Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga vs Coastal mtihani wa miaka 12

Muktasari:

  • Mchezo huo wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa saa 12:30 jioni, unawakutanisha Yanga iliyotoka kuanza msimu kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo ugenini na Coastal Union iliyopoteza bao 1-0 nyumbani dhidi ya Mashujaa katika mchezo wake wa kwanza.

COASTAL Union leo inaingia Uwanja wa KMC Complex uliopo Dar es Salaam ikiwa na kibarua cha kuvunja rekodi ya miaka 12 na siku 357 dhidi ya Yanga, baada ya kupoteza mechi 10 mfululizo ilizocheza ugenini dhidi ya bingwa huyo mtetezi wa Ligi Kuu Bara bila kufunga hata bao moja.

Mchezo huo wa pili wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa saa 12:30 jioni, unawakutanisha Yanga iliyotoka kuanza msimu kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Namungo ugenini na Coastal Union iliyopoteza bao 1-0 nyumbani dhidi ya Mashujaa katika mchezo wake wa kwanza.

Kwa Coastal, kinachoongeza uzito wa mchezo huo ni kwamba katika mechi 11 za mwisho ilizocheza ugenini dhidi ya Yanga, imepoteza 10 mfululizo na kupata sare moja pekee ambayo ni ile ya bao 1-1 iliyopatikana Agosti 28, 2013, ikiwa pia ndiyo mara ya mwisho kwa Wagosi hao wa Kaya walipofunga bao dhidi ya Yanga wakiwa ugenini kwenye ligi.

Tangu sare hiyo, Coastal imekutana na Yanga mara 10 ugenini bila kufunga bao, ikipoteza kwa matokeo ya 2-0, 8-0, 1-0, 1-0, 3-0, 3-0, 3-0, 1-0, 1-0 na 3-0 huku mchezo wa mwisho Mei 9, 2026 ukimalizika kwa Yanga kushinda mabao 3-0.

Kwa jumla, katika mechi hizo 11, Yanga imefunga mabao 24 dhidi ya moja la Coastal, rekodi inayowapa wenyeji nafasi kabla ya mchezo wa leo. Hata hivyo, kwa Coastal, takwimu hizo zinaweza kuwa kichocheo cha kutafuta matokeo tofauti na yaliyopita, hasa baada ya kuanza msimu kwa kipigo.

Kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi ameonekana kutokuwa muumini wa historia na badala yake amesisitiza kuwa bado yupo katika hatua ya kuwatazama wachezaji wake na kutengeneza timu anayoiamini.

“Tunataka kuwafanya wote wafikie kiwango kizuri, lakini katika hatua hii ya msimu ni vigumu kufanya mabadiliko makubwa kwa sababu bado tunaangalia ni aina gani ya wachezaji tunaowahitaji na kila mmoja anaweza kutupa nini,” alisema Mngqithi.

Mngqithi alisema michezo ya mwanzo ya msimu, ikiwamo mitano ya kwanza, inampa nafasi ya kuendelea kuwafanyia tathmini wachezaji wake kabla ya kufanya maamuzi ya kitu kingine.

“Ni vigumu kufanya mabadiliko makubwa katika michezo mitano ya kwanza ya msimu. Bado tunawaangalia wachezaji na kile wanachoweza kutoa kwenye timu,” alisema.

Mngqithi pia aligusia nguvu ya mashabiki wa Yanga katika michezo ya nyumbani, akiwataka kujitokeza kwa wingi na kuiunga mkono timu hiyo, huku akiwataja kama mchezaji wa 12.

Kwa upande wa Coastal Union, Kocha Fikiri Elias anakiri ukubwa wa mtihani unaowakabili, lakini alisema kikosi chake kimejiandaa kuhakikisha kinafanya vizuri dhidi ya Yanga.

“Haitakuwa mechi nyepesi hata kidogo kutokana na aina ya wapinzani ambao tutakutana nao lakini tumejiandaa kuhakikisha tunafanya vizuri, haijalishi nini kilitokea katika mchezo uliopita, hii ni nafasi nyingine ya kujaribu kufanya kitu tofauti,” alisema kocha huyo.

Kabla ya mechi hiyo, leo pia kutakuwa na mchezo kati ya Polisi Tanzania na JKT Tanzania, timu ambazo zote zilianza msimu kwa sare. Polisi ikitoka 1-1 dhidi ya Azam, wakati JKT Tanzania ikitoka sare kama hiyo dhidi ya TRA United. Baadaye, macho yatahamia Chamazi ambako Azam FC itakuwa mwenyeji wa TRA United.

Rekodi ya msimu uliopita inaonyesha Azam na TRA United ziligawana ushindi katika michezo yao miwili, Azam ikianza kwa kuichapa TRA United mabao 2-0 nyumbani, kabla wakusanya kodi hao hawajajibu mapigo katika mzunguko wa pili kwa ushindi wa mabao 4-1.

Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Azam, Florent Ibenge, alisema anafahamu ubora wa TRA United na namna ilivyo muhimu kwa kikosi chake kupata ushindi wa kwanza wa msimu mbele ya mashabiki wake.

“Tulifanya makosa mengi ya kiuchezaji katika mechi yetu ya kwanza, hivyo hii ni nafasi ya kuonyesha namna nzuri ya kuanza msimu,” alisema kocha huyo ambaye aliiongoza Azam msimu uliopita kushika nafasi ya tatu kwenye ligi na kucheza fainali ya CRDB.

Kwa upande wa TRA United, kocha Ettiene Ndayiragije alisema kikosi chake kimejiandaa kupambana na mwenyeji wao huku wakifanyia kazi upungufu ambao ulijitokeza katika mchezo uliopita wa ligi ili waondoke Chamazi na matokeo mazuri.