Matunda 10 ya kula kwa ajili ya ngozi nzuri
Muktasari:
- Wapo wanaokimbilia bidhaa za gharama wakitaka ngozi iwe laini, yenye unyevunyevu na yenye mwonekano mzuri, huku matunda yakipita pembeni kana kwamba hayana kazi. Ukweli ni kwamba baadhi ya matunda yana virutubisho vinavyosaidia mwili kutengeneza kitu kikubwa kama kulinda seli za ngozi, kusaidia ngozi yenye ukavu na kuupa mwili maji.
UKIWA unatumia hela nyingi kununua krimu, mafuta na vipodozi mbalimbali lakini bado unajiuliza kwa nini ngozi yako haing’ai, huenda tatizo si kwenye kioo unachojitazamia kila siku, bali kwenye sahani unayokula. Ndiyo, usishangae. Ngozi haijengwi kwa vipodozi pekee, bali hata kile unachokula kinaweza kuwa na mchango mkubwa katika mwonekano na afya yake.
Wapo wanaokimbilia bidhaa za gharama wakitaka ngozi iwe laini, yenye unyevunyevu na yenye mwonekano mzuri, huku matunda yakipita pembeni kana kwamba hayana kazi. Ukweli ni kwamba baadhi ya matunda yana virutubisho vinavyosaidia mwili kutengeneza kitu kikubwa kama kulinda seli za ngozi, kusaidia ngozi yenye ukavu na kuupa mwili maji.
Hapa tunakuletea matunda 10 ambayo unaweza kuyaweka kwenye mlo wako mara kwa mara ili kuupa mwili virutubisho muhimu kwa afya ya ngozi.
PARACHICHI KWA NGOZI KAVU
Parachichi ni moja ya matunda yanayoweza kuwa rafiki kwa mtu mwenye ngozi kavu. Lina mafuta mazuri pamoja na vitamin E, ambayo husaidia kulinda seli za mwili dhidi ya uharibifu.
Daktari wa ngozi Dorcas Natse anasema;”Mafuta mazuri yaliyopo kwenye parachichi yana umuhimu katika lishe kwa sababu mwili huyatumia katika kazi mbalimbali.
Kwa mtu mwenye ngozi kavu, kuwa na lishe yenye mafuta mazuri ni sehemu ya kuitunza ngozi kutoka ndani.”
PAPAI
Daktari wa Natse anasema vitamin C inahusika katika utengenezaji wa collagen, ambayo husaidia ngozi kuwa na uimara na muundo wake wa kawaida.
“Vitamin A pia ina nafasi katika ukuaji na uundaji wa seli za ngozi. Kwa hiyo, papai linaweza kuwa sehemu ya lishe inayosaidia mwili kupata virutubisho muhimu kwa afya ya ngozi,” anasema.
EMBE
Anasema; “Vitamin C husaidia mwili kutengeneza collagen, wakati vitamin A ina nafasi katika afya ya seli za ngozi. Hii ndiyo sababu embe linaweza kuwa sehemu ya mlo wa mtu anayejali afya ya ngozi yake.”
TIKITI MAJI
Tikiti maji lina maji mengi, hivyo linaweza kusaidia kuongeza maji mwilini. Ngozi ikiwa katika hali nzuri ya maji, huwa na nafasi nzuri ya kudumisha mwonekano wake wa kawaida.
Pia lina vitamin C na virutubisho vingine vinavyosaidia kulinda seli za mwili. Lakini usifanye kosa la kuacha maji ya kunywa ukitegemea tikiti maji pekee.
MAPERA KWA UIMARA WA NGOZI
Anasema; “Mapera ni tunda ambalo watu wengi hulila bila kujua kwamba lina vitamin C kwa kiwango kizuri. Vitamin C ni muhimu kwa sababu mwili huitumia katika kutengeneza collagen.
Collagen husaidia kutoa muundo na uimara wa ngozi. Kwa hiyo, kupata vitamin C ya kutosha kupitia vyakula kama mapera ni muhimu katika lishe ya mtu anayejali afya ya ngozi.”
NDIZI
Anasema,”Ndizi huenda zisitajwe sana kwenye mada za urembo, lakini zina virutubisho muhimu kwa mwili. Zina potassium na vitamin B6, ambazo zinahitajika katika kazi mbalimbali za mwili.
Potassium husaidia mwili kufanya kazi zake kwa kawaida, ikiwemo kazi za misuli na seli. Mwili unapokuwa na afya nzuri kwa ujumla, hilo pia lina umuhimu katika afya ya ngozi.”
ZABIBU
“Zabibu zina virutubisho vinavyosaidia kulinda seli za mwili. Miongoni mwa virutubisho hivyo ni antioxidants, ambazo husaidia mwili kupambana na uharibifu wa seli.”
STROBERI
Anasema, “Stroberi ina vitamin C, kirutubisho ambacho mwili huhitaji katika utengenezaji wa collagen.
Collagen ni muhimu katika kuifanya ngozi iwe na muundo na uimara wake wa kawaida.
Hivyo, kupata vitamin C kutoka kwenye matunda kama stroberi ni sehemu ya lishe inayoweza kusaidia afya ya ngozi.”
NANASI
“Nanasi lina vitamin C ambayo ina nafasi katika utengenezaji wa collagen. Hii inafanya nanasi kuwa miongoni mwa matunda yanayoweza kuongezwa kwenye mlo wa mtu anayejali afya ya ngozi.”
MACHUNGWA
“Machungwa ni chanzo kizuri cha vitamin C. Kirutubisho hiki kina nafasi kubwa katika utengenezaji wa collagen, ambao ni muhimu kwa muundo na uimara wa ngozi.
Vitamin C pia husaidia kulinda seli za mwili. Kwa hiyo, kula chungwa zima ni njia rahisi ya kuongeza vitamin C kwenye mlo wako.”
USHAURI
Kwa hiyo, kama unataka kuitunza ngozi yako, usiangalie kioo pekee. Angalia pia kile unachokula. Parachichi linaweza kusaidia kwenye lishe ya mtu mwenye ngozi kavu, papai na mapera vina vitamin C na virutubisho vinavyohusika na afya ya ngozi, tikiti maji husaidia kuongeza maji mwilini, huku embe, stroberi, nanasi na machungwa vikitoa vitamin na virutubisho muhimu.