Prime
Kutoka Zinedine Zidane hadi Julian Alvarez, dunia imepoa
MATAJIRI wamelala. Viwanja vya ndege vimelala. Mawakala wamelala wanakoroma. Nyakati zimekwenda wapi? Hivi ni nyakati kama hizi Zinedine Zidane alikuwa anahama kutoka Juventus kwenda Real Madrid?
Si ni nyakati kama hizi Inter Milan walikuwa wanamchukua Ronaldo wa ukweli. Ronaldo Di Lima kutoka Barcelona kwenda Inter Milan? Si ni nyakati kama hizi Cristiano Ronaldo katika ubora wake alikuwa anahama kutoka Manchester United kwenda Real Madrid.
Ni nyakati kama hizi ulitokea uhamisho wa kushangaza duniani. Luis Figo alihama kutoka Barcelona kwenda Real Madrid. Dunia ilishangaa. Ulimwengu ulipigwa na butwaa. Nyakati zimekwenda wapi?
Nyakati kama hizi walikuwa wanatamba mawakala maarufu duniani kina Mino Raiola. Kina Jorge Mendes. Kina Pini Zahavi. Kina Kia Joorbachian. Walikuwa wanachanganya akili za makocha mbalimbali duniani.
Wangeweza kukamilisha dili ambayo usingeweza kuifikiria. Dunia ilikuwa lazima ichangamke. Kitu kibaya zaidi huwa ni vita, lakini kwingineko dunia lazima ichangamke.
Kuna wakati dunia inachangamka, kuna wakati dunia inazubaa. Kule kwa Wazungu kuna mpira halafu kuna usajili. Huwa vinachangamsha dunia, lakini upande wa usajili dunia imepoa.
Zamani dirisha la uhamisho kama hili dunia ingesimama na kupigwa na butwaa. Hata hivyo, kwa sasa dirisha limepoa. Hadi mpira umeanza tena na dirisha linakaribia kufungwa hakuna maajabu yanayoendelea katika uhamisho wa mastaa.
Kuna sababu nyingi. Kwanza kabisa. Mastaa wenyewe wa kuhamishwa kwa mbwembwe wako wapi? Katika dunia ya leo labda ghafla ahame Vinicius Junior, Erling Haaland, Lamine Yamal na Kylian Mbappe tunaweza kushtuka.
Tena wahame wakiwa katika mikataba mirefu. Kwa mfano, uhamisho wa Mbappe kutoka PSG kwenda Real Madrid haukusisimua kwa sababu hakuna pesa ndefu iliyotumika.
Alikuwa mchezaji huru. Na wote tulijua kwamba Mbappe alikuwa anakwenda Real Madrid baada ya kugoma kusaini mkataba mpya PSG huku mkataba wake klabuni hapo ukiwa umefika ukingoni.
Hatuna mastaa wengi wakubwa siku hizi. Sijui kwanini. Labda kwa sababu mpira umekuwa mchezo wa kitimu zaidi tofauti na zamani. Siku hizi timu zinatamba kuliko wachezaji. Zamani wachezaji walikuwa wanatamba kuliko timu.
Mfano ni Arsenal yangu. Ni timu bora sana Ulaya. Hakuna mchezaji mwenye hadhi ya Ronaldo, Lionel Messi, Figo, Rivaldo, Thierry Henry na wengineo wakiwa katika ubora wao. Hakuna mchezaji ambaye ukimuuza atavunja rekodi ya uhamisho wa dunia.
Hata hivyo, timu ni bora sana. Ni kama ilivyo PSG. Wamechukua ubingwa wa Ulaya mara mbili mfululizo, lakini hakuna mchezaji wao ambaye utamuuza na atavunja rekodi ya mwanasoka ghali duniani. Ndivyo ilivyo kwa sasa.
Kama Haaland na Mbappe hawawezi kuuzwa kwa sasa, basi hakuna kitu cha kusisimua unachoweza kusimulia. Vinicius hata angeuzwa kwenda Arsenal asingevunja rekodi ya uhamisho ya dunia kwa sababu mkataba wake na Madrid ulikuwa unakaribia kukata roho.
Sio lazima wachezaji wa sasa wavunje rekodi ya uhamisho, lakini ukweli ni kwamba dunia imepoa. Wachezaji wamepoa. Soko limepoa. Hii inasababisha hata mawakala nao wawe wamepoa. Hakuna maajabu sana.
Rodri anaelekea kuwa mwanasoka bora wa dunia mwishoni mwa mwaka huu. Ametwaa Kombe la Dunia 2026 na Hispania. Akiwa na umri wa miaka wa miaka 32 amehamia zake Barcelona kimyakimya. Hakukuwa na mbwembwe nyingi.
Na hapa ndipo tunapoanzia. Katika zama za leo eti unaweza kuwa na mwanasoka bora wa dunia ambaye anacheza katika eneo la chini la kiungo. Yote haya ni kwa sababu Messi na Ronaldo wamemaliza zama zao na mpira pia umebadilika.
Mpira umehama kutoka kwa mawakala umekwenda kwa mabingwa wa tetesi kina Fabrizio Romano. Huwa anasema ‘Here we go’. Mashabiki huwa wanasisimkwa na habari kuhusu klabu zao, lakini ukweli ni kwamba wachezaji wenyewe wanaoingizwa katika hizi sentensi sio wakubwa sana.
Sidhani kama tutarudi katika msisimko wa usajili. Sioni kama klabu zinaweza kuvunja benki katika kiasi kikubwa. Klabu chache zinazotamba kwa sasa zinatumia zaidi silaha ya muunganiko wa kitimu kuliko kutumia majina ya wachezaji wakubwa.
Kwa mfano, PSG haina haja yoyote ya kulazimisha kumchukua Yamal. Wao wana timu bora ambayo haina Yamal. Hawahitaji kipaji cha mchezaji mmoja mmoja kuisaidia timu yao. Na timu yao imekuwa kali zaidi baada ya kuachana na Messi, Neymar na Mbappe. Wanawezaje kutumia kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya Yamal?
Arsenal wamekuwa na timu bora yenye muunganiko ambayo haiwezi kulazimisha kuvunja benki kwa ajili ya Yamal. Mpira umeondoka kuwa mchezo wa vipaji vya mchezaji mmoja mmoja na umekwenda katika timu.
Na sasa tumefika mahala kwamba mchezaji ambaye watu wanamsikilizia kwamba anaweza kuondoka katika dirisha hili la uhamisho ni Julian Alvarez. Ana mabao manane na pasi nne za mabao. Hata hivyo, anatingisha katika dirisha la usajili kama vile amefunga mabao 31 na ametoa pasi 13 za mabao.
Hapa ndipo soko la uhamisho lilipotuleta. Kuanzia wakati ule ambao tulikuwa hatuamini macho yetu kwamba Zidane anaweza kuhama Juventus kwenda Madrid kwa dau la uhamisho la dunia, leo tunasubiri kuona kama Alvarez anaweza kuhama kutoka Atletico Madrid kwenda Barcelona au Arsenal. Nyakati zimekwenda wapi?
Halafu hawa wababe wa Hispania nao wameishiwa pesa. Barcelona na Madrid. Walikuwa wababe sokoni, lakini sasa hivi wamechoka. Wanasubiri wachezaji wa bure wanaomaliza mikataba. Ukikumbuka kwamba Kevin De Bruyne alimalizia mpira wake Manchester City akiwa katika ubora wa juu na hakwenda Real Madrid wala Barcelona unaishiwa pawa.