Mastaa 9 wamchomoa Saido Yanga

Sunday October 10 2021
mastaa pic
By Mwandishi Wetu

KUNA uvumi flani unadai kocha wa Yanga Nesreddine Nabi amezichapa na mshambuliaji wake mkongwe Saido Ntibazonkiza, lakini wenyewe wawili hakuna aliyetolea ufafanuzi hilo na uchunguzi umebaini kuna mastaa tisa ndiyo wanamuondoa straika huyo Mrundi.

Iko hivi msimu huu Saido amevaa jezi katika mechi mbili pekee zile za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United na zote akiingia kipindi cha pili.

Hata hivyo kuna ugumu mkubwa wa mshambuliaji huyo kuanza kikosi cha kwanza au hata kukaa benchi kutokana na uwepo wa mastaa tisa tofauti pamoja na kanuni za ligi.

Iko hivi kanuni ya 62 ya ligi inaeleza kuwa kila klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji 12 wa kigeni na kati ya hao ni nane pekee wanaruhusiwa kuanza mchezo mmoja.

Yanga ambayo msimu huu imesajili wachezaji 10, katika mechi mbili za ligi imewatumia nane pekee huku wawili wakikosekana kwa sababu mbalimbali na kiungo Mukoko Tonombe ambaye amesimamishwa akitumikia adhabu ya kukosa mechi tatu na mwingine ni Saido.

Hata hivyo, Yanga kuanza na wachezaji nane katika mechi hizo mbili kumeonekana kuminya nafasi ya Saido kutokana na umuhimu wa wachezaji hao ambao wanakwenda kuamua ugomvi wa kocha huyo na mshambuliaji huyo.

Advertisement

Ugomvi mkubwa wa Nabi na Saido, Mwanaspoti linafahamu kwamba mshambuliaji huyo hafurahii kukosa mechi na kukaa jukwaani, lakini uwepo wa mastaa hao unamnyima nafasi ya Nabi kumpa nafasi.

Nabi amewatumia kipa Diarra Djigui, mabeki Djuma Shaban, Yannick Bangala wakati katikati viungo kuna Khalid Aucho na Jesus Moloko ilhali katika ushambuliaji akianza Yacouba Sogne na Fiston Mayele, huku Heritier Makambo akitokea benchi.

Upande wa pili mfumo wa Nabi akimtumia kiungo Feisal Salum kama kiungo mshambuliaji - yaani namba 10 amekuwa mchezaji wa tisa kumpokonya namba Saido kutokana na jinsi anavyokuwa muhimu katika mifumo yake.

Nabi anataka kasi ya Feisal katika kupandisha mashambulizi, pia uwezo wake wa kuja kati kusaidia ukabaji na zaidi kiungo huyo akiwa katika kiwango bora kwa sasa akiwa tayari amepachika bao moja ndani ya mechi mbili imezidi kuongeza makali kwa Saido kupewa nafasi.


Msikie Nabi

Mapema Nabi aliliambia Mwanaspoti kuwa sio rahisi kumweka nje Feisal na kumpa nafasi Saido kutokana na jinsi anavyotekeleza yale anayotaka katika mfumo .

“Narudia sina tatizo na Saido, namheshimu sana lakini niseme wazi mfumo wangu unanilazimu kuendelea kumuamini Feisal zaidi kutokana na jinsi anavyotekeleza kile ambacho tunataka kukifanya kwenye timu,” alisema Nabi.

“Feisal bado ni kijana mdogo, ana nguvu za kuja kati na kusaidia ukabaji, soka la kisasa linahitaji hilo kama, unakuwa na timu yenye wachezaji wengi wanaojua kutafuta mipira unakuwa na urahisi kushinda.”


Wasikie wadau

Kocha mkongwe na mkufunzi wa Caf, Abdul Mingange anasema Nabi yupo sahihi kutomtumia Saido kwa sasa kutokana na aina ya usajili ambao Yanga imeufanya.

Anasema mchezaji wa kwanza anayemuondoa Saido katika mfumo wa Nabi ni Feisal ambaye jinsi anavyong’ara akiwa kama namba 10 kunaweka wakati mgumu matumizi ya mchezaji huyo.

“Saido hawezi kupata nafasi kirahisi pale Yanga. Sio kwamba Nabi hajampa nafasi, lakini kwa jinsi Yanga ilivyosajiliwa sasa inamnyima nafasi ya kuanza wala kukaa benchi. Unajua hizi timu zina presha, sasa kocha lazima atataka kuwatumia watu ambao wanampa matokeo,” anasema.

“Wamekuja watu ambao wako juu yake (Saido). Mchawi wake wa kwanza ni Feisal, Saido hawezi kucheza kama winga kwa mpira ambao anautaka Nabi au akitumia mfumo wa 4-3-3, wale wachezaji wawili wa pembeni wanakuwa kama washambuliaji pia wanageuka kuwa viungo.

“Watu hawamuangalii yule Moloko, hapa Yanga imepata mchezaji anapandisha mashambulizi na anakuja kusaidia kukaba. Mchezaji ni lazima ukabe, kile anachofanya Moloko kinamsaidia sana beki wa kulia na timu kwa ujumla. Sasa Saido hawezi kukimbia sana kama ambavyo anakimbia Moloko au Feisal, ni kweli Saido ni mchezaji mzuri na anayejua lakini mpira wa sasa unamnyima nafasi unataka mtu anayekimbia sana ndani ya uwanja.”

Naye kocha Ulimboka Mwakingwe anasema: “Huwezi kumlinganisha anachofanya Feisal sasa na Saido ni lazima tuwe wazi. Ni kweli Saido ni mchezaji mzoefu na anaweza kufanya kitu, lakini kwa kiwango cha Feisal sasa unamuwekaje nje. Lakini mechi ziko nyingi kitu ambacho Saido anatakiwa kukifanya ni kuendelea kujiweka sawa tayari kwa mechi zingine hii ni ligi inaweza kuja kutokea mtu akaumia atapata nafasi,” anasema Mwakingwe.

“Unajua ukiangalia Yanga ina watu bora kwa sasa, mnamzungumzia Saido vipi Mukoko akirudi leo hali itakuwaje. Kwa hiyo nafikiri bado ana nafasi lakini subira inatakiwa.”

Advertisement