Prime
Miundombinu hii kuna mahali tunajisahau
WAKATI fulani walikuja maofisa wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kukagua maendeleo ya soka kiufundi ya nchi na kujua hali ya viwanja vinavyotumiwa na klabu mbalimbali kwa ajili ya mashindano ya ndani na nje, pia kujua sehemu ambazo timu hizo zinajiandalia.
Baada ya kuona na kujifunza mengi kuhusu hali ya soka Tanzania, walikuwa na mapendekezo yao, ikiwamo kushauri viwanja vya mazoezi vyenye vipara, yaani majani kwenye baadhi ya sehemu tu, kama inashindikana kuwa na majani sehemu zote, ni bora yaondolewe ili kuufanya uwanja usiwe na migongo inayosababisha mpira upoteze uelekeo.
Ushauri mwingine ni kuhusu viwanja vinavyotumika kwa mashindano mbalimbali ambavyo havimilikiwi na klabu au Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ni muhimu sana kwa mamlaka kujenga mahusiano mazuri na wamiliki, ikiwa ni pamoja na kuchangia gharama za matengenezo pale shirikisho linapoona liko kwenye uwezo mzuri kifedha.
Huu ni ushauri ambao unafaa kuendelezwa wakati wote, ukizingatia ni klabu chache za Ligi Kuu, Championship na za Daraja la Kwanza zinazomiliki viwanja vyao.
Ukizungumzia umiliki ni kama Azam FC inavyomiliki uwanja wa Chamazi Complex au Mtibwa Sugar na Manungu, JKT na Isamhuyo na KMC na uwanja wake ulioko Mwenge, jijini Dar es salaam.
Ukiachana na Azam Complex, viwanja vingine vyote vimeshawahi kukutana na rungu la Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi, maarufu kama Kamati hya Saa 72 linalotolewa kwa taarifa ile inayofanana kila siku yenye sentensi ya “haukidhi viwango” bila ya kujata ni kiwango gani ambacho hakikufikiwa.
Ni kama vile kamati inaona wamiliki wa viwanja hivyo wanazitaka sana mechi za Ligi Kuu na Championship. Kwa hiyo wanapokaa wanaona wakitoa taarifa ya “haukidhi viwango”, mara moja wamiliki watakimbiakimbia kuhakikisha wanafikia viwango na mechi kurejeshwa.
Taarifa ya “haukidhi viwango” iliyotolewa wiki iliyopita na kamati hiyo kuhusu Uwanja wa KMC ni mwendelezo wa mazoea hayo ya kuwasumbua wamiliki ili wahangaike kufanya marekebisho wanayodhani yanafaa.
Taarifa hiyo inaeleza suala la miundombinu ya uwanja huo ndiyo haikidhi viwango. Ingawa haijataja hasa ni kitu gani hakikidhi viwango, unapotaja miundombinu unazungumzia suala kubwa sana linalohitaji matengenezo makubwa kurekebisha ili lilingane na mahitaji ya mchezo wa mpira wa miguu.
Tangu ufunguliwe, uwanja huo umeshatumika kwa mechi nyingi na timu kadhaa zinafanya mazoezi hapo. Inakuwaje ghafla kunatoka taarifa eti “miundombinu haikidhi viwango?”
Kuanzia lini miundombinu haikidhi viwango? Ni kitu gani kimesababisha Kamati ya Saa 72 iibuke na taarifa ambayo ilitakiwa itolewe kabla ya uwanja kuanza kutumika kwa mechi rasmi za mashindano?
Yote hayo yamefichwa kwenye taarifa ya “miundombinu haikidhi viwango” na hivyo huwezi kuhoji sana mtu wa pembeni kwa kuwa ‘kwanza haukuhusu’.
Ajabu ni Uwanja wa KMC uko Dar es salaam, wamiliki ambao ni Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, wako Dar es salaam, wakaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) wapo Dar es salaam na Manispaa ya Kinondoni ilishatoa taarifa inajenga uwanja.
Sasa ilikuwaje mamlaka za soka hazikujihusisha na maandalizi ya ujenzi huo, japo kwa kushauri ni mambo gani ya kuzingatiwa katika miundombinu ili ukidhi viwango vya mpira wa miguu.
Hata kama Bodi ya Ligi haitoi hata senti tano kuchangia ujenzi, ushauri ungetosha kuwapa wamiliki taarifa muhimu za kuzingatia wakati wa kujenga uwanja huo.
Viwanja hutumika kwa shughuli tofauti kama vile michezo mingine ya baseball, kriketi, mpira wa miguu wa aina ya Kimarekani (American football) na mwelekeo sasa ni viwanja hivyo kutumika kwa shughuli za starehe kama matamasha ya muziki, harusi na mabonanza mengine.
Shughuli za starehe zinafanywa na watu tofauti na zinachotaka ni eneo la wazi tu, mambo mengine kama kupanga jukwaa na kupamba yanafanywa na wenye shughuli. Lakini mpira wa miguu kama ilivyo michezo mingine mikubwa ina viwango ilivyoweka ili mchezo huo uchezwe bila ya matatizo.
Eneo lenyewe la kuchezea ni kulingana na vipimo vya kimataifa, bado vyumba vya kubadilishia nguo, vyumba vya waamuzi, vyumba vya mikutano na waandishi wa habari, vyumba vya huduma ya kwanza na vyumba kwa ajili ya kupima matumizi ya daa za kusisimua misuli.
Bado kunatakiwa kuwe na eneo bora kwa ajili ya watangazaji wa redio na televisheni na mazingira mazuri kwa ajili ya wapigapicha za mnato na televisheni.
Kwa viwanja ambavyo ni vya viwango vya Olimpiki, matatizo si makubwa sana kwa wanahabari na wengine, lakini mwenendo uliopo sasa hapa nchini na ulishakuwepo kwa wenzetu walioendelea, ni kujenga viwanja kwa ajili ya mpira wa miguu tu. Viwanja hivi havina sahemu ya kukimbilia riadha wala vyumba vingi. Ni viwanja ambavyo ni rahisi kwa kuwa havihitaji vitu vingi.
Ndiyo maana kumekuwa na mwamko wa taasisi kujenga viwanja vyake kama ilivyofanya Manispaa ya Kinondoni, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Azam na Singida Black Stars.
Hawa hawatakiwi wapewe taarifa za kufungia viwanja “kutokana na miundombinu kutokidhi viwango”, bali kushirikiana nao kutafuta suluhisho la kasoro hizo. Na tatizo linapotokea ni lazima kujadiliana na wamiliki hao kwa kina kujua tatizo hilo linatatuliwa vipi, badala ya kujifungia na kutoa tamko la “viwango”.
Kama nilivyoeleza awali, hivi sasa viwanja vinatumika kwa shughuli nyingi. Kama wamiliki wakiona waendeshaji wa shughuli nyingine nje ya mpira wa miguu wanaongezeka, hawataona tabu kuachana na mchezo huo na kujikita na shughuli ambazo hazisababishi waumbuliwe kila siku kwenye vyombo vya habari.
Kama viwanja kama Santiago Bernabeu na Camp Nou sasa vinatumika kwa harusi na matamasha ya muziki na miundombinu umejengwa kwa namna ambayo ni rafiki kwa shuhghuli hizo, nini kitazuia uwanja wa KMC au Isamhuyo kutumika kwa shughuli hizo, hasa nyakati hizi ambazo jiji la Dar es salaam limekuwa zaidi na mji kuwa mpana kiasi kwamba sherehe kama za harusi zinaweza kuanza kufanyika mchana?
Alex Mnyeti alishaonyesha hilo aliposema yuko tayari uwanja wake utumike kulishia mifugo kuliko kuendelea kuona timu yake ya Gwambina inanyanyaswa. Gwambina haipo tena na uwanja haupo tena.
Ni muhimu sana kwa Kamati ya Saa 72 kuishauri Bodi ya Ligi kufikiria mara mbilimbili matamko hayo yanayoonekana kutolewa kimazoea, huku yakiwa na picha hasi inayochafua wamiliki na wafanyakazi wa taasisi hizo.
Isitoshe matamko hayo yanaweza kutumiwa vibaya na wahusika, yaani kuiyumbisha timu ambayo kimekuwa na mwendelezo mzuri kwenye uwanja fulani kwa imani kuhama uwanja kutaiyumbisha. Au kuiondoa timu kwenye uwanja mzuri inapocheza na mpinzani ambaye anakuwa mzuri zaidi kwenye uwanja mzuri.
Naona Kamati ya Saa 72 inazidi kujisahahu na kujitwalia mamlaka mengi, kiasi kwamba sasa imekuwa ni mazoea na si haja ya kulitafutia suluhisho tatizo la viwanja au mengine yanayosumbua uendeshaji ligi.