Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mahadhi: Yanga walimleta mama uwanja wa ndege

TANZANIA imebarikiwa kuwa na wachezaji wengi mahiri na kila mgeni aliyewahi kufika hapa nchini, amekuwa akisema Tanzania ina wachezaji wengi bora.
Baadhi ya watu maarufu katika soka duniani kutoka mataifa mbalimbali waliwahi kufanya mahojiano kuhusu wachezaji wa Tanzania.
Mbrazili Ricardo Kaka, Yaya Toure akiwa na Ivory Coast, pia makocha kama Dunga wa Brazil na wengine wengi walizungumzia vipaji vilivyopo nchini.
Kila mmoja alisema Tanzania imebarikiwa wachezaji wengi mahiri, ina vijana bora, lakini baadaye manguli hao walisema kama wataendelezwa Tanzania itaweza kufanya vizuri zaidi.
Hapa kuna mchezaji wa zamani wa Yanga, Waziri Mahadhi ‘Mendieta' ni mmoja kati ya wachezaji ambao ukikutana na watu walioufahamu mpira wa Tanzania watakuambia alikuwa kiungo mahiri.
Wengi wanajiuliza yuko wapi sasa? Kwa nini aliacha soka mapema?
Mwanaspoti limefanikiwa kukutana na kiungo huyo mahiri wa zamani wa Yanga ambaye anazungumza mambo mengi kuhusu maisha yake ya soka.
“Wakati nacheza soka ni kama walivyo wachezaji wengine wengi wa Tanzania, sikuwa naamini kama nitakuwa mchezaji mahiri nchini, niliojiona ni mchezaji wa kawaida ambaye naweza kucheza nikimaliza naenda nyumbani kupumzika,” alianza kusema Mahadhi.
“Niliamini kuhusu kufanya mazoezi kuliko kuamini soka ni ajira,” anasema kiungo huyo aliyekuwa na umbo kubwa uwanjani.
Mendieta ambaye hadi leo ukitazama unamwona ni mtu wa mazoezi ya kutosha, anasema alitumia muda mwingi kwenye timu ndogo kabla ya kufika Yanga na haikuwa kazi rahisi hata kidogo.
Mandieta anasema ni vigumu kwa mwanasoka kufanikiwa hapa nchini, hasa sasa uwekezaji ndiyo ukiwa umepamba moto.
“Nilicheza timu nyingi,  nakumbuka mwaka 1996 ndiyo nilianza kuitumikia timu ya Vijana ya Ilala, nikiwa na wachezaji mahiri kwa miaka kadhaa iliyopita kama Omary Matuta pamoja na Said Sued ‘Panuchi’.
“Wakati nacheza Ilala mdogo wangu alikuwa anaichezea Ashanti (nayo ya Ilala), nilikaa kwenye kikosi cha vijana kwa miaka miwili tu nikapandishwa kwenda kikosi cha wakubwa na nilikutana na wachezaji wengine mastaa kama Omary Tamba na Said Sued ‘Kusi’ ambao walikuwa wanachipukia kwa kasi kubwa kwenye soka la Tanzania.”
Mendieta ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho, anasema baada ya kutumika kwenye timu hiyo kwa mwaka mmoja tu aliondoka na kwenda kujiunga na timu ya nyumbani kwao, Shangwe FC.
“Kila mmoja alinishangaa kwa sababu nilikuwa timu kubwa lakini nikaamua kwenda Shangwe ambayo ilikuwa haina jina kubwa kama Vijana, lakini nilifanya hivyo kwa kuwa kipindi kile ni tofauti na sasa ilikuwa jambo la heshima kucheza kwenye timu ya nyumbani kwako.
“Shangwe ilikuwa timu ya jirani kabisa na nyumbani kwetu nilipozaliwa na nilikaa hapo mwaka mmoja na kuondoka, nikajiunga na Cargo ambayo ilikuwa chini ya Kocha Kenny Mwaisabula na baadaye nikajiunga na Coastal Union na hapa ndiyo maisha ya soka yalipoanzia,” anasema kiungo huyo ambaye kwa sasa ni meneja wa Geita Gold.
“Wakati nikiwa Cargo kuna siku kocha mmoja mkubwa hapa nchini, aliniambia sitakiwi kuwa Cargo ambayo wakati huo ilikuwa daraja la kwanza(sasa Championship), kwa kuwa nina uwezo wa kucheza timu yoyote ya Ligi Kuu Bara.
“Aliniambia jambo pekee ambalo natakiwa kulifanya ni kuongeza juhudi ya mazoezi na kusikiliza kila ambacho nafundishwa na baada ya hapo nitaona matunda ya soka ninalocheza.
“Kipindi cha nyuma pamoja na timu nyingine nyingi kuonekana kuwa mahiri, lakini Coastal Union ilikuwa na heshima kubwa sana kwenye soka, walikuwa na kikosi imara na ni kati ya timu zilizokuwa zinatajwa zina mashabiki wengi ukiziondoa Simba na Yanga.
“Siku moja nikiwa nyumbani nilipigiwa simu, nikaambiwa natakiwa kwenda Tanga kujiunga na Coastal Union kwenye timu ya vijana, kwanza sikuamini kwa kuwa hii ilikuwa timu kubwa na sikuwa nafikiri kama kuna siku nitaitumikia timu kubwa kama hiyo.
“Nilikwenda Tanga na kujiunga na timu hiyo, nilionyesha uwezo mkubwa sana kwenye kiungo na wakati huo timu ilikuwa chini ya Kocha Mansour Magram ambaye alikuwa na heshima kubwa kwenye soka la Tanzania na amewahi pia kuzifundisha Sigara na Simba.
“Nikiwa timu ya vijana, nilionyesha kiwango kizuri, wakati huo soka la vijana siyo kama leo, kile kipindi kila mmoja alikuwa anaamini huku ndiyo sehemu ya kuanzia ili uwe mchezaji mahiri, basi lazima uwe bora kwenye timu za vijana na baada ya hapo utapanda kwenda kikosi cha kwanza.



Mendieta ambaye alikuwa anafananishwa na kiungo wa zamani wa Hispania, Gaizika Mendieta, anasema baada ya kucheza kwenye timu ya vijana kwa mwaka mmoja tu alionyesha makeke yake kwenye ukabaji pamoja na kwamba wachezaji wengine waliamini hawezi kufanya vizuri kutoka na umbile lake.
“Nilikuwa bonge lakini anayejua sana, nilikuwa nikipewa nafasi nafanya kazi yangu kama inavyotakiwa na sisemi bali mashabiki walikuwa wanazungumza mara nyingi walikuwa wanasema ‘yule bonge anajua sana.’
“Ndani ya mwaka huo kwenye kikosi cha vijana cha Coastal niliitwa kwenye Timu ya Taifa ya Vijana (U20) Ngorongoro Heroes muda mchache baada ya kupandishwa.
“Nakumbuka nilipata nafasi ya kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha Coastal na kocha  alikuwa Nzoyisaba Tauzany, aliniita siku moja kabla ya mchezo dhidi ya Yanga na kuniambia anataka kunipa kazi maalumu.
“Yanga walikuwa na mshambuliaji hatari sana wakati huo anaitwa Idd Moshi na kocha aliniambia nifanye mambo yote lakini Moshi asifunge bao, kweli nakumbuka hiyo mechi tulipoteza 2-0, lakini Moshi hakufunga na alishindwa kumaliza mchezo ule, nilipotoka mashabiki walinishangilia sana kutokana na kazi kubwa niliyokuwa nimeifanya ya kumzuia staa huyo.”


 NDEGE YA KWANZA
“Kwanza wengi wanatakiwa kufahamu nilipoitwa kwenye timu ya vijana kwenye mashindano ya kufuzu Kombe la Mataifa Afrika, tulitakiwa kusafiri kwenda kuvaana na Namibia.
“Hii ilikuwawa safari yangu ya kwanza na ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kupanda ndege, nilikuwa pamoja na ndugu yangu kwenye timu hii anaitwa Habib Mahadhi na wote tulikuwa na nafasi kwenye kikosi cha kwanza.”
Mahadhi anasema baada ya kuitwa kwenye timu hiyo alianza kuonja utamu wa soka kwani alipewa posho na kuona mpira unalipa, pia ndoto yake ya kucheza Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ilianza kutimia.


YANGA WAMFUATA NAMIBIA
“Nikiwa hapa nchini wakati tunafanya mazoezi na Timu ya Taifa ya Vijana, kuna siku alinifuata kaka yangu mmoja na kuniambia maisha yangu yatabadilika siku siyo nyingi kwani kuna taarifa Yanga inanitaka na amewasikia baadhi ya wanachama wakisema.”
“Sikuamiani, nilikuwa najiuliza Yanga wameniona wapi? Wakati sikuwa nimecheza kwa kiwango kikubwa, niliamini nilitakiwa kucheza Coastal kwenye kikosi cha kwanza ndiyo nipate nafasi ya kusajiliwa kwenye timu nyingine lakini kwangu mambo yalikuwa tofauti.
“Tulipoondoka kwenda Namibia na timu ya vijana, nilielezwa kuna viongozi wa Yanga walikuwa wamesafiri kwa ajili ya kuwatazama wachezaji, lakini mmoja wapo nilikuwa mimi.
“Nakumbuka ule mchezo nilicheza kwa dakika zote 90 na nilifanya kazi kubwa kwenye eneo la kiungo baada ya mechi kumalizika wachezaji wenzangu waliniambia nimekichafua, sikufurahi sana kwa kuwa niliona kama nimeongeza deni kwenye maisha yangu ya soka."


YANGA YAMTUMIA MAMA YAKE
Mendieta anasema wakati ule jambo hili halikuwa limesambaa kama sasa, hivyo hakuwasiliana na mtu yeyote wakati anarejea nchini, lakini akiwa Uwanja wa Ndege aliwaona viongozi wa Simba aliokuwa anawafahamu wakawa wanamuita.
Wakati akiwafuata mama yake alimfuata kwa kasi na kumshika mkono akampeleka kwa viongozi wa Yanga waliokuwa upande mwingine.
“Kwanza sikufahamu imekuwaje mama amefika uwanja wa ndege, lakini nilijikuta nimepanda naye gari moja na viongozi wa Yanga ambao walikuwa wanacheka na kuwakebehi wale wa Simba kuona kuwa wameishinda vita.


KISA NI BABA YAKE
“Unajua hapa kuna mambo mawili, baba yangu Omary Mahadhi Bin Jabir alikuwa mmoja kati ya makipa bora zaidi wa soka kuwahi kutokea hapa nchini.
“Baba aliitumikia Simba, hivyo viongozi wao waliamini nami nitakuwa Simba, lakini haikuwa hivyo, Yanga waliwahi nyumbani na kumshawishi mama wakaja naye uwanja wa ndege ilikuwa ngumu kumgomea.”


MKATABA MNONO ENZI HIZO
Mendieta anasema wakati ule Yanga ilikuwa chini ya Tarimba Abass na Abdul Sauko, viongozi waliokuwa na ushawishi mkubwa kwenye soka la Tanzania na waliaminika ni mamafia kwenye masuala ya usajili.
“Tulifika kwenye ofisi moja mjini nilipewa mkataba mbele ya mama yangu.
“Kwanza nilishangaa, nilisaini mkataba ule na kupewa Sh1.5 milioni hapo hapo. Nakumbuka mshahara wangu ulikuwa Sh70,000 kwa mwezi mwaka 2000 zilikuwa fedha nyingi sana.
“Sikulala, kwa kuwa nilikuwa sijawahi kushika fedha nyingi kiasi hicho, mama akaniambia natakiwa kupambana kama nataka kupata fedha nyingi zaidi.”


YANGA YA MASTAA
“Siku mbili baadaye nilienda mazoezini Yanga, hali ilikuwa tofauti, timu ilikuwa na mastaa wengi wakati ule, walikuwepo kina Ediblily Lunyamila, Mohammed Hussein, Peter Manyika, Ally Mayay na wengine wengi.
“Mazoezi yao yalikuwa ya mastaa hasa, ukienda mazoezini unakutana na watu kweli kweli ukiwa legelege huchezi hata mazoezi tu.


AMKUTA MWAMBA WA JANGWANI
 Mahadhi anasema pamoja na kutamba na kuwa mwamba kwenye timu zote alipopita, akiwa Yanga hakuwa na ubabe wowote kwani alimkuta kiungo mahiri kwenye timu hiyo, Shabani Ramadhani.
“Siyo tu watu walikuwa wanaamini Shabani anajua mimi mwenyewe nilikuwa najua kabisa siwezi kumweka benchi kwenye kikosi cha Yanga kwani alishaweka mizizi yake kwenye timu na alikuwa anajua sana soka.
“Huwezi kuamini nilikaa nje Yanga hadi alipoondoka kwenda Mauritius ndipo nikapata nafasi kwenye timu na mechi yangu ya kwanza ilikuwa dhidi ya Mtibwa Sugar baada ya hapo nilicheza mechi nyingine mfululizo.”


STARS, AUMIA FAINALI
Mahadhi anasema baada ya kupata nafasi Yanga alicheza kikosi cha kwanza kwa miaka minne na kuitwa Taifa Stars na kwenda kwenye michuano ya Castle yaliyokuwa yanafanyika Mwanza na timu ilifika fainali dhidi ya Kenya.
“Nakumbuka tulitwaa ubingwa wa Castle baada ya kuifunga Kenya kama sikosei tulishinda mabao 3-0, mabao yalifungwa na Salvatory Edward na Emmanuel Gabriel na dakika za mwisho niliumia na nafasi yangu aliingia Selemani Matola.”


SAFARI YA UMANGANI
“Kipindi kile kulikuwa na ligi fupifupi Uarabuni, niliondoka mwaka 2003 na kwenda huko, nilicheza mwaka mmoja.
Mwaka 2004 nilirudi tena Yanga wakaniambia bado walikuwa wakinihitaji, nikajiunga nao tena, nilicheza mwaka mmoja nikajiunga na Moro United.
“Unajua leo ukiwaambia watu wengi watashindwa kukuelewa, lakini wakati najiunga na Moro nilikiwa pamoja na Pitchu Congo, Salum Sued na Patrick Katalay ilikuwa inamilikiwa na watu wawili, mmoja aliitwa Seif Magari ambaye alikuwa Yanga na Kassim Dewji aliyekuwa kigogo wa Simba.
Baada ya mwaka mmoja nilirudi tena Yanga, yaani walikuwa wakinitaka wananichukua, nikitaka kuondoka naondoka zangu.


MWISHO WA ENZI
Mahadhi anakumbuka alikwenda Moro United na akaanzaa kusumbuliwa na majeraha akaamua kuachanana na soka.


FAMILIA YA SOKA  
Mahadhi anafunguka kwao kila mtoto aliyezaliwa mwanaume alikuwa mchezaji.
“Baba yangu alikuwa kipa Simba, mpwa wangu Rashid Mahadhi alikuwa kipa CDA, Habib Mahadhi alikuwa mdogo wangu aliwahi kuibuka mfungaji bora wa ligi mwaka 1999, Bakary Mahadhi ni mdogo wangu alicheza Ashanti na Manyema.
“Hivyo kwetu sisi ni familia ya soka hasa kila mmoja alikuwa akianza kukua anataka kucheza soka tu.”


GEITA TIMU KUBWA
Mahadhi anasema wengi wanaamini yeye ni kocha msaidizi wa Geita, lakini siyo kweli kwani cheo chake kwenye timu hiyo ni meneja na anaamini timu hiyo ni mahiri sana ipewe muda.
“Unakumbuka Geita iliuza zaidi ya wachezaji wanane na kila mmoja akaamini timu itafanya vibaya, lakini tazama sasa kila kitu kinakwenda vizuri, kwa kuwa Geita ni timu siyo kikundi, mfumo wa timu hii ni bora zaidi.
“Kwa sasa kuna tofauti kubwa sana ya soka kwa kuwa uwekezaji ni mkubwa, kila mmoja anayewekeza kwenye soka atafanikiwa, naona kitu hicho pale Geita, nafikiri baada ya miaka miwili itakuwa timu mahiri zaidi.


KIKOSI CHAKE HAKINA MASTAA
Mendieta anasema anaamini Tanzania ina wachezaji wengi mahiri, lakini akielezwa apange kikosi chake cha kwanza cha miaka yote, basi atapanga hivi:
Kipa, Mengi Matunda, mabeki Mecky Maxime, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Salum Sued,  Kelvin Yondani, viungo Shaban Kisiga, Salvatory Edward, Danny Lyanga na Edibily Lunyamila na mshambuliaji George Mpole.