Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mechi 10 usizopaswa kuzikosa Kombe la Dunia

Muktasari:

  • Kwa mashabiki enzi za kutazama kila mchezo wa Kombe la Dunia zilishapitwa, lakini kuongezwa kwa timu kutoka 32 hadi 48 kunamaanisha kutakuwa na michezo 72 ya hatua ya makundi.

NEW YORK, MAREKANI: KWA kuwa kutakuwa na michezo mingi katika makundi 12 ya Kombe la Dunia 2026 kabla ya kufika hatua ya mtoano, hizi hapa ni 10 ambazo inafaa uhakikishe kwamba huzikosi walau kutupia jicho lako kwenye runinga mara tu utakaposikia kwamba zinachezwa.

Kwa mashabiki enzi za kutazama kila mchezo wa Kombe la Dunia zilishapitwa, lakini kuongezwa kwa timu kutoka 32 hadi 48 kunamaanisha kutakuwa na michezo 72 ya hatua ya makundi.

Hii ina maana kwamba kabla hata ya kufikia ukubwa wa mashindano uliyozoea kuyaona, kutakuwa na saa 108 za soka katika hatua ya makundi, bila kuhesabu muda wa nyongeza na mapumziko ya kunywa maji yaliyopangwa rasmi.

Pia, kwa sehemu kubwa ya dunia, baadhi ya michezo imepangwa kuchezwa katika nyakati zisizo rafiki kwa watazamaji. Hivyo, itakuwa vigumu kufuatilia kila mchezo unaotamani kuuona. Kwa kuzingatia hilo, tumekuchagulia idadi ndogo na rahisi zaidi ya michezo ya hatua ya makundi ambayo inafaa kuhakikisha umeweka kengele ili usiikose.

Hii si michezo pekee inayostahili kutazamwa, lakini ukiitazama angalau hii utakuwa umejiwekea msingi mzuri wa kufurahia hatua ya makundi. Hizi hapa mechi unazopaswa kuzicheki.


Mexico vs Afrika Kusini

11 Juni, saa 4:00 usiku

Mchezo huu unarudia mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia 2010. Mexico na Afrika Kusini watafungua mashindano katika Uwanja wa Estadio Azteca jijini Mexico City, moja ya viwanja vya kihistoria zaidi duniani.

Uwanja huo uliwahi kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 1970 na 1986, zilizoshindwa na Brazil ya Pele na Argentina ya Diego Maradona mtawalia.

Mechi ya 2010 inakumbukwa zaidi kwa bao la kipekee la Siphiwe Tshabalala lililoitwa “bao la Afrika nzima” ambalo lilifungua mashindano hayo. Kwa kuwa Mexico itakuwa nyumbani, mashabiki wanatarajiwa kuwa na mshikamano wa kipekee katika uwanja wenye uwezo wa kupokea zaidi ya watazamaji 87,000 kwa wakati mmoja.


Brazil vs Morocco

13 Juni, saa 7:00 usiku

Moja ya changamoto za mfumo mpya wa timu 48 ni kwamba timu bora zimegawanyika zaidi katika makundi, hivyo mechi za kiwango cha juu katika hatua ya makundi zimepungua.

Hata hivyo, siku ya tatu tu ya mashindano itatuletea pambano kubwa kati ya mabingwa mara tano Brazil na Morocco, waliowashangaza wengi kwa kufika nusu fainali mwaka 2022. Brazil ina kikosi chenye nguvu kubwa ya ushambuliaji chini ya Carlo Ancelotti, huku Morocco nayo ikija na falsafa mpya ya soka la kushambulia.

Mchezo huo una kila dalili ya kuwa burudani bab'kubwa.


Uholanzi vs Japan

14 Juni, saa 5:00 usiku

Mchezo wa ufunguzi wa Kundi F ni mwingine unaovutia macho. Uholanzi ina kikosi chenye vipaji vingi na inaonekana kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kutwaa ubingwa, ingawa ilionyesha udhaifu kwa kufungwa bao 1-0 na Algeria katika mchezo wa kirafiki.

Kwa upande wa Japan inaweza isiwe miongoni mwa vigogo wa kutwaa taji, lakini imeonyesha mara kadhaa uwezo wa kushangaza dunia. Katika Kombe la Dunia la 2022, iliifunga Ujerumani na Hispania katika hatua ya makundi. Ushindi kwa Japan hapa unaweza kubadili kabisa mwelekeo wa kundi.


Hispania vs Cape Verde

15 Juni, saa 1:00 usiku

Mabingwa wa Ulaya na vinara wa kutajwa kuwania ubingwa wa Kombe la Dunia 2026 wataanza kampeni yao dhidi ya Cape Verde, ambayo inacheza mashindano haya kwa mara ya kwanza. Cape Verde ni moja ya nchi zenye idadi ndogo zaidi ya watu kuwahi kufuzu Kombe la Dunia.

Ingawa imefanya kazi kubwa kufika hapa, mechi hii inaweza kuwa moja ya zile zenye uwezekano mkubwa wa kushuhudia ushindi mkubwa. Hispania ilianza Kombe la Dunia 2022 kwa kuifunga Costa Rica mabao 7-0.


Ufaransa vs Senegal

16 Juni, saa 4:00 usiku

Timu hizi zimekutana mara moja tu katika historia ya Kombe la Dunia. Mwaka 2002, mabingwa watetezi Ufaransa walipigwa 1-0 na Senegal katika moja ya matokeo ya kushtua zaidi katika historia ya mashindano hayo. Matokeo hayo yaliashiria mwanzo wa kampeni mbaya kwa Ufaransa. Miaka 24 baadaye, Ufaransa inaweza kuwa na hamu kubwa ya kulipa kisasi.


Irak vs Norway

16 Juni, saa 7:00 usiku

Irak inarejea Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1986. Wakati huo ilipoteza michezo yote mitatu ya makundi na kufunga bao moja pekee. Safari hii itakutana na Norway yenye kikosi cha nyota kama Erling Haaland, Martin Odegaard, Alexander Sorloth na Jorgen Strand Larsen.

Norway imekuwa ikipewa nafasi ya kuwa timu ya kushtua wengi katika mashindano haya.


Ecuador vs Curacao

21 Juni, saa 9:00 usiku

Ecuador inakuja Kombe la Dunia baada ya kufanya vizuri sana katika mechi za kufuzu, ikimaliza nyuma ya Argentina huku ikifungwa mara mbili tu katika michezo 18.

Ulinzi wao imara unaweza kuwafanya kuwa mshangao wa mashindano. Kwa upande mwingine, Curaçao ni nchi ndogo zaidi kuwahi kufuzu Kombe la Dunia, jambo ambalo tayari linaifanya kuwa moja ya hadithi nzuri za mashindano hayo.


Scotland vs Brazil

24 Juni, saa 7:00 usiku

Scotland inarejea Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika karne hii. Mashabiki wake wanatarajiwa kusafiri kwa maelfu kwenda Amerika Kaskazini, na mchezo huu dhidi ya Brazil ni moja ya waliokuwa wakisubiri kwa hamu kubwa.

Ni marudio ya mechi ya ufunguzi ya Kombe la Dunia 1998, mara ya mwisho Scotland iliposhiriki mashindano haya. Je, safari hii wataweza kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia yao?


DR Congo vs Uzbekistan

28 Juni, saa 8:30 usiku

Kwa mtazamo wa kwanza, huu si mchezo unaobeba historia kubwa ya Kombe la Dunia. DR Congo ilishiriki mara moja tu 1974 kwa jina la Zaire, huku Uzbekistan ikicheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa.

Lakini, kwa kuwa Ureno na Colombia zinaonekana kuwa na nguvu zaidi katika kundi, na mchezo huo unaweza kuwa muhimu sana katika mbio za kutafuta nafasi ya kufuzuhatua inayofuata kama moja ya timu bora za nafasi ya tatu.


Jordan vs Argentina

28 Juni, saa 11:00 alfajiri

Kwa kuwa ni mchezo wa mwisho wa Kundi J, ni vigumu kujua mapema nini kitakuwa hatarini. Argentina inaweza kuwa tayari imefuzu kama kinara wa kundi, lakini pia inawezekana mechi hii ikawa na umuhimu mkubwa kwa timu zote mbili.

Jordan ni miongoni mwa timu dhaifu zaidi katika mashindano haya, wakati Argentina ni mabingwa watetezi. Hata hivyo, Kombe la Dunia limewahi kushuhudia miujiza mingi.

Argentina ilifungwa 2-1 na Saudi Arabia mwaka 2022, na mabingwa watetezi wamewahi kutolewa hatua ya makundi mara nne katika matoleo sita yaliyopita.

Mfumo mpya wa mashindano unapunguza uwezekano wa Argentina kutolewa mapema, lakini historia inaonyesha kuwa presha ya kutetea taji inaweza kuleta matokeo yasiyotegemewa.


THAMANI YA VIKOSI KOMBE LA DUNIA

1. Ufaransa         (Pauni 1.32bilioni)

2. England           (Pauni 1.13bilioni)

3. Hispania          (Pauni 1.09bilioni)

4. Ureno              (Pauni 880 milioni)

5. Ujerumani      (Pauni 862.97 milioni)

6. Brazil                  (Pauni 788.78 milioni)

7. Uholanzi          (Pauni 723.93 milioni)

8. Argentina       (Pauni 707.76 milioni)

9. Norway           (Pauni 519.68 milioni)

10. Ubelgiji          (Pauni 469.45 milioni)

11. Ivory Coast  (Pauni 459.07 milioni)

12. Morocco       (Pauni 422.15 milioni)

13. Senegal         (Pauni 408.92 milioni)

14. Uturuki          (Pauni 408.74 milioni)

15. Sweden        (Pauni 370.25 milioni)

16. Uruguay        (Pauni 350.9 milioni)

17. Croatia           (Pauni 333.51 milioni)

18. Marekani      (Pauni 327.03 milioni)

19. Ecuador         (Pauni 325.3 milioni)

20. Uswisi            (Pauni 288.46 milioni)

21. Colombia      (Pauni 263.95 milioni)

22. Japan             (Pauni 241.16 milioni)

23. Austria           (Pauni 234.94 milioni)

24. Algeria           (Pauni 222.75 milioni)

25. Ghana            (Pauni 199.64 milioni)

26. Canada          (Pauni 175.58 milioni)

27. Mexico          (Pauni 168.27 milioni)

28. Czech             (Pauni 164.45 milioni)

29. Scotland        (Pauni 152.39 milioni)

30. Paraguay      (Pauni 135.89 milioni)

31. Bosnia            (Pauni 129.04 milioni)

32. DR Congo     (Pauni 128.91 milioni)

33. Korea Kusini                (Pauni 123.07 milioni)

34. Misri               (Pauni 116.48 milioni)

35. Australia       (Pauni 63.7 milioni)

36. Uzbekistan  (Pauni 63.16 milioni)

37. Tunisia           (Pauni 60.06 milioni)

38. Cape Verde (Pauni 48.59 milioni)

39. Haiti                (Pauni 48.09 milioni)

40. Afrika Kusini  (Pauni 39.61 milioni)

41. Saudi Arabia  (Pauni 32.09 milioni)

42. New Zealand  (Pauni 30.57 milioni)

43. Panama         (Pauni 30.12 milioni)

44. Iran                 (Pauni 28.24 milioni)

45. Curacao         (Pauni 22.51 milioni)

46. Iraq                  (Pauni18.21 milioni)

47. Qatar              (Pauni 17.24 milioni)

48. Jordan           (Pauni 16.89 milioni)