Mchezaji ghali JKT milioni 10
MWANASPOTI lilipata nafasi ya kwenda kwenye kambi ya JKT Tanzania, likishuhudia shughuli mbalimbali zilizokuwa zinaendelea, kwa maana ya wapishi walikuwa wanafanya kazi yao, ila kubwa zaidi wapo wachezaji wanaolinda amani yao.
Msafara wa waandishi wa makala haya ulianzia kwenye mazoezi yao yaliyofanyika Machi 30 chini ya Kocha mkuu, Malale Hamsini kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Katika mazoezi hayo, Mwanaspoti lilifahamu upande wa pili wa kocha Malale namna alivyokuwa akiwakoromea wachezaji ambao walikuwa hawafanyi kile alichokuwa akiwaelekeza, wakati mwingine alionyesha kwa vitendo.
Kabla ya kuanza kwa mazoezi hayo saa 3:00 asubihi, Malale alianza kwa kuwasimamia kupasha misuli kwa kukimbia kuzunguka uwanja, kisha akaanza kuwanoa kwa kuwapa mazoezini mengine, hivyo yalikuwa ya nguvu na kama mchezaji hayupo fiti asingewezana nayo.
Meneja wa Uwanja huo na timu hiyo, Sajenti, Ashraf Omar Said anaeleza mipango yao namna walivyojipanga kuhakikisha wanarejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao.
"Panda shuka yetu ilitufanya tukae chini na kujitafakari tunakwama wapi, kisha tukatatua tatizo ndiyo maana umeona msimu huu, timu yetu ina ushindani wa kutosha."
Kuhusu uwanja wao, wanatarajia kuweka majukwaa, kumalizia ukarabati wa vyumba vya kubadilishia nguo za wachezaji ili waanze kuutumia msimu ujao endapo timu hiyo ikipanda daraja na imebakiza pointi chache tu kutimiza hilo.
BAJETI
Japokuwa hakutaka kuweka wazi ni kiasi gani walitenga kwa ajili ya msimu huu, ila anasema walitenga fungu la maana kuhakikisha wanasajili vizuri na mchezaji ghali kwenye kikosi chao anagharimu Sh10 milioni.
"Kuanzia benchi la ufundi, wachezaji tulijitahidi kuwekeza ndio maana unaona msimu huu tupo tofauti, hatuishii hapo tu ila tukipanda lazima tutasajili tena wa kuongeza nguvu," anasema.
Anasema katika usajili wa kikosi chao, wachezaji raia na askari wanakuwa nusu kwa nusu. "Kocha akitaja mahitaji ya wachezaji anaowataka anapewa uhuru wake."
KAMBI YAHAMISHWA
Anasema awali kambi ya timu hiyo ilikuwa jeshini, lakini kutokana na masharti mengi ambayo kwa raia wakati mwingine yalikuwa yanawapa ugumu hivyo wakaamua kuihamisha.
"Ujue sehemu za jeshi zina vitu vingi sana, ndio maana ikatafutwa nyumba ili kila mchezaji awe huru, zile amri amri waepukane nazo, pamoja na hilo bado kambi yao ina ulinzi wa kutosha kuhakikisha wanakuwa salama wakati wote," anasema.
Baada ya kupiga stori za hapa na pale na meneja huyo, safari ya kwenda kambini iliyopo maeneo ya Tegeta Namanga jijini Dar es Salaam, ikaanza na haikuchukua muda mrefu kufika eneo hilo lililoonekana tulivu na linafaa kwa mapumziko ya wachezaji.
MSOSI SASA BALAA
Baada ya kufika kambini hapo, waandishi wa makala haya waliwakuta kinamama wanaandaa msosi wa maana hasa kwa wachezaji ingawa waliokula walikuwa wachache kutokana na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na Kwaresma.
Mahojiano na daktari wa timu hiyo, Regina Nyeme anayezungumzia afya za wachezaji na namna wanavyotakiwa kuzingatia ulaji wa vyakula kwa kuzingatia programu husika ya kocha, anasema kocha anampa programu ya mazoezi, inayomfanya atoe mwongozo wa chakula cha wachezaji kwa siku.
"Kabla ya kwenda mazoezini asubuhi lazima wachezaji wanywe chai iwe ya rangi ama ya maziwa, wanaweza wakatumia chapati, mchana ugali samaki na mboga za majani za aina tatu mchicha wa kuchemsha, sukuma wiki, spinachi, dagaa na hizo mboga za majani zinasaidia kuongeza protini na lazima kuwepo na maji, tikiti, ndizi kwani mazoezi yao ni magumu kutokana na kutoka sana jasho jingi."
"Usiku wanakula wali samaki na mboga za majani lazima ziwepo, juisi ambazo zikitengenezwa kama ni tikitiki liwe peke yake, kwa kifupi hatuchanganyi matunda kiafya ndivyo inavyotakiwa.
"Kila siku ina chakula chake, mfano Jumatatu ni chai na chapati, Jumanne ni chai na viazi vitamu ama mihogo, Jumatano ni supu ya kuku wa kienyeji na chapati, Alhamisi ni chai na maandazi, Ijumaa ni supu ya nyama ya ng'ombe na chapati, Jumamosi na Jumapili supu ya samaki na mihogo ama viazi ama ndizi za kuchemsha."
Anaeleza changamoto za kiafya kwa kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma, kuna wakati mwingine anamwona mchezaji kachoka anahitaji msaada inashindikana kumsaidia kutokana na imani yake.
"Ilitokea baadhi yao waliumwa, nikawa nahitaji kuwachoma sindano walikataa, ikabidi niwatafute watu wanaojua dini, wakaniambia wanaweza wakachoma isipokuwa sehemu za wazi kama sikio, macho, pua ambazo hutumika kwa ajili ya kutilia udhu (Kuziosha) kabla ya kusali ila nyingine zote ambazo hazina uwazi wanachomwa.
"Baada ya kujua ukweli wakakiri ni kweli, hilo angalau limepita, ila kipindi hiki ni kigumu zaidi," anasema.
Nje na hilo amekiomba Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), baada ya kumalizika ligi zote watenge muda wa kukutana ili kujadiliana changamoto ambazo wamekutana nazo, kisha wazitafutie ufumbuzi.
"Kama inavyofanyika kwa makocha na waamuzi, tukifanya hivyo yapo matatizo ambayo yatapungua na afya za wachezaji zitakuwa salama zaidi," anasema.
NENO LA NAHODHA
Kiongozi wa wachezaji wa timu hiyo (nahodha), Edward Songo anasema kuna wakati timu haikufanya vizuri mwanzoni, kigogo wa juu alihoji mbona timu nyingine zinafanya vizuri na wao wanakwama wapi.
"Mkuu akiongea hapingwi, ilibidi nikae na wachezaji wenzangu kuitafakari amri ya mkuu, tulipewa adhabu ya kushinda mechi 10 mfululizo, tukashinda tisa na kupoteza moja angalau tukapata unafuu.
"Mfano nisipofunga nulizwa kwa nini hufungi na kwa sababu mimi ni askari napigishwa pushapu, hivyo huu msimu tumepambana na bado tunapigania pointi tano ili tujihakikishie kupanda," anasema.
Anataja tofauti na kukaa kambi ya jeshi na uraiani "Jeshini huruhusiwi kuzurura nje, yapo maeneo hupaswi kupita, ila huku unaweza ukaenda hadi dukani ingawa kipindi ambacho tulipewa kushinda mechi 10 ilikuwa hakuna kutoka getini, ukikamatwa unahojiwa," anasema.
Pamoja na hilo, lilishuhudiwa tukio la wachezaji wa dini ya kiislamu, ulipofika muda wa kusali, waliandaa sehemu ya kufanyia sala ya Adhuhur, kisha wakaanza kuswali kwa nyakati tofauti.