Majina ya utani yalitawala redioni na kuhamia mchangani
Muktasari:
- Wakati mwingine, jina la utani la mchezaji limekuwa sehemu muhimu ya urithi wa soka, likimfanya shabiki kumtambua zaidi kwa jina hilo kuliko hata jina lake halisi.
KATIKA historia ya soka la Tanzania, si mabao, ushindi na vikombe pekee vilivyoacha kumbukumbu kubwa kwa mashabiki.
Wakati mwingine, jina la utani la mchezaji limekuwa sehemu muhimu ya urithi wa soka, likimfanya shabiki kumtambua zaidi kwa jina hilo kuliko hata jina lake halisi.
Enzi ambazo redio ilikuwa mfalme wa burudani ya michezo, watangazaji walikuwa na jukumu kubwa la kuyapa uhai majina hayo.
Kwa sauti zao zenye msisimko, walipolitaja jina kama “Popat”, “Tostao”, “Sungura”, “Homa ya Jiji” au “Fundi”, si tu walikuwa wakimtambulisha mchezaji, bali walikuwa wakijenga taswira yake ndani ya fikra za wasikilizaji.
Celestine Mbunga “Sikinde” ni mmoja wa mawinga wa kushoto alipata umaarufu mkubwa akichezea klabu ya Majimaji FC ya Songea, mkoani Ruvuma, baadaye alisajiliwa na Yanga.
Akiwa Yanga, alitengeneza pacha hatari sana na winga mwingine mahiri, Abubakary Salum “Sure Boy” (Mzee wa Vimto).
“Sikinde” ni jina lake la utani lililotokana na miondoko maarufu ya muziki wa dansi wa bendi ya Mlimani Park Orchestra (“Wana Sikinde Ngoma ya Ukae”), ikiwa ni ishara ya jinsi uchezaji wake uivyokuwa na madoido na ladha kama muziki.
Makumbi Juma “Homa ya Jiji” naye alikuwa na jina lenye picha nzito homa inayolivamia jiji akitokea timu ya Pamba Kigoma. Alipewa jina la Homa ya Jiji na mtangazaji wa Redio Tanzania wakati huo Charles Hilary (kwa sasa ni marehemu).
Mohamed Yahaya “Tostao.” Alipachikwa jina la utani “Tostao” akifananishwa na nyota mkubwa wa zamani wa Brazil na washindi wa Kombe la Dunia 1970, Eduardo Gonçalves de Andrade aliyefahamika kama Tostão.
Abbas Dilunga, aliyejulikana zaidi kwa jina la utani “Sungura,” alikuwa winga hatari wa Simba wakati wa miaka ya 1970.
Jina la utani “Sungura” lilitokana na uwezo wake mkubwa wa kukimbia kwa kasi ya ajabu akiwa pembeni na jinsi alivyokuwa mwepesi kuwatoka mabeki wa timu pinzani.
John Makelele “Zig Zag” mmoja kati ya washambuliaji wa Simba. Mwaka 1988 aliinusuru Simba kushuka daraja baada ya kupachika bao la pili lililoikosesha Yanga ubingwa.
Jina la Zig Zag inasemekana alilipata kutoka kwa mtangazaji maarufu Charles Hillary kutokana na aina yake ya uchezaji mpira.
Boi Iddi, anayejulikana zaidi kwa jina la utani “Wickens” (au Boi Wickens), ni mchezaji gwiji wa soka nchini aliyetamba sana miaka ya 1960 na mapema miaka ya 1970.
Chimbuko la jina la utani “Wickens” lilitokana na utamaduni wa Dar es Salaam katika miaka ya 1960, kwa vijana na wachezaji wa mpira wa miguu jijini kupewa au kujipachika majina ya utani.
Pia, Kitwana Manara “Popat” naye ni jina lililogeuka kuwa utambulisho wa kipekee wa mmoja wa mastaa waliotikisa soka la Tanzania.
Wengine ni Mohamed Kajole “Machela”, Rashid Iddi “Chama”, Athuman Iddi Chama “Jogoo”, Edgar Mwafongo “Fongo” na Juma Pondamali “Mensah” nao walikuwa sehemu ya kizazi ambacho majina ya utani yalikuwa kama chapa ya mchezaji.
“Jogoo”, kwa mfano, ni jina lenye taswira ya kujiamini, ujasiri na kujitokeza mbele, wakati “Fongo” na “Mensah” yalitoa utambulisho uliowafanya wachezaji hao kutambulika kwa urahisi.
Salum Kabunda “Ninja” naye alikuwa na jina lililobeba taswira ya ujanja, wepesi na uwezo wa kujipenyeza bila kutabirika awapo mchezoni.
Maulid Dilunga alipewa jina la “Mexico” ambalo ni miongoni mwa majina yaliyoongeza ladha ya kimataifa kwenye utambulisho wa wachezaji.
Kizazi kingine kilikuja na majina yaliyokuwa na mvuto wa aina yake. Mfano, Michael Paul “Nylon”, Said Sued “Scud”, Frank Kassanga “Bwalya”, Malota Soma “Ball Juggler”, Mohamed Hussein “Mmachinga” na Madaraka Selemani “Mzee wa Kiminyio” walifanya orodha hiyo kuwa tajiri zaidi.
Wengine ni Iddi Selemani “Nyigu”, Athuman China “Dynamo”, Fumo Felician “Mwalimu”, Juma Bakari “Kidishi”, Jimmy Mored “Moro”, Abubakar Salum “Sure Boy”, Said Mwamba “Kizota”, Hamis Gaga “Gagarino” na Hussein Marsha “Smart Boy” waliendeleza utamaduni huo.
“Nyigu” lilikuwa jina lenye taswira ya mtu anayechoma au kusumbua mpinzani; “Dynamo” likibeba picha ya nguvu na nishati; “Mwalimu” likitoa wazo la mchezaji mwenye maarifa na uwezo wa kuongoza wengine; huku “Sure Boy” na “Smart Boy” yakibeba taswira ya kujiamini na akili ya mchezo.
Pia, kulikuwa na Methord Mogella “Fundi” jina ambalo liliakisi taaluma kwa maana ya uchezaji wake.
Sanifu Lazaro “Tingisha” naye alikuwa na jina lililoweza kuleta msisimko hata kabla ya mpira kuchezwa. Godwin Aswile “Scania” alibeba jina la gari kubwa, likitoa picha ya nguvu na uimara.
Twaha Hamidu “Noriega”, Fred Felix “Minziro”, Jobe Ayoub “Kwasa”, Said Mrisho “Zicco”, Sunday Manara “Computer”, Abeid Mziba “Tekero”, Zamoyoni Mogella “Golden Boy/DHL”, Razak Yusuph “Carecca”, Thomas Kipese “Uncle Thom” na Kelvin Yondan “Vidic” nao waliingia katika historia ya majina yaliyofanya soka liwe na lugha yake.
“Computer” hasa lilikuwa jina lililovutia kwa sababu lilihusishwa na akili, usahihi na uwezo wa kufanya maamuzi uwanjani, wakati “Golden Boy” lilitoa taswira ya kijana mwenye thamani na kipaji. “DHL” nalo liliweza kuleta picha ya kasi na ufanisi wa kufikisha kitu kinapohitajika.
Kelvin Yondan “Vidic” alibeba jina lililomfanya shabiki amhusishe na beki maarufu wa soka la Ulaya, likisisitiza taswira ya ulinzi na nguvu.
Lakini nguvu kubwa ya majina haya ilikuwa redioni. Mtangazaji aliposema, “Fundi anaingia eneo la hatari!”, “Sungura anakimbia na mpira!” au “Computer anapanga shambulizi!”, jina hilo lilifanya tukio liwe hai zaidi.
Watangazaji walikuwa na kipaji cha kuyatamka kwa msisitizo na kuyafanya kuwa sehemu ya burudani ya mchezo.