Prime
Ubingwa wa mezani, wahuni wa CAF wametuvua nguo
Muktasari:
- Vikao vya soka la Afrika, mechi muhimu za Afrika, zote zinafanyika Morocco. Usishangae kusikia Afrika Mashariki imenyang’anywa uenyeji wa michuano ya Afcon na Morocco kupewa jukumu hilo. Kuna mtu anaitwa Fouzi Lekjaa. Makamu wa Rais wa CAF, Waziri wa michezo wa Morocco. Na ni bilionea. Ameiweka CAF mkononi kwa sasa.
TULIKUWA tunasubiri mwezi uandame huku hali ikiwa shwari kabisa. Ghafla wahuni fulani wakakutana ndani ya ofisi fulani pale Morocco na kuamua kuchafua hali ya hewa. Waliamua tu kuliabisha Bara la Afrika. Zamani uhuni ulikuwa unafanyika Misri siku hizi unafanyika Morocco. Mpira wa Afrika umehamia Morocco.
Vikao vya soka la Afrika, mechi muhimu za Afrika, zote zinafanyika Morocco. Usishangae kusikia Afrika Mashariki imenyang’anywa uenyeji wa michuano ya Afcon na Morocco kupewa jukumu hilo. Kuna mtu anaitwa Fouzi Lekjaa. Makamu wa Rais wa CAF, Waziri wa michezo wa Morocco. Na ni bilionea. Ameiweka CAF mkononi kwa sasa.
Tulipotangaziwa Morocco imepewa ubingwa wa Afrika mezani nilitabasamu. Kwamba bingwa sio tena Senegal ila ni Morocco. Fouzi lazima amefanya mambo yake. Ni aibu kubwa kwetu. Kwa mara nyingine tumeendelea kuithibitishia dunia namna ambavyo Afrika ipo nyuma. Tupo nyuma kwa mambo mengi. Unaweza kufikiria bingwa wa Euro au Copa America anaweza kutoka mezani? Hapana. Haitakuja kutokea.
Kwa mujibu wa masela waliokaa mezani kule Morocco waliamua Morocco ipewe ubingwa wa Afrika kwa sababu Senegal waliondoka uwanjani.
Kwa mujibu wa kifungu namba 84 cha mambo yao ya mpira ni timu ambayo imegomea mechi na kuondoka uwanjani inampa nafasi aliye uwanjani kupewa mabao matatu na ushindi. Inachekesha kuona mwamuzi, Jean-Jacques Ndala hakumaliza mechi.
Ndala alisubiri Senegal warudi uwanjani na mechi iendelee. Ndala alipaswa kutumia kipengele hiki kumaliza mechi na Morocco wangepewa ubingwa wao siku ile ile.
Hata hivyo Senegal walirudi uwanjani na mechi ikaendelea. Kwa nini uwaadhibu kwa kanuni ya kugomea mechi wakati pambano liliendelea uwanjani na kumalizika salama?
Ambacho kilipaswa kuheshimiwa baada ya hapo ni ile kanuni inayosema filimbi ya mwamuzi ni ya mwisho katika mchezo wa soka.
Ndala alimaliza mechi wakati Senegal ikiwa imeshinda 1-0. Hakumaliza mechi wakati Senegal wapo vyumbani wakiwa wamegomea mchezo.
Kwa mujibu wa Fouzi na genge lake ni penalti ya Brahim Diaz haikuwa halali. Kwamba ilipigwa baada ya mechi kumalizika. Kwamba bao la Senegal halikuwa halali kwa sababu lilifungwa wakati mechi imemalizika.
Fouzi kaongoza genge lake la wahuni siku 57 baada ya Ndala kupuliza filimbi ya mwisho pale Rabat. Filimbi halali kabisa. Imetutia aibu kwa wenzetu walioendelea ambao mambo kama haya yalikuwa yanafanyika kabla ya vita ya kwanza ya dunia.
Mpira wa Afrika ukidharauliwa na kina Jamie Carragher huwa tunakasirika. Kuna siku ambayo Carragher alidai ubingwa wa Afrika hauwezi kumpa Mo Salah tuzo ya mwanasoka bora wa dunia tukanuna. Alikuwa sahihi. Tulishasau kilichotokea Morocco.
Kilichopaswa ni kufunika kombe ili mwanaharamu apite. Hata wachezaji wa Morocco hawajisikii vizuri kwa kilichotokea majuzi. Kwamba mtu amekaa katika kochi nyumbani anaambiwa yeye ni bingwa katika mechi ambayo ilipita siku 57 zilizopita na timu yake ilipoteza 1-0. Kwamba ghafla mbele ya watoto wake na mkewe anyanyuke na kushangilia?
Nimesoma mahala Achraf Hakimi akidai anaamini pambano lilimalizika siku ile na Senegal walitwaa ubingwa. Nadhani ndio hisia za wachezaji wa Morocco kwa sasa. Sidhani kama wanaweza kukutana katika nyumba ya mmojawapo wakaanza kusheherekea ubingwa. Itakuwa aibu ya mwaka.
Hisia za ubingwa au kupoteza mechi ya fainali zinakuwepo siku ile ile ya pambano. Ndivyo mchezo wa soka ulivyo. Kwamba Senegal warudishe medali? Kwamba wachezaji wa Morocco wapelekewe medali nyumbani? Kwamba ghafla mitaa ya Rabat, Casablanca, Marrakeish na kwingineko walipuke kwa furaha ghafla wakiwa majumbani siku 57 baada ya fainali kupita?
Walichopaswa kina Fouzi na genge lake ni kukubali tu fainali imepita. Na wangekuwa na busara zaidi wangeamua kutengeneza mazingira ya kuhakikisha kilichotokea katika fainali ile hakirudiwi tena.
Kulikuwa na mazingira ya kuipatia Morocco ubingwa. Waamuzi walikuwa wanazinyima penalti timu ambazo zilikuwa zinacheza na Morocco. Hakukuwa na haki.
Bahati mbaya katika hili Morocco wamejijengea chuki kubwa katika kila pembe ya dunia. Wamebaki peke yao tu. Wanapigana vita wakiwa wenyewe tu. Huku nchi za watu weusi hawapendwi. Lakini pia kule Afrika Kaskazini kwa waarabu wenzao hawapendwi. Wote wapo upande wa Senegal. Klabu ya Pharco ya Misri imetangaza kutoshiriki michuano yoyote ya CAF kama Senegal itaendelea kuporwa ubingwa wake.
Kina Fouzi wamejikuta wameleta vurugu katika mpira wetu. Watu walishaanza kusahau habari hizo na walijikita zaidi kutazama mwisho wa ligi mbalimbali duniani kote. Habari za Afcon walishasahau na walijua kwamba haki ilikuwa imetendekea kwa akina Sadio Mane kuvaa medali za ubingwa.
Bahati nzuri Morocco wana timu nzuri tu ya kutwaa ubingwa wa Afcon Dar es salaam mwakani. Kulazimisha lazima wachukue ubingwa siku 57 baada ya fainali ni ujinga ambao hauna maana.
Tumejivua nguo kwa wenzetu ambao siku za karibuni wamekuwa wakifuatilia michuano hii kwa karibu zaidi tofauti na zamani.
Nimewasikia kina Wayne Rooney na Rio Ferdinand. Wametushangaa. Hawa ni watu wazito katika dunia ya soka lakini jicho lao lilikuwa katika michuano hii.
Kuambiwa bingwa amepatikana mezani baada ya siku 57 tangu michuano hii kumalizika ni jambo lililowashangaza. Kwao hakuna bingwa aliyewahi kupatikana mezani kwa staili hii.
Ni sawa sawa leo Liverpool ipokwe pointi nyingi kwa makosa fulani kisha tutangaziwe kwamba bingwa wa msimu uliopita alikuwa Arsenal. Sidhani kama mashabiki wa Arsenal watarukaruka na kushangilia. Wanachosubiri ni ubingwa wa msimu huu ambao wameendelea kuutolea jasho. Huu ndio ubingwa halali kwao.
Lakini kitu kingine cha kujiuliza kwa makini ni kama Morocco wangeshinda pambano lile baada ya Senegal kurudi uwanjani. Hatua hii ingechukuliwa? Kwamba kama Morocco angeshinda bao 1-0 tungeweza kuambiwa kuanzia sasa tusihesabu tena bao moja bali ni mabao matatu? Naamini wangeacha matokeo yawe kama yalivyo na tusingesikia tena habari tofauti.
Sasa kombe limepelekwa katika jeshi la Senegal. Ni aibu tupu na tunaonekana vichekesho. Kinachoweza kufuata kama kina Fouzi watashikilia msimamo wao, itakuwa vurugu zaidi.
Senegal wanaweza kuamua kutoshiriki michuano yote ya CAF. Wanaweza wakaamua wasije Dar es salaam, Kampala au Nairobi mwakani. Nani atawalazimisha? Ukiwafungia pia utaonekana mwendawazimu. Lakini kwa wazimu huu wa kina Fouzi tutegemee tu kuona maamuzi mengi ya kiuwendawazimu.
CAF ya rafiki yetu, Patrice Motsepe imetuvua nguo hadharani dhidi ya dunia ya nje ya Afrika. Wangeacha tu mambo haya na kuwatia Morocco moyo waje kutwaa ubingwa wa Afrika pale Temeke mwakani. Sio mbali sana.