Ukivaa hivi kazini utavutia
Muktasari:
- Wengine huvaa nguo nzuri lakini wanashindwa kuzichanganya vizuri, matokeo yake badala ya kuonekana nadhifu wanapunguza mvuto wao. Ukweli ni kwamba huna haja ya kuwa na kabati lililojaa nguo za gharama kubwa ili unoge kazini.
KUNA watu kila Jumatatu wanaingia ofisini wakionekana kama viongozi wakubwa wa kampuni, lakini ukifika Jumatano tayari wanakuwa wameishiwa mawazo ya mavazi.
Wengine huvaa nguo nzuri lakini wanashindwa kuzichanganya vizuri, matokeo yake badala ya kuonekana nadhifu wanapunguza mvuto wao. Ukweli ni kwamba huna haja ya kuwa na kabati lililojaa nguo za gharama kubwa ili unoge kazini.
Unachohitaji ni kujua nini uvae kila siku ya kazi, jinsi ya kuoanisha rangi na kuchagua mavazi yanayolingana na mazingira ya ofisi. Ukifanya hivyo, kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa utakuwa ukitoka nyumbani ukiwa na muonekano unaovutia, unaoonyesha kujiamini na unaokuongezea heshima mbele ya kila mtu.
JUMATATU – VAA KITAALUMA
Jumatatu ndiyo siku ya kuanza wiki mpya, hivyo ni muhimu kuvaa mavazi yanayoonyesha umakini na weledi. Wanaume wanaweza kuchagua suti ya rangi ya daki bluu kwa wapenda suti, nyeusi, kijivu au kahawia pamoja, kwa wale wa mashati vaa jeupe au la rangi tulivu.
Kwa wanawake, gauni la ofisini lisilobana sana au suti yenye blazer ni chaguo zuri. Viatu safi vya kufunika vidole na mkoba au begi la kazi vitakamilisha muonekano.
Epuka nguo zenye michoro mingi au rangi zinazopiga kelele siku ya Jumatatu kwa kuwa zinapunguza uhalisia wa kitaaluma.
JUMANNE – ZINGATIA RANGI
Baada ya kuanza wiki vizuri, Jumanne ni siku ya kuongeza ubunifu kwenye mavazi. Wanaume wanaweza kuvaa suruali ya kitambaa yenye rangi nyeusi, kijivu au krimu pamoja na shati la rangi nyepesi kama light blue au pinki iliyopoa.
Wanawake wanaweza kuvaa suruali ya kitambaa au sketi ya ofisini wakaiunganisha na blauzi yenye rangi tulivu.
Mchanganyiko huu huwafanya wafanyakazi waonekane wenye kujiamini, wanaopenda mtindo na wanaovutia bila kupitiliza.
JUMATANO – VAA JIACHIE KIDOGO
Katikati ya wiki ni wakati mzuri wa kuvaa mavazi yanayokupa nafasi ya kufanya kazi kwa uhuru huku ukiendelea kuonekana nadhifu.
Wanawake wanaweza kuvaa gauni la ofisini au sketi na blauzi, huku wanaume wakichagua suruali ya kitambaa na shati la mikono mirefu au mifupi kulingana na utaratibu wa sehemu yao ya kazi.
Rangi kama Daki bluu, Ugoro iliyopoa, Chocolate, maroon au kijivu huongeza mvuto na kuonyesha kuwa hujapania sana kuvaa ila wewe ni mtu msafi unaejipenda.
ALHAMISI – VAA KIMTOKO KIDOGO
Alhamisi ni siku ambayo wafanyakazi wengi hupendelea muonekano wa kisasa lakini usiowatoa kwenye mstari wa kiofisi au kazi.
Kwa wanaume, suruali ya jeans iliyotulia ambayo haijachakina, shati safi na blazer huleta muonekano wa kuvutia. Kwa wanawake, suruali ya kitambaa au sketi ikiambatana na blazer na blauzi nzuri ni chaguo linaloendana na mazingira mengi ya kazi.
Viatu vya ngozi vilivyosafishwa vizuri huongeza hadhi ya muonekano kwa jinsia zote.
IJUMAA – JIACHIE
Katika maeneo mengi ya kazi, Ijumaa huwa na uhuru kidogo wa mavazi. Hata hivyo, uhuru huo haupaswi kuondoa hadhi ya ofisi.
Wanaume wanaweza kuvaa jeans ya rangi nyeusi au dark blue isiyochanika pamoja na shati la kola au blazer nyepesi. Wanawake wanaweza kuvaa jeans nzuri na blauzi nzuri, gauni la kali linalobana kidogo.
USIACHE VIATU
Viatu vina mchango mkubwa katika muonekano wa mfanyakazi. Viatu safi, vinavyong'aa na vinavyoendana na mavazi huongeza mvuto na kuonyesha uko umakini.
Rangi kama nyeusi, kahawia au cream ni rahisi kuendana na mavazi mengi ya ofisini. Epuka viatu vilivyochakaa, vichafu au visivyolingana na mazingira ya kazi.
USISAHAU HIVI
Mkoba, saa, mkanda, tai kwa wanaume au hereni na mkufu mfupi wa kawaida kwa wanawake ni vitu vinavyoweza kuboresha muonekano. Hata hivyo, usitumie vitu vingi kwa wakati mmoja. Chagua vinavyokamilisha muoekano wako.
USICHANGE RANGI UTACHEKESHA
Wanamitindo wengi hushauri kutumia rangi zisizozidi tatu katika vazi moja. Hii hufanya mwonekano uwe wa kuvutia na wenye mpangilio.Ukichagua nguo ya rangi kali, basi viatu, mkanda au begi viwe na rangi tulivu ili kuleta usawa mzuri.
USAFI MUHIMU
Haijalishi nguo yako ni ya bei gani, ikiwa imekunjamana, imefifia au ina madoa, haitakufanya uonekane nadhifu.Hakikisha nguo zako zimepigwa pasi vizuri, viatu vimesafishwa na vifaa vyako vya kazi viko katika hali nzuri kila siku unapoenda kazini.