Marcio Maximo azitaja Simba, Yanga zinavyopiga bao wengine
Muktasari:
- Maximo anasema jambo muhimu zaidi ni kuendelea kuamini katika mchakato wa maendeleo ya muda mrefu unaolenga kukuza vipaji vya ndani kitu ambacho KMC inaonekana kukiwekea makazo huku ikijenga miundombinu yake.
KOCHA wa KMC, Marcio Maximo anaiona klabu hiyo ikiwa na kesho bora zaidi kutokana na uwekezaji unaofanywa na Manispaa ya Kinondoni, akiamini miaka michache ijayo itatoa wachezaji wenye uwezo wa kucheza soka la kulipwa Ulaya.
Maximo anasema jambo muhimu zaidi ni kuendelea kuamini katika mchakato wa maendeleo ya muda mrefu unaolenga kukuza vipaji vya ndani kitu ambacho KMC inaonekana kukiwekea makazo huku ikijenga miundombinu yake.
Mbrazil huyo, ambaye amewahi kufundisha timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), anaamini mafanikio hayaji kwa bahati mbaya, bali kwa kupanga na kuwekeza kwenye misingi ya soka la vijana. Anasema safari ya KMC inapicha kubwa ambayo inaweza kuipa matunda Tanzania.
Katika mahojiano maalum na Mwanaspoti, Maximo anasema tofauti na klabu nyingi ambazo hutegemea usajili wa wachezaji wa kigeni, KMC imekuwa mfano kwa kutoa nafasi kwa wachezaji wa ndani zaidi, jambo analoliona kama hatua ya kujenga utambulisho wa klabu na taifa kwa jumla.
"Ninafurahia kuwa hapa, naiona kesho nzuri kwa klabu hii, inawezekana kuzalisha wachezaji wengi wenye misingi mizuri ya soka ambayo itawasaidia kufika mbali, Tanzania inawachezaji wengi sana wenye vipaji lakini vinakosa misingi," anasema.
KIKOSI CHAKE
Licha ya kuanza ligi kwa kushinda mechi moja na kupoteza mbili mfululizo dhidi ya Singida Black Stars na Tanzania Prisons kwa bao 1-0 kwenye kila mechi, Maximo anajivunia kuwa na kikosi mchanganyiko chenye vijana wengi pamoja na wachezaji wazoefu wanaotoa mwongozo kwa chipukizi.
“Ninafurahishwa na kikosi nilicho nacho. Tuna vijana wengi wenye vipaji vikubwa. Tuna uhusiano mzuri na timu zetu za vijana chini ya miaka 17 na 20. Wapo baadhi niliowapandisha kwenye timu ya wakubwa, huenda ukashuhudia makubwa kutoka kwao hivi karibuni,” anasema.
Anaongeza wachezaji wazoefu waliopo hutoa hamasa na mfano bora kwa vijana, hali inayounda moyo wa ushindani ndani ya timu.
“Utaona kwenye mazoezi, kila mchezaji anapambana, anataka kuboresha kiwango chake. Huu ndiyo moyo tunaoutaka KMC iwe nao,” anafafanua Maximo.
NAFASI YA AJIBU
Kuhusu maoni ya wengi juu ya uwezo wa Ibrahim Ajibu, Maximo anaeleza mchezaji huyo bado yuko kwenye mchakato wa kufikia ubora unaotakiwa.
“Ajibu ni mchezaji mzuri, lakini anahitaji muda. Tunamwandaa kwa ajili ya baadaye. KMC hatuchagui mchezaji kwa CV yake, bali kwa kile anachoonyesha uwanjani. Atakuwa muhimu kwa wakati sahihi,” anasema.
Tangu ajiunge na timu hiyo, Ajibu hajawa na nafasi ya kutosha kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
DIRA YA KMC
Kwa Maximo, KMC si tu klabu inayoshiriki ligi, bali ni taasisi ya kukuza vipaji vya ndani. Anasema zaidi ya wachezaji 120 wako chini ya mfumo wa KMC kuanzia timu ya vijana chini ya miaka 17 hadi kikosi cha wakubwa.
“KMC ina wachezaji wote wa Kitanzania. Hii ni nafasi kubwa kwa vijana wa nchi hii kuonyesha uwezo wao. Mwaka hadi mwaka timu zetu za vijana zitakuwa imara zaidi. Hiyo ndiyo njia sahihi ya kujenga klabu yenye misingi,” anaeleza.
Anaongeza; “Ninafuraha kwa sababu kwa sasa inajenga gym mpya, tunaboresha idara ya tiba na tumeanzisha chumba cha video kwa ajili ya uchambuzi wa michezo. Lengo ni kuwapa wachezaji mazingira bora ya kukua kimchezo na kiakili.”
MIPANGO YA USAJILI
Kuhusu mipango ya dirisha la usajili la Januari, Maximo anakiri benchi la ufundi linawafuatilia baadhi ya wachezaji, ingawa anasisitiza ushindani wa ndani ya timu ndiyo kipaumbele chake.
“Ni kweli, tunafuatilia baadhi ya majina, lakini siwezi kuyataja sasa. Wachezaji waliopo wanajua ushindani upo, lakini ushindani wa uwanjani tu na sio wa chuki. Ndiyo njia bora ya kila mchezaji kujituma zaidi,” anasema.
KMC NA VIGOGO
Maximo anakiri pengo la rasilimali kati ya KMC na klabu kubwa, lakini anaamini pengo hilo litafutika kadri KMC inavyoendelea kuwekeza.
“Ni vigumu kulinganisha KMC na Simba au Yanga kwa sasa. Wana rasilimali kubwa zaidi, wanacheza mechi nyingi za kimataifa na wamewekeza kwenye miundombinu. Lakini naamini katika miaka michache ijayo, tukidumisha mwelekeo huu, tutakuwa kwenye kiwango chao,” anasema.
KUHUSU TAIFA STARS
Akiulizwa kuhusu maendeleo ya soka la Tanzania tangu kuondoka kwake kama Kocha wa Taifa Stars, Maximo anakiri ni vigumu kutoa maoni ya kina kwa kuheshimu kocha aliyepo, lakini anasema ana matumaini makubwa.
“Si rahisi kutoa maoni juu ya Taifa Stars kwa sababu kuna kocha kazini ambaye namheshimu. Lakini natamani kuona Tanzania ikipiga hatua zaidi na kufikia nafasi inayostahili barani Afrika,” anasema.
MAISHA TANZANIA
Licha ya kuwa raia wa Brazil, Maximo anasema Tanzania ni nyumbani kwake na anajisikia fahari kuwa hapa.
“Nimeishi Tanzania kwa miaka mingi. Nimezoea kabisa. Watu ni wakarimu, napenda maisha hapa. Hii ni nchi yangu ya pili,” anasema akitabasamu.
Anapoulizwa kuhusu vyakula na muziki anaouvutiwa nao, anakiri kupenda mihogo, mishkaki na muziki wa Bongo Fleva.
“Napenda mihogo, mishikaki… na napenda muziki wa Bongo, hasa ule wa dansi na Fleva. Muziki wa Tanzania una fleva nzuri, unaenda sambamba na mpira,” anasema akicheka.