Prime
Mambo 10 katika Jicho la Mwewe Stars ya AFCON
TUPO Morocco tunacheza kwa raha zetu. Mechi ya kwanza tumewaduwaza Nigeria. Sawa tumefungwa 2-1, lakini haikuwa mechi rahisi sana kwao. Juzi tumetoka sare na Waganda. 1-1. Majirani walikosa penalti dakika za lala salama.
Kuna jicho la mwewe nimelipitisha katika kikosi cha kocha Manuel Gamondi. Kitu cha kwanza. Stars imebadilika. Kutoka kwa Hemed Morocco kuja kwa Manuel Gamondi Stars imebadilika. Kuna kasi fulani imeongezeka katika timu katika suala zima la ujenzi wa mashambulizi. Tunashambulia kwa idadi kubwa ya watu.
Chini ya Morocco hatukuweza kujenga mashambulizi mengi. Stars hii ina muundo mzuri wa mashambulizi. Hata hivyo, unachoweza kumsifu Morocco kwa Gamondi ni kwamba Stars yake ilikuwa inacheza kwa kujihami vizuri. Mabao ya Nigeria yalikuwa rahisi.
Bao la Uganda lilikuwa rahisi. Morocco alikuwa mzuri katika kucheza ‘compact’ lakini Gamondi amekuwa mzuri katika kujiachia na suala la kushambulia.
Kitu cha pili. Stars ya Gamondi imeondoa kwa kiasi kikubwa suala la Usimba na Yanga. wachezaji wetu kutoka nje wameonyesha kiwango kizuri. Wachezaji wengi ambao wamepangwa baada ya ukuta wa nyuma sio wa Simba wala wa Yanga na wameuwasha vizuri tu.
Gamondi hajakariri sana majina. Mfano, Alphonce Mabula anauwasha vema tu. wengi walikuwa hawamfahamu kwa sababu hadi wakati anaondoka nchini alikuwa hajacheza Simba wala Yanga.
Kuna mzungu wetu ambaye ni kipenzi cha mashabiki, Tarryn Allarakhia anawasha moto vema. Ni roho ya timu katika kuisogeza timu mbele. Novatus Dismas amekuwa bora kwa mara nyingine tena.
Kitu cha nne. Tujifunze jambo kutoka katika kuufahamu mpira. Mashabiki wengi walikuwa wanamlilia Kevin John kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa. Alianza pambano la juzi huku nahodha Mbwana Samatta akikaa benchini.
Kevin alicheza vizuri, lakini kuna mashabiki walikuwa na maoni tofauti kuhusu yeye. Kwamba walitaka atolewe wakati wa mapumziko kwa sababu hakufanya kitu. Ukweli ni kwamba unapocheza katika kikosi cha timu kama ya Tanzania hauwezi kufanya maajabu peke yako.
Mashabiki wale wale ambao walikuwa wanasema Samatta atupishe baada ya kiwango chake dhidi ya Nigeria, ndio wale wale ambao walisema Kevin ampishe Samatta katika pambano dhidi ya Uganda.
Kule mbele sio kwepesi kama watu wengi wanavyofikiria. Ni kugumu. Na sasa tutafunga midomo na kuwaheshimu wanaocheza.
Kitu cha tano. Tumuheshimu Bakari Mwamnyeto. Watu wengi huwa wanamdharau nahodha Nondo. Kuanzia katika klabu yake hadi timu ya taifa. Sijui kwanini. Hata hivyo, safari hii amepata muda wa kutukumbusha ubora wake akiwa katika jukwaa kubwa.
Nondo anaonyesha uzoefu. Anaonyesha uongozi wake. Katika mechi zote mbili amekuwa bora. Chini ya Mzungu Gamondi Nondo anafaidika kupangwa pale katikati kwa sababu ya kimo chake. Anacheza kando ya Ibrahim Bacca.
Kumbe Gamondi alikuwa na kitu moyoni wakati anafundisha Yanga. Inawezekana alikuwa na shinikizo la kuwapanga zaidi Job na Bacca. Kwanini katika kikosi chake cha Stars ameamua kwenda na Nondo na Bacca? Inanikumbusha wakati ule wa Marcio Maximo alipoamua kwenda na Ivo Mapunda badala ya Juma Kaseja.
Jambo la sita. Tumesifu kipa wetu, Zuberi Foba. Anaweza kuwa kipa wa pili nyuma ya Yakoub Suleiman ambaye ameumia, lakini kama tungekwenda na Aishi Manula basi Foba angeweza hata kuwa kipa wa tatu. Ni michuano mikubwa kwake, lakini ameonyesha ukomavu.
Aliyumba kidogo katika pambano la kwanza wakati alipozungukwa na Victor Osimhen mara mbili kwa sababu ya kutoka langoni bila ya kuwa na uhakika na anakokwenda. Hata hivyo, kuanzia hapo amekuwa hodari wa kuokoa michomo.
Michuano hii imesababisha apate mashabiki wengi nje wa klabu yake ya Azam. Ni hazina kwa taifa na ni jambo zuri tumeongeza kipa mwingine katika suala la uzoefu hasa kwa kipindi hiki ambacho tuna uhaba mkubwa wa makipa.
Jambo la nane. Tunaweza kusonga mbele kama tukiamua. Niliwahi kuandika hapa kwamba tulihitaji kiburi kucheza na Nigeria. Ni kweli tulionyesha kiburi kikubwa. Basi tu tulijisahau na kuruhusu mapema bao la pili dakika chache baada ya Charles M’Mombwa kufunga bao letu la kusawazisha.
Tunahitaji kiburi hiki kwa mara nyingine katika pambano dhidi ya Tunisia. Ni pambano letu la mwisho la makundi. Tunahitaji ushindi na inawezekana. Nadhani Nigeria ni wakali kuliko Tunisia. Kwanini tusife na Tunisia?
Nigeria ana pointi sita. Tunisia ana pointi nne. Sisi na Uganda tuna pointi moja. Sioni Uganda akiambulia lolote kwa Nigeria. Kama sisi tukipata ushindi tu inamaanisha kwamba tunakwenda zetu na Nigeria. Ni kazi chafu, lakini lazima mwanadamu aifanye.
Tunisia wanafungika ingawa tatizo kubwa na wao wanafunga. Hadi sasa katika michuano hii wamesharuhusu mabao manne wakati sisi tumeruhusu mabao matatu. Tatizo ni kwamba na wao wanajua sana kufunga.
Jambo la kumi. ‘Tunammiss’ Clement Mzize. Aibu iliyoje. Ilipaswa kuwa michuano yake hii, lakini majeraha yamekatili nafasi yake. Labda atakuwa fiti katika michuano ya 2027, lakini tulimuhitaji sana katika michuano hii.
Wakati huu kina Samatta na Msuva wakiwa wanaenda chini, hii ilikuwa ni nafasi adimu ya Mzize kujitangaza kwa mawakala wazungu ambao wametua Morocco. Mzize angesumbua zaidi kwa sababu kwa sasa nguvu zake zipo juu zaidi.