Mjadala wa Simba, Yanga unafia hapa
MECHI ya Simba na Yanga ndiyo kubwa ambayo inasubiriwa kwa siku chache zijazo kabla timu hizo hazijacheza michuano ya kimataifa siku chache mbele.
Mechi hii ni ya pili kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya awali timu hizo kuvaana kwenye Uwanja wa Mkapa na mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 Yanga akiwa mwenyeji.
Jumapili itakuwa siku ya kumaliza ubishi kwa timu hizo ambazo zote mbili kila moja inapambana kuona kuwa inamaliza ubabe wa msimu huu kwa mwenzake.
Kama zitafanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho ASFC basi zinaweza kukutana kwa mara ya nne msimu huu.
Kumekuwa na mambo mengi yanazungumzwa kuhusu mchezo huu, wengi wakisema kuwa ni mchezo ambao utaamua ubingwa, lakini wengine wakiona kuwa hauna umuhimu wowote hata kama Simba ambao wapo nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi nane watapata ushindi.
Hata hivyo, mashabiki wengi wamekuwa wakiizungumzia dabi hii tofauti na misimu kadhaa iliyopita, wengi wanaamini kuwa msimu huu mechi hiyo ya watani haina mwamko ambao ilikuwa nao kwa miaka miwili iliyopita na imekuwa haizungumzwi sana.
Deus Kaseke ambaye amewahi kucheza michezo kadhaa ya dabi na sasa anaitumikia Singida Big Stars amekuwa wa kwanza kuzungumza hilo na kusema hali ambayo ilikuwa inaonekana siku chache za mechi ya Simba na Yanga na sasa ni vitu viwili tofauti.
Hata hivyo, kuna baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kupoteza umaarufu wa mechi hiyo kubwa na maarufu barani Afrika lakini mojawapo ikichangiwa na timu hizo zenyewe.
Kwa msimu huu hadi sasa ni dhahiri kuwa Yanga wana nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa kwa sasa wakiwa pointi nane tofauti na Simba, zikiwa zimebaki mechi tano ligi hiyo imalizika.
Hii ina maana kuwa Yanga hata kama wakipoteza mchezo wao dhidi ya Simba bado watakuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa huo, hali ambayo inawafanya mashabiki kupunguza morali kwenye mechi hiyo.
Kwa wale wa Simba wanaona kuwa ni mechi ya kawaida, faida kubwa ambayo imebaki ni ya kishabiki zaidi ya kuwatania watani wao endapo watapata ushindi lakini siyo mabadiliko ya msimamo.
Lakini jambo lingine ni hamasa ya mchezo kutokana na fedha, kumekuwa na mfumo wa tofauti kwa miaka ya hivi karibuni, mechi za Ligi Kuu Bara kwa sasa timu mwenyeji imekuwa ikichukua mapato yote ya mlangoni, hii imesababisha kupunguza pia mwamko wa mchezo huu kwa kuwa wasemaji na viongozi ambao wamekuwa wakizungumzia mchezo huo ni wa upande mmoja.
Mfano katika mchezo wa kwanza wa Yanga na Simba, Yanga ndiyo walikuwa wanafanya mikutano ya waandishi wa habari na kuzunguka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kupata mashabiki kwenye mechi hiyo kwa kuwa mapato yote ambayo yalipatikana yalikuwa ya kwao.
Hii iliwafanya Simba kukaa kimya kwa kwa walihofia kuwapigia debe Yanga wapate fedha nyingi, ingawa mwishoni sana waliibuka na kuzungumza ingawa siyo kwa ukubwa.
Jambo lingine ni mashabiki kuzitazama Simba na Yanga mara nyingi zaidi kwa siku za karibuni, pamoja na kwamba bado mechi hiyo inaweza kuwa na mashabiki wengi, gumzo lake mtaani siyo kubwa kwa kuwa michezo miwili mfululizo mashabiki wa soka wamefanikiwa kuziona sana timu hizo za Dar es Salaam.
Kwa mara kwanza, msimu huu inawezekana ndiyo kikawa kipindi pekee ambacho mashabiki wameziona timu hizo mara nyingi zaidi kwa kuwa zote zimeshiriki michuano ya kimataifa kwa Simba kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kucheza hatua hiyo ya Kombe la Shirikisho ni dhahiri kuwa kwa kipindi kifupi mashabiki wameziona timu hizo kwa zaidi ya mara tano kwenye Uwanja wa Mkapa tu wakicheza michezo mikubwa.
Hii inawafanya mashabiki kuzoea kuzitazama timu hizo hali inayopunguza mwamko kwenye mchezo huo.
Lakini jambo lingine ni kushinda kwa Yanga mara kwa mara kwenye ligi, huku kumekuwa kukiwafanya mashabiki wa Simba kuona kama wanakwenda uwanjani kukutana na jambo lile lile, lakini pia Yanga nao wanaamini kuwa mchezo utakuwa na matokeo yaleyale hali ambayo inapunguza mjadala mkubwa mtaani.
Mara ya mwisho Simba kuibuka na ushindi kwenye mchezo dhidi ya Yanga kwenye Ligi Kuu Bara ni mwaka 2019.
Hizi zinaweza kuwa baadhi ya sababu, lakini ukweli ni kwamba kumalizika ushabiki wa Simba na Yanga ni jambo gumu ambalo litachukua miaka mingi ijayo kutokana na mizizi ambayo imewekwa na timu hizi.
Hata hivyo, kocha wa KVZ na beki wa zamani wa Simba, Amri Said alitaja sababu mojawapo inayopunguza msisimko wa dabi kwamba ni matokeo ya droo, akiwataka wachezaji kujituma ili kuwafanya mashabiki wapende kwenda uwanjani kuangalia ushindani.
“Zamani kulikuwa hakuna promosheni za media kama sasa, lakini msisimko ulikuwa unaanzia mitaani hadi uwanjani, mipira ilikuwa linanunua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilikuwa inalindwa na mashabiki hadi wakati wa kuingia uwanjani na ushindani mkali na timu moja wapo lazima ishinde,” .
Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni alisema enzi zao dabi ilikuwa na mvuto na wachezaji walikuwa wanaacha rekodi za kusisimua tofauti na sasa.
“Wachezaji wa sasa wanapaswa kuongeza ushindani, raha ya utani mmoja afungwe mwingine azomewe, lakini imekuwa tofauti sare zimekuwa nyingi, dabi ina heshima kubwa ingawa ligi ni ile ile, inawagawanya Watanzania kwenye makundi mawili,” alisema.
Straika wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema anaona msisimko umehamia mitandaoni, tofauti na zamani ambapo stori nyingi zilikuwa zinapigwa kijiweni.
“Sayansi na teknolojia imekuwa kwa sasa mashabiki wanabishana mitandaoni na sio vijiweni tena, hii ni dabi hata zikikutana mara 100 lazima msisimko upo palepale, Simba na Yanga zimeshika nchi,” alisema.