Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Maximo kama Mourinho, nyakati zimewapita

JICHO Pict


ALISIKIKA Rais wa Fenerbahce, Alic Koc wakati akimfukuza kocha Jose Mourinho, Septemba mwaka huu. Alisema: “Tulijua kocha wetu angesisitiza sana katika ulinzi wakati ule tumeleta. Lakini tuliongea naye umuhimu wa kucheza soka safi na kutawala mechi.”

Hatimaye, Mourinho mwenye umri wa miaka 62 kwa sasa ameangukia Benfica. Ni endelezo la anguko lake. Tatizo sio umri. Carlo Ancelotti hadi kufikia umri wa miaka 66 alikuwa anafundisha Real Madrid.


Nimemkumbuka Mourinho kama nilivyomkumbuka rafiki yangu, Marcio Maximo. Majuzi alifukuzwa na klabu ya KMC baada ya kupokea vichapo saba akiwa na timu. Hakuweza kuipa msaada wowote wa kiufundi KMC. Ni huzuni. Wote wawili, Maximo na Mourinho wana sifa mbili na ushujaa wa zamani.

Wakati Mourinho alitumia staili yake ya soka la kujihami na kupata mafanikio akiwa na klabu za Porto, Chelsea, Inter Milan na nyinginezo, Maximo aliingia nchini mwaka 2006 na kuliteka soka la Tanzania katika timu ya Taifa kwa soka la namna hiyo hiyo.

JICH 01

Tofauti ya Maximo na Mourinho ilikuwa ndogo tu. Kwamba Mourinho alikuwa katika ngazi ya klabu akifundisha wachezaji wakubwa, wakati Maximo alitumia soka hilo hilo akiwa na timu ya taifa dhaifu lenye wachezaji wasio na uwezo mkubwa na lengo lilikuwa kupata matokeo hata ya sare ili kuleta furaha kwa Watanzania.

Maximo alikuwa na hamasa kwa wachezaji na mashabiki. Akaendeleza hamasa hata kwa kampuni zilizokuwa zinaidhamini Taifa Stars pamoja na viongozi wa nchi. Uwanjani hatukucheza soka safi. Tulitumia muda mwingi kujihami.

Alikuwa anacheza na mshambuliaji mmoja pale mbele. Muda mwingi alikuwa Gaudence Mwaikimba. Kisha kukawa na mchezaji mmoja mwenye kasi ya kumfikia Mwaikimba. Alianza na Said Maulid kisha baadaye akamalizia na Mrisho Ngassa.

JICH 02

Kwa mahitaji yetu ya wakati huo tuliona alikuwa shujaa. Unapataje suluhu na Msumbiji ugenini? Unashindaje bao moja la bahati bahati dhidi ya Burkina Faso ugenini? Haya ndio mambo ambayo yalimpa ushujaa Maximo.

Baadaye tukaachana naye. Mpira ukabadilika zaidi duniani. Yanga wakamrudisha tena nchini Maximo chini ya utawala wa Yusuph Manji mwaka 2014. Tofauti ya mahitaji ya Yanga ilimkwamisha Maximo. Alikuja na mpira ule ule wakati Yanga kama timu kubwa walikuwa wanapenda kutawala mechi.

Yanga wakagundua kwamba walikuwa wameiingia katika majanga wakaachana naye. Sijui KMC waliona nini kuhusu Maximo wakaamua kumrudisha nchini. Tupo katika dunia ambayo timu nyingi zinazocheza soka safi ndizo huwa zinapata matokeo.

JICH 03

Maisha ya ‘counter attack’ katika mpira yanatoweka. Nadhani mabosi wa KMC waliamua kulileta jina lake nchini bila ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu aina ya mpira wa Maximo. Leo tuna makocha bora nchini ambao wanaweza kufundisha soka la kutawala mechi kuliko Maximo.

Kuna Ahmad Ally yupo JKT Tanzania, kuna Juma Mgunda yupo Namungo, kuna Habib Kondo ambaye sidhani kama ana timu. Wote hawa wanaweza kufundisha mpira mzuri kuliko Maximo. Sijui mabosi wa KMC waliona nini kwa Maximo.

Nilichojua ni kwamba asingewasaidia. Uamuzi kama huo waliwahi kuuchukua Tottenham Hotspur wakati walipomchukua Mourinho, ingawa alikuwa katika anguko lake. Aina ya mpira wao Maximo na Mourinho umepitwa na wakati.

JICH 04

Kucheza mpira wa kuviziavizia bila ya kujali kuitawala mechi, ni aina ya mpira ambao umepitwa na wakati. Siku hizi tunaona hata katika timu ndogo za kawaida wachezaji wanaanza kucheza soka kutokea nyuma. Hawachezi kwa kubahatisha.

Kipa anaanza kwa mabeki wake, anarudishiwa kwa miguu na habutui mbele. Anatafuta namna gani wataanzisha shambulizi kuanzia nyuma. Mpira wa pasi moja ndefu ya kumpigia Didier Drogba au Mwaikimba umepitwa na wakati.

Kitu kibaya zaidi kwa aina ya makocha kama Maximo na Mourinho huwa wanashindwa kubadilika kutokana na nyakati. Hawaamini zaidi katika falsafa za mpira wa kisasa na wanaamini katika kile ambacho kiliwahi kuwapa umaarufu katika siku za nyuma.

JICH 05

Tatizo ni kwamba mbinu za kisasa zimekwenda mbali zaidi kuliko wao na ndio maana wamejikuta wakiangukia katika timu ndogo. Mfano ni Mourinho mwenyewe. Leo yupo Benfica baada ya kupitia timu kadhaa ndogo. Unaamini anaweza kutwaa ubingwa wa Ulaya akiwa na Benfica hii? Ni ndoto.

Alifanya hivyo akiwa na Porto kwa sababu nyakati zile ziliruhusu. Mwaka huo huo aliotwaa ubingwa wa Ulaya na Porto ndio mwaka huo huo ambao Ugiriki ilitwaa michuano ya Euro. Wakati huo mbinu za kujihami ziliruhusu.

Leo mbinu za kujihami ni nadra kufanya kazi kwa sababu kina Pep Guardiola wameongeza makali yao katika kuzifungua kuta ngumu.

Kuna timu nyingi zingetamani kuwa na Mourinho, lakini kadri wanavyotazama mpira wa kisasa unavyokwenda wamegundua kwamba kocha huyo Mreno kwa sasa hawezi kuwasaidia.

Kila la kheri kwa rafiki Maximo. Wakati mwingine hadithi nzuri ni ile ambayo inaishia patamu. Nadhani asingerudi kuifundisha Yanga wala KMC pengine jina lake lingekumbukwa milele kwa namna ambavyo alitusaidia wakati ule kwa mambo mengi tu ikiwamo kufuzu michuano ya Chan kwa mara ya kwanza.

Kwa hali ilivyo sasa naona amejivunjia heshima kwa kiasi kikubwa.  Kufukuzwa na Yanga kisha KMC kumetia dosari kwa kiasi kikubwa heshima aliyojijengea wakati ule tulipouhitaji mpira wake. Hata hivyo, siwezi kumlaumu kwa sababu ukocha ni kazi yake. Anahitaji kuisukuma familia yake kwa kupitia mpira. Hata hivyo, ujio wake mara mbili katika soka la Tanzania umeyumbisha wasifu wake kwa Watanzania.