zetu.
Halafu sio kwamba Moshi hamna wadau ambao wanaweza kuwasapotini katika suala la ukarabati wa uwanja kama tatizo ni fedha itakuwa tu kuna mahali mnayumba jamaa zetu.
Halafu ujue hiyo timu ikichezea kulekule kwenu Kilimanjaro kuna faida nyingi ambazo mtapata nyie na ndugu zenu ambazo sasa hivi wanazipata watu wa Arusha ambao wakati nyie mnahaha kupandisha timu wao walikuwa hawana hata habari.
Ila jamaa wa Arusha wanaonekana wazuri sana katika kushawishi timu za mikoa mingine zihame vituo vyao na kwenda kwao licha hata ya kutoshiriki katika kuzipandisha Ligi Kuu.
Ilianzia kwa TRA United, ikaja Fountain Gate na sasa Polisi Tanzania. Mungu hakunyimi vyote kwa kweli. Arusha hawawezi kupandisha timu Ligi Kuu ila Mungu kawajalia ushawishi wa kuzivuta kwao timu za mikoa mingine.