Prime
Mihemko ilivyowaharibia viongozi Simba kwa Pantev
HESABU vidole vyote viwili vya mikono yako. Hivyo ni vingi kuliko idadi ya mechi ambazo kocha ‘matatuu’ Dimitar Pantev alifundisha Simba. Wanaojua kuhesabu wanadai amekuwa kocha wa Simba kwa siku 61 tu. Namna maisha yanavyokwenda haraka.
Aliletwa kwa mihemko kweli kweli. Simba walicheza na Gaborone United katika mechi za kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika. Gaborone waliwamudu Simba kwa kiasi kikubwa na lolote lingeweza kutokea. Katika mechi zote mbili Gaborone waliupiga mwingi. Simba wakajifunza kitu.
Ilisemwa kwamba katika mechi zote za kufuzu kwa timu za Tanzania basi Simba ndio walikuwa wamekutana na mpinzani mwenye afya. Nasikia kiongozi mmoja alipagawa zaidi na kiwango cha Gaborone United kiasi cha kuamua kumpa mkataba Pantev.
Inadaiwa jambo lenyewe lilileta migogoro ndani ya Simba kwa sababu baadaye walikuja kugundua kwamba Pantev hakuwa na hadhi ya kukaa katika benchi lao. Baada ya Pantev kupewa mkataba ikaonekana nafasi pekee ambayo itamuweka katika benchi la Simba ilikuwa awe meneja. Kocha mwenye sifa ambaye angeendelea kuwa kocha alikuwa Seleimani Matola.
Huo ulikuwa muhemko wa kwanza. Kumchukua kocha kwa sababu alikuwa amecheza vizuri dhidi yenu. Haishangazi sana kwa sababu imewahi kutokea sana nchini hata kwa wachezaji. Perfect Chikwende aliwahi kucheza mechi mbili nzuri za timu yake ya Zimbabwe, Platinum FC, na Simba papo hapo wakampa mkataba. Baadaye akachuja katika jezi zao.
Muhemko mwingine ilikuwa ni kumpa mkataba bila kuchunguza wasifu wake. Wakati mwingine tunahitaji watu wasomi na wanaofikiria kwa haraka. Ni jambo ambalo limeitia fedheha Simba bila kujali nani alifanya hivyo. Sisi huku nje hatujui kwamba anayepaswa kulaumiwa ni mtu mmoja na sio wote.
Muhemko wa mwisho kabisa ni namna alivyoondolewa. Hatujui kama Simba ilikuwa inatafuta upenyo wa kuachana naye baada ya kugundulika kwamba hadhi ya umeneja isingewafaa klabuni hapo. Hata hivyo tunaweza kujadili sababu za uwanjani.
Uwanjani Simba walikuwa wanakwenda vizuri tu na Pantev, na ndio maana kuna mashabiki wamegawanyika kuhusu kuondoka kwake. Sehemu moja tu ambayo Pantev alionekana kuwakera mashabiki wa Simba ni pale alipoanza mechi bila washambuliaji katika pambano gumu la ufunguzi wa makundi dhidi ya Petro Luanda ambalo Simba walilala 0-1 pale Temeke.
Tatizo katika hili ni kwamba Pantev amekuja katika soka letu huku akijaribu kuwa mbele ya muda. Sisi mashabiki wa kawaida pamoja na mabosi wa hizi timu tupo nyuma ya muda linapokuja suala la soka la kisasa ambalo Pep Guardiola ametuletea.
Sio kitu cha ajabu kwa kocha kuanza na viungo watupu. Kwa mujibu wa filosofia ya Pep Guardiola ambaye ndiye ameanzisha mambo haya yeye anaamini kwamba wachezaji wengi uwanjani wanapaswa kuiunganisha timu na sio lazima kuwa na mshambuliaji mmoja anayesimama katika boksi pale mbele.
Akiwa na Barcelona kuna wakati alikuwa anamuweka benchi mshambuliaji asilia tena mwenye jicho la goli, David Villa na akawa anamuanzisha Cesc Fabregas kucheza kama mshambuliaji wa uongo pale mbele (false number 9).
Lengo ni kuhakikisha Fabregas anarudi katikati kuunganisha timu na kutengeneza nafasi ambazo yeye mwenyewe au mtu mwingine anaweza kutumia. Tatizo Pantev alikuwa mbele ya muda katika jambo hili. Sisi hatujafika huko.
Lakini hata katika pambano lenyewe Simba walitengeneza nafasi ambazo Pantev alikuwa anazitaka. Elly Mpanzu na Morice Abrahamwakapoteza nafasi za wazi. Mpaka leo najiuliza kama hawa wawili wangetumia nafasi zao wakati wanatazamana na nyavu leo Pantev angefukuzwa? Simba wangekuwa wameshinda 2-1 Pantev angefukuzwa?
Bao lenyewe ambalo Simba walifungwa lilitokana na mpira kumgusa mlinzi mmoja wa kwao na kumpoteza maboya kipa Yakubu Suleiman. Kama yote hayo yasingetokea Simba wangeondoka na pointi tatu na nadhani Pantev angeondoka shujaa kwa kufanikiwa kuondoka na pointi tatu muhimu huku akiwa ameanza mechi bila mshambuliaji.
Kuonyesha kwamba mashabiki walikuwa wamechanganyikiwa na kipigo kumbuka kwamba baada ya kumalizika kwa mechi walikuwepo hadi mashabiki ambao waliamini kwamba uwanja huu kwa sasa una nuksi kwao.
Wakahoji kwanini Yanga walikuwa wamekimbia uwanja huo na kwenda Zanzibar.
Wakatokea wengine waliodai kwamba Yanga walikuwa ‘wameweka’ vitu vyao katika uwanja na wakakimbia huku wakiwaachia Simba msala. Wanaosema haya walikuwa wamesahau kumlaumu Pantev kwa kuanza mechi bila mshambuliaji kwa sababu waliona nafasi ambazo zilipotezwa.
Ikaja mechi dhidi ya Stade Malien ambapo Jean Charles Ahoua alipoteza nafasi ya wazi akiwa anatazamana na nyavu.
Baadaye Simba waliruhusu mabao mawili na wao wakapata moja. Najaribu tu kuwaza kwamba huenda pambano hili lingeisha kwa sare ya 2-2.
Ina maana kama Simba wangekuwa na pointi nne leo hii kama ilivyo kwa watani zao Yanga, sidhani kama Pantev angefukuzwa. Na kama kuna kisa kilikuwa kinatafutwa basi angetafutiwa sababu mbele ya safari na sio kwa mechi hizi mbili.
Kuonyesha pia kwamba kuwa mbele ya muda kulikuwa kunamponza Pantev inasemekana alikuwa hamtaki kipa Yakubu Suleiman katika lango lake kwa sababu alikuwa hawezi kucheza sana mpira kwa miguu.
Hili limeanza kuwa jambo la kawaida kabisa kwa makocha wa kisasa huko duniani lakini kwetu sisi msingi wa kipa ni kujua kuokoa michomo kwanza.
Simba ya Pantev ilikuwa inatoa matumaini. Ikumbukwe kwamba Pantev hakwenda na timu katika maandalizi ya msimu mpya na badala yake Fadlu Davis ndiye aliyekwenda na timu Misri.
Nahisi Pantev angeweza kuigeuza Simba icheze kama Gaborone United ilivyokuwa inacheza.
Sijui bado kama kuna sababu nyingine za nyuma ya pazia ambazo zimemuondoa Pantev Simba lakini kama ni kwa sababu za kisoka basi nadhani kulikuwa na mhemko katika kumfukuza kama ambavyo kulikuwa na mhemko katika kumchukua kiasi kwamba hawakujua kama atakuwa meneja au kocha.