Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MJUAJI: Hii ndio Simba ya 1993 na maajabu yake

KUMBUKA nilishaandika hapa, Simba ilikuwa imetoka Kampala, Uganda baada ya kutolewa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kombe la Kagame).
Mwaka 1993, Simba ilienda Kampala Uganda ikiwa watetezi wa taji ililolitwaa mwaka 1992 kuifunga Yanga kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1 ya muda wa kawaida katika fainali ziliyopigwa visiwani Zanzibar.


ILIANZA KICHOVU
Baada ya kupoteza Kombe la Kagame 1993 nchini Uganda, Simba ilianza kichovu katika mchezo wake wa kwanza ya michuano ya Kombe la CAF ilipovaana na Ferreviario de Maputo ya Msumbiji kwa kutoka suluhu nyumbani. Wengi waliikatia tamaa kwa matokeo hayo wakiamini Simba ingeenda kutolewa raundi ya kwanza, lakini cha ajabu ilipoenda mjini Machava kurudiana na wapinzani wao hao walitoka sare ya 1-1 na bao la ugenini likawabeba kwenda raundi ya pili.
Kwenye mechi za raundi ya pili ya michuano hiyo iliyokuwa ndio kwanza ina mwaka mmoja tangu kuasisiwa kwake mwaka 1992 baada ya mfanyabiashara maarufu nchini Nigeria, Moshood Abiola, Simba ilikutana na Manzini Wanderers ya Swaziland (sasa Eswatini) na ikapata ushindi wa jumla wa mabao 2-0 baada ya kushinda nyumbani na ugenini kwa bao 1-0 kila mechi. Bao la mechi ya nyumbani liliwekwa kimiani na Malota Soma 'Ball Juggler' sekunde chache kabla ya mapumziko.
Matokeo hayo yakaivusha Simba hadi hatua ya robo fainali ikiungana na timu za Gor Mahia ya Kenya, Al Haracch ya Algeria, Mbilinga ya Gabon, Atletico Sports Aviacao (Angola), Insurance (Ethiopia), Zamunta (Niger) na Stella Abidjan (Ivory Coast).
Katika mchezo wa robo fainali Simba ilipangwa kukutana na Waalgeria, Al Harrach na kuing'oa kwa jumla ya mabao mabao 3-2 baada ya awali kushinda nyumbani kwa mabao 3-0 yaliyowekwa kimiani na Edward Chumila 'Edo' aliyefunga mawili na jingine Abdul Ramadhan 'Mashine'. Hata hivyo ilipoenda ugenini ilikandikwa mabao 2-0, lakini ikavuka salama kwenda nusu fainali na kukutana na Atletico Sports Aviacao ya Angola ambao waliiduwaza kwa kuwafumua kwa mabao 3-1.


MVUA KUBWA ANGOLA
Kabla ya mchezo huo, Aviacao ilikuwa imetoka kuing'oa Gor Mahia kwa penalti 4-2 huku kipa wake Kanka Vemba akisifiwa kudaka penalti na sifa zake zilifika nchini haraka kutokana na kuelezwa ndiye aliyeikwamisha K'Ogalo kutinga nusu kwenye pambano lao la robo fainali.
Hata hivyo, Simba ilimaliza kazi mapema dhidi ya ASA na kipa wao huyo kwa kupata ushindi wa mabao 3-1 nyumbani yaliyofungwa na Chumila tena aliyetupia mawili, huku jingine lililokuwa la pili Waangola wakijifunga, huku bao lao la kufutia machozi likifungwa na Nello.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida na iliyoleta utata ni kwamba Simba ilipoenda Angola baada ya miaka mingi sana mvua ilinyesha.  Na mchezo huo, uliisha kwa sare tasa 0-0, huku Waangola wakishindwa kuamini kilichoikuta timu yao na kuamua kufanya fujo za kumrushia chupa na vitu vingine kipa Mohammed Mwameja ili kumzingua kwani ndiye waliyemuona kikwazo kwao tangu Dar.
Baada ya Simba kufanikiwa kuingia hatua ya fainali kwa kuwatoa Waangola hao moja kwa moja ilivyorudi Tanzania wakaingia kambini visiwani Zanzibar
Mfanyabiashara, Naushad Mohammed alihusika kwa kiasi kikubwa kuipa Simba msaada wa hali na mali.
Kuelekea mchezo huo  wa ugenini, Simba ilikumbwa na majeruhi, mshambuliaji wake Edward  Chumila ‘Smile Killer’ alikuwa na tatizo la nyama pamoja na beki wake wa kushoto Deo Mkuki waliukosa mchezo huo muhimu mno kwao.
Kocha Abdallah Kibadeni akisaidiana na Etenne Eshette alilazimika kumtumia mshambuliaji David Mihambo kuchukua nafasi ya Chumila, huku Twaha Hamidu alicheza beki wa kushoto kuziba pengo la Deo Mkuki.
Simba ilicheza vizuri sana na kuibana Stella Abidjan kama sio kukosa umakini kwa Mihambo na Feruz Teru ingeshinda mchezo huo ugenini na kujitengenezea mazingira mazuri katika mchezo wa nyumbani, lakini hadi dakika 90 zilipomalizika matokeo ya timu hizo ilikuwa ni suluhu.


VURUGU ZA VIONGOZI
Hapo sasa ndipo mambo yalipoonza kwani baada ya Simba kurudi tu, viongozi, wanachama na baadhi ya viongozi wa serikali wakaona kama vile kazi ilikuwa imekwisha akili zote zikaelekezwa kwenye maandalizi ya jinsi ya kulitembeza kombe.
Kambi ya Simba pale Zanzibar ilikuwa bize kila siku viongozi wa serikali walitembelea huku kila mmoja akitoa ahadi lengo ni kuwahamasisha wachezaji wafanye vizuri.


MATUMAINI MAKUBWA
Novemba 13 siku ya mchezo uwanja ulifurika watu na viingilio vilikuwa Tsh 50,000 sehemu maalumu, Tsh 10, 000 jukwaa kuu, Tsh 5,000 jukwaa la kijani, Tsh. 1,500 mzunguko
Baada ya mchezo kuanza huku Watanzania wakiwa na matumaini makubwa ya kuona Simba kushinda mchezo huo ilishtushwa na bao la mapema lililofungwa na mchezaji Koume Disire katika dakika ya 17 tu ya mchezo huo.
Uwanja ulikuwa kimyaa (hapa hata wale mashabiki wa Yanga nao walificha makucha yao kwanza ) bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili, Simba ilitafuta bao la kusawazisha bila mafanikio, huku mara kadhaa mshambuliaji wake Damian Morisho Kimti akikosa nafasi za kufunga, majonzi yalikuja dakika ya 77 pale mshambuliaji hatari wa Stella Abdijan Jean Zozo ‘Boli Zozo’ alipopokea pasi safi toka kwa N'guessan Serge na kumpindua beki wa kushoto wa Simba, Rashid Abdallah aliyecheza mchezo huo wa pili wa marudiani kisha kupachika bao safi la pili bao ambalo lilishangiliwa mno na mashabiki wa Yanga huku wakiimba; 'Uzalendo umetushinda...Uzalendo umetushinda...!" 
Benchi la Simba lilijaa simanzi baadhi ya wachezaji walitokwa na machozi.


STELLA ILIWASAPRAIZI
Stella Abidjan ilibadilika tofauti na ile ilivyocheza mechi ya kwanza wiki mbili nyuma jijini Abidjan.
Wachezaji Amani Celestine, Solo Jean, Austine Koune, N'guessan Serge waling'ara na kuwafunika vibaya wachezaji wa Simba ambao walikata tamaa.
Hadi dakika 90 zinakamilika Simba ilishindwa kutwaa ubingwa na kuambulia nafasi ya pili iliyowawezesha kupata medali za fedha na kumpa wakati mgumu Rais wa Awamu ya Pili wakati akiwa madarakani na kuwa mgeni rasmi kulikabidhi Kombe la wageni. 


KIA ZAOTA MBAWA
Mabao hayo yalifuta ndoto ya Simba ya kutwaa kwa mara ya kwanza kombe hilo na pia mabao hayo yaliwakosesha wachezaji wa Simba kupata magari aina ya KIA, ambayo waliahidiwa na mfadhili wao mkuu, Azim Dewji.
Simba ambayo ilikuwa na kikosi ambacho kilikuwa kikiundwa na wachezaji nyota, kilitoka sare ya bila kufungana katika mchezo wa awali uliofanyika Jumamosi Novemba 14, 1993.


KIKOSI KAMILI
Katika msimu huo, Simba ilikuwa chini ya Kocha Abdallah 'King' Kibadeni akisaidiwa na Etenne Eshente kutoka Somalia, huku Abdulrahman Muchacho akiwa Meneja wa timu, akisaidiwa na beki wa zamani wa timu hiyo, Mavumbi Omar na Rashid Msemakweli ndiye aliyekuwa Daktari wa timu.
Kikosi kamili cha wachezaji kiliundwa na makipa Mohammed Mwameja, Mackezie Ramadhani na Offen Martin Chussa, mabeki wakiwa ni Deo Mkuki, Twaha Hamidu 'Noriega', Seleman Pembe, Fikiri Magosso, George Masatu 'GM', Godwin Aswile 'Scania', Kassongo Athuman na Rashid Abdallah.
Wachezaji wengine ni; Abuu Omar, Idd Seleman 'Kibode' a.k.a Nyigu, Joachim Masumbuko, Ramadhan Lenny, George Lucas 'Gazza', Hussein Masha 'Smart Boy', Razak Yusuf 'Careca', David Mihambo, Mbuyi Yondani, Feruz Teru, Michael Paul 'Nylon', Thomas Kipese 'Uncle Tom', Nico Kiondo, Damian Morisho 'Kimti', Abdul Ramadhan 'Mashine', Bakar Idd 'Beka Joe', Dua Said na Malota Soma 'Ball Juggler'.