Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi za moto Kariakoo Derby za Ngao ya Jamii

Muktasari:

  • Mechi hiyo itayopigwa saa 2:30 usiku, inazikutanisha timu hizo zikiwa na rekodi bora, ambapo Simba inaongoza kwa kutwaa mataji mengi ya Ngao ya Jamii mara 10, kuanzia rasmi mwaka 2002, 2003, 2005, 2011, 2012, 2017, 2018, 2019, 2020 na 2023.

TAMBO za mashabiki wa soka kwa sasa ni katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii kati ya watani wa jadi Yanga dhidi ya Simba ‘Kariakoo Derby’, itakayopigwa leo Jumatano ya Agosti 12, 2026, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mechi hiyo itayopigwa saa 2:30 usiku, inazikutanisha timu hizo zikiwa na rekodi bora, ambapo Simba inaongoza kwa kutwaa mataji mengi ya Ngao ya Jamii mara 10, kuanzia rasmi mwaka 2002, 2003, 2005, 2011, 2012, 2017, 2018, 2019, 2020 na 2023.

Kwa upande wa watani zao wa jadi Yanga, inafuatia kwa kuchukua ubingwa huo mara tisa tu, ikianza mwaka 2001, 2010, 2013, 2014, 2015, 2021, 2022, 2024 na 2025, huku Azam ikichukua mara moja mwaka 2016, sawa na Mtibwa Sugar iliyolichukua 2009.

Yanga ambayo ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026, inakutana na Simba katika hatua hii baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la CRDB, huku mashabiki wa pande zote mbili wakisubiria kuona kitakachotokea visiwani, Zanzibar.

Kupitia makala haya, Mwanaspoti linakuletea mechi za kusisimua za Ngao ya Jamii, ilizozikutanisha timu hizo tangu mwaka 2001.


YANGA 2-1 SIMBA (2001)

Mechi hii iliyopigwa Jumamosi ya Februari 17, 2001, ilishuhudia Yanga ikitwaa ubingwa huo wa Kombe la Ngao ya Jamii baada ya kuifunga Simba mabao 2-1, yaliyofungwa na Edibily Lunyamila dakika ya 47 na Ally Yussuf ‘Tigana’ dakika ya 80.

Kwa upande wa bao la kufutia machozi kwa upande wa kikosi hicho cha ‘Wekundu wa Msimbazi’ Simba, lilifungwa na aliyekuwa nyota wa timu hiyo, Steven Mapunda ‘Garrincha’ dakika 43, hivyo, kuishuhudia Yanga ikitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.


YANGA 0-0 SIMBA (2010)

Katika mechi hii ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Jumatano ya Agosti 18, 2010, Yanga iliendeleza tena ubabe wake baada ya kushinda kwa penalti 3-1, kufuatia miamba hiyo kushindwa kutambiana muda wa kawaida ulioshuhudia zikitoka suluhu (0-0).

Mabao matatu ya Yanga yalifungwa na Geofrey Bonny, Stefano Mwasyika na Isaac Boakye, huku Ernest Boakye akikosa, wakati kwa upande wa kikosi cha Simba aliyefunga ni Mohamed Banka na waliokosa ni Emmanuel Okwi, Uhuru Suleiman na Juma Nyosso.

SIMBA 2-0 YANGA (2011)

Baada ya unyonge wa muda mrefu, Simba ikafanya kweli kwa kulipa kisasi na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, katika mechi iliyopigwa Jumatano ya Agosti 17, 2011, yaliyofungwa na Haruna Moshi ‘Boban’ dakika ya 15 na Felix Sunzu dakika ya 38.


YANGA 0-0 SIMBA (2017)

Katika mechi hiyo iliyopigwa Jumatano ya Agosti 23, 2017, timu hizo zilikutana ambapo Yanga ilitoka kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2016-2017 kwa tofauti ya mabao, huku kwa upande wa Simba ikitoka kutwaa Kombe la Shirikisho (FA).

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ilishuhudia Simba ikiwa na wachezaji wapya wenye uzoefu wakiwemo, Haruna Niyonzima, Aishi Manula, Erasto Nyoni, Salim Mbonde, James Kotei na Emmanuel Okwi aliyerejea tena kipindi hicho.

Kwa upande wa kikosi cha Yanga, kilisheheni pia wachezaji wenye uwezo yakiwemo maingizo mapya wakati huo wakiwemo, Papy Tshishimbi aliyecheza soka safi, Gadiel Michael na Ibrahim Ajibu pia aliyecheza mechi yake ya kwanza tangu atoke Simba.

Katika mechi hiyo, Simba ilishinda kwa penalti 5-4, baada ya pambano hilo kuisha suluhu (0-0) ndani ya dakika 90, ambapo aliyekuwa nahodha wa timu ya Yanga kwa wakati huo, Kelvin Yondani maarufu ‘Vidic’, alianza kupiga na kukosa mkwaju huo.

Hata hivyo, licha ya Yondani kukosa, beki wa kushoto wa sasa wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyekuwa anaichezea Simba alikosa pia, kabla ya Juma Mahadhi kupaisha mpira kisha, Mohamed Ibrahim ‘Mo’ kuifungia Simba na kutwaa taji hilo.


SIMBA 0-1 YANGA (2021)

Baada ya kukosa taji la Ngao ya Jamii mwaka 2017 kwa penalti, Yanga ikalipa kisasi na kuibuka na ushindi mzuri wa bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho raia wa DR Congo, Fiston Mayele kunako dakika ya 12.

Mechi hiyo ilipigwa Jumamosi ya Septemba 25, 2021, huku Mayele akikumbukwa msimu wa 2022-2023, alipokuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, baada ya kufunga mabao 17, sawa na aliyekuwa nyota wa Geita Gold na Simba, Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’. 

YANGA 2-1 SIMBA (2022)

Pambano hili lililopigwa Agosti 13, 2022, Simba ilianza kupata bao la aliyekuwa nyota wa timu hiyo raia wa Senegal, Pape Ousmane Sakho dakika ya 16, kisha Fiston Mayele akapeleka kilio kwa kuifungia Yanga mabao mawili ya dakika ya 50 na 81.


YANGA 0-0 SIMBA (2023)

Katika fainali hii iliyopigwa Agosti 13, 2023, kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Simba ilishinda kwa penalti 3-1, baada ya mechi hiyo kumalizika kwa suluhu (0-0), huku aliyekuwa kipa wa kikosi hicho, Ally Salim akiibuka ndiye shujaa.

Ally anayecheza Dodoma Jiji aliyojiunga nayo Septemba 7, 2025, akitokea Simba, alidaka penalti tatu zilizoinyima Yanga kutwaa taji hilo, zikiwemo za nyota wakubwa na wazoefu wakiwemo, Khalid Aucho, Pacome Zouzoua na Kouassi Attohoula Yao.

Penalti hizo tatu za Simba, zilifungwa na Mzamiru Yassin, Leandre Willy Essomba Onana na Jean Baleke, wakati aliyekosa ni Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’, huku kwa aliyeifungia Yanga bao hilo moja alikuwa ni nyota wa zamani, Stephane Aziz KI.


YANGA 1-0 SIMBA (2024)

Miamba hii ilikutana tena katika pambano la nusu fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Alhamisi ya Agosti 8, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Yanga ilishinda kwa bao 1-0, la nyota wa kikosi hicho, Maxi Mpia Nzengeli dakika ya 44.

Ushindi huo uliipeleka Yanga fainali na kuichapa Azam FC mabao 4-1, Agosti 11, 2024, yaliyofungwa na Prince Dube dakika ya 19, Yoro Mamadou Diaby akajifunga mwenyewe dakika ya 21, Stephane Aziz KI dakika ya 31 na Clement Mzize dakika ya 90.

Kwa upande wa bao pekee la kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, lilifungwa mapema dakika ya 13 na kiungo mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Feisal Salum ‘Fei Toto’, aliyecheza pia Yanga awali kabla ya kujiunga rasmi na Azam FC.


YANGA 1-0 SIMBA (2025)

Yanga chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mfaransa Romain Folz ilishinda bao 1-0, dhidi ya Simba katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Septemba 16, 2025, lililofungwa na Pacome Zouzoua dakika ya 54.

Kwa upande wa Simba, ilipoteza mechi hiyo ya fainali ikiwa inafundishwa na aliyekuwa Kocha Mkuu, Fadlu Davids raia wa Afrika Kusini, aliyejiunga na kikosi hicho Julai 5, 2024 na kudumu kwa siku 444, baada ya kuondoka Septemba 22, 2025.


YANGA Vs SIMBA (2026)

Timu hizi zinakutana tena ikiwa imepita siku 101 tu, ambazo ni sawa na miezi mitatu na siku 11, tangu mara ya mwisho kwa miamba hii kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara ya msimu wa 2025-2026, iliyoisha kwa sare ya kufungana mabao 2-2, Mei 3, 2026.

Mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, mabao ya Simba yalifungwa na Libasse Gueye dakika ya pili na Clatous Chama dakika ya 10, huku ya Yanga yakifungwa na Prince Dube dakika ya 17 na Bakari Mwamnyeto dakika ya 50.

Katika mechi hiyo, ilishuhudiwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama akifunga bao hilo kwa staili ya (Tiki-Taka) na kuibua mjadala kutokana na ubora wake, huku akitabiriwa kushinda bao bora la msimu wa 2025-2026, la Ligi Kuu Bara.

Pia, timu hizo zinakutana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, huku mara ya mwisho kukutana uwanjani hapo, ilikuwa ni Aprili 29, 2026, katika fainali ya Kombe la Muungano na Simba kutwaa taji hilo kwa ushindi wa bao 1-0.

Mechi hiyo iliyochezwa dakika 120, baada ya suluhu (0-0), za dakika ya 90, bao hilo la Simba lilifungwa kwa penalti na Seleman Mwalimu ‘Gomez’ dakika ya 120+4, kufuatia Clatous Chama kufanyiwa madhambi akiwa eneo la hatari na Edmund John.

Yanga inaingia katika mechi hii na benchi jipya la ufundi, chini ya Kocha Mkuu, Manqoba Mngqithi raia wa Afrika Kusini, aliyetambulishwa rasmi Julai 10, 2026, akichukua nafasi ya Mreno Pedro Goncalves aliyejiunga na AS FAR Rabat ya Morocco.  Mngqithi amejiunga na Yanga baada ya kuachana na Golden Arrows ya kwao Afrika Kusini, huku akiwa na jukumu kubwa mbeleni mwake la kutetea mataji mbalimbali iliyochukua timu hiyo, ikiwemo Ngao ya Jamii na Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027.