Prime
Mikel Arteta anatazamana na lango tupu, ashindwe yeye tu
MIKEL Arteta anaanza ligi leo. Ni kama vile anatazamana na lango. Ni kama vile mchezaji aliyesimama hatua kumi na mbili mbele ya kipa akijaribu kufunga penalti. Ligi inapaswa kuwa yake hii.
Alianza kuondoka Jurgen Klopp. Na mwishoni mwa msimu uliopita uwanja wa Ettihad pale Manchester ulimuaga kocha mwenye akili nyingi. Pep Guardiola. Huyu huyu Pep ndiye aliyemfundisha Arteta ukocha.
Huyu huyu Pep ndiye aliyetuingiza katika dunia ya mpira mpya. Mpira ambao Arteta alijifunza na kuupeleka Arsenal. Msimu uliopita ni mpira huu huu ambao uliwapa Arsenal taji lao la kwanza baada ya miaka 22.
Msimu huu Arteta ashindwe mwenyewe tu. Kwanza kabisa Pep ameondoka. Hakuna kitu kigumu kama kushindana na Pep katika ligi kuu ya England. Kamuulize Jurgen Klopp. Hata Arteta mwenyewe anafahamu hili. Katika msimu ambao City walikuwa chini bado nusura waipoke Arsenal ubingwa msimu uliopita.
Na sasa Pep ameondoka. Lakini wiki iliyopita mtu anayeitwa Rodri naye ameondoka. Huyu ndiye roho ya aina ya mchezo wa Pep. Huyu ndiye mtawala wa dimba. Huyu ndiye kila kitu. Kule Barcelona Pep alikuwa Sergio Busquet. Pale City Pep alikuwa na Rodri. Sioni namna ambavyo City inaweza kupata mbadala wa hawa wawili. Sioni.
Twende Liverpool. Wana kocha mpya Andoni Iraola. Walimtoa kule Bournemouth. Huyu kocha na wachezaji wake ndio waliipa Arsenal ubingwa wakiwa sebuleni. Msimu uliopita walikuwa katika ubora wao.
Huyu Iraola ni Mhispaniola. Ndio, tunaishi katika dunia ambayo makocha bora kwa sasa wanatoka Hispania. Sijui anaweza kuifanyia nini Liverpool. Ni msimu wake wa kwanza na timu kubwa. Itabidi ajipambanue kama yeye ni kocha wat imu ndogo au kocha wa timu kubwa. Ataweza kupambana na Arteta? Hatujui.
Iliwahi kuwatokea makocha kadhaa huko nyuma. Akina David Moyes. Alifanya vizuri na Everton lakini alipopewa Manchester United maisha yakawa magumu kwake. Bado Arteta yupo hatua nyingine mbele yake. amepambani ubingwa mara kadhaa na ametwaa ubingwa msimu ulioisha.
Tunakuja kwa Michael Carrick na Manchester United yake. kumbukumbu za nyuma zinatisha. Alikuwa kocha wa muda akafanya vizuri lakini sasa amepewa timu moja kwa moja. Simkumbuki kocha wa muda aliyepewa timu jumla halafu akatisha.
Huwa wanakuja kwa moto wa kifuu. Mfano ni hapo hapo Old Traffprd. Ole Gunnar Solskjaer aliwahi kupewa timu kwa muda akafanya vizuri. Alipopewa jumla timu ikampalia. Pale Stamford Bridge wamewahi kupata kesi hiyo kwa mchezaji wao wa zamani Roberto Di Mateo.
Di Mateo aliwahi kupewa timu kwa muda akaipa hadi ubingwa wa Ulaya. Alipopewa timu jumla msimu uliofuatia akafukuzwa Novemba. Tuone kama kweli Carrick anaweza kufanya maajabu akiwa kocha wa kudumu. Tukumbuke kwamba kabla hajapewa Manchester United kwa muda alishawahi kufukuzwa kule Middlesbrough.
Nani mwingine? Xabi Alonso. Huyu amepewa kitu kinachoitwa ‘project’ katika timu ambayo haieleweki. Chelsea. Anaweza kumzuia Arteta kutwaa ubingwa katika msimu wa kwanza? Hiyo bahati aliipata Arnie Slot.
Alonso alifanya vizuri akiwa na Bayer Leverkusen kiasi cha kutwaa ubingwa mbele ya Bayern Munich. Ubingwa wa kwanza wa Bundesliga katika historia ya Leverkusen. Baadaye alienda timu kubwa zaidi duniani, Real Madrid. Wote tunajua kilichotokea. Alifukuzwa.
Na sasa amepewa timu kubwa nyingine pale England. Chelsea. Ndiyo, Chelsea ni wakubwa kuliko Leverkusen. Ataweza? Ataweza kuipa Chelsea ubingwa katika msimu wake wa kwanza pale London? Sidhani.
Kwanza kabisa Alonso ana kazi kubwa ya kufanya katika mradi huu mpya wa Chelsea. Ana kazi kama ambavyo Arteta ameifanya kwa misimu sita hivi. Kikosi kipo ovyo. Inabidi aifumue timu kwa misimu kadhaa.
Lakini pia amepewa nafasi nyingine ya kuthibitisha kwamba anaweza kuwa kocha wa timu kubwa. Akishindwa tena kazi hii kama alivyoshindwa kule Madrid nadhani timu nyingi kubwa zitaamini kwamba yeye anapaswa kuwa kocha wa Leverkusen au Roma.
Arteta ashindwe yeye tu msimu huu. Bahati nzuri alimfumua City katika pambano la ngao ya jamii na kutoa kiashiria namna gani ligi inaweza kuwa msimu ujao. Uzuri mwingine kwa Arteta ni kwamba ana matajiri wanaoujua kutumia pesa.
Katika nyakati kama hizi Arsene Wenger alikuwa anajaribu kujionyesha kwamba yeye ni ‘genius’. Alikuwa analeta ubahili wa hali ya juu huku akienda Ufaransa kumchukua mchezaji wa Daraja la pili, Yaya Sanogo.
Hata hivyo Arteta anaonekana kurithi tabia za Sir Alex Ferguson. Ndani ya ubingwa wake Sir Alex alikuwa anatia pesa ya kuchukua wachezaji mahiri ambao wameshaijua ligi kuu ya England. Ndicho ambacho Arteta amefanya. Tayari ana kikosi imara lakini amemuongeza Bruno Guimares. Nahodha wa Newcastle United.
Katikati ya ubingwa wake amemuongeza Mgiriki, Christos Tzolis. Msimu uliopita pale Ubelgiji Tzolis alifunga mabao 17 na kupika mabao 23. Hii ndio ilikuwa tabia ya Sir Alex ndio maana alikuwa anatetea taji la England mara nyingi. Wenger alikuwa hafanyi hivi na ndio maana hakuwahi kutetea taji la ligi kuu ya England.
Viashiria ni vingi kwamba Arteta ameachiwa ligi na Pep. Asipotwaa kwa mara nyingine tena atakuwa mjinga. Liverpool, Chelsea na Manchester City zote zina makocha wapya.
Vile vile ni ngumu sana kwa Enzo Maresco kuwa Pep mpya. Kumbuka alifukuzwa kule Chelsea baada ya mfululizo wa matokeo mabaya. Anawezaje ghafla akawa mrithi wa Pep? Mechi ya kwanza tu ya kufungua msimu alifundishwa mpira na Arteta.