Mabilionea timu wanazo, hela wanazo
Muktasari:
- Miongoni mwa matajiri zaidi duniani, wachache walikuwa na mwaka bora kama Rob Walton. Mrithi huyo wa biashara za supermaket za Walmart mwenye umri wa miaka 80, mwaka huu ameshuhudia utajiri wake ukipanda kwa Dola 32.6 bilioni kufikia thamani ya takriban Dola 110 bilioni. Hii ni kutokana na mafanikio makubwa ya kampuni hiyo iliyoanzishwa na baba yake zaidi ya miongo sita iliyopita.
WASHINGTON, MAREKANI: STEVE Ballmer wa Los Angeles Clippers kwa mara nyingine tena anaongoza orodha ya mabilionea 25 wanaomiliki timu za michezo mbalimbali duniani wakiwa na jumla ya ukwasi wa thamani ya Dola 607 bilioni akimuacha nyuma kidogo Rob Walton wa Broncos, lakini wote wapo hatarini kupitwa ifikapo mwakani.
Miongoni mwa matajiri zaidi duniani, wachache walikuwa na mwaka bora kama Rob Walton. Mrithi huyo wa biashara za supermaket za Walmart mwenye umri wa miaka 80, mwaka huu ameshuhudia utajiri wake ukipanda kwa Dola 32.6 bilioni kufikia thamani ya takriban Dola 110 bilioni. Hii ni kutokana na mafanikio makubwa ya kampuni hiyo iliyoanzishwa na baba yake zaidi ya miongo sita iliyopita.
Lakini, kwa Walton aliyeinunua timu ya Denver Broncos 2022 kwa rekodi ya Dola 4.65 bilioni ongezeko hilo kubwa la utajiri halikumfanya awe mmiliki tajiri zaidi wa timu za michezo duniani, kwani nafasi ya bilionea zaidi mmiliki wa timu bado inashikwa na Ballmer.
Bilionea huyo mmiliki wa Los Angeles Clippers na mtu wa 10 tajiri zaidi duniani ana utajiri unaokadiriwa kuwa Dola 118 bilioni yaani zaidi ya Walton kwa Dola 8 bilioni.
Bernard Arnault, mmiliki wa himaya ya bidhaa za kifahari za LVMH na mtu wa tano tajiri zaidi dunianikwa Dola 178 bilioni alinunua klabu ya mpira wa miguu ya Ufaransa, Paris FC 2024. Timu hiyo ilipanda Ligi Kuu Ufaransa (Ligue 1) msimu huu. Mwaka huu, Forbes imepanua mbinu ya kuorodhesha wamiliki wa timu za michezo ikijumuisha ligi nyingi zaidi za daraja la kwanza Ulaya na kutanua orodha kutoka wamiliki 20 mwaka 2023 na 2024 hadi 25. Mabadiliko hayo yaliwaruhusu wamiliki wapya watatu kuingia kwenye orodha wakiwamo Muisrael Idan Ofer mwenye Dola 22.5 bilioni anayeimiliki FC Famalicao ya Ureno.
Mwingine ni Mdenmark Anders Holch Povlsen anayemili FC Midtjylland mwenye Dola 12.8 bilioni, mmiliki mwenza wa Aston Villa na Mmisri Nassef Sawiris mwenye Dola 9.6 bilioni.
Kwa pamoja, wamiliki 25 tajiri zaidi wa timu za michezo duniani wana ukwasi wa Dola 607 bilioni, huku 20 wa juu wakichangia Dola 557 bilioni katika jumla hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 16 ukilinganisha mwaka 2024. Karibu kila mmiliki ameshuhudia utajiri wake ukipanda kutokana na soko imara la hisa, huku Robert Pera, mmiliki wa timu ya kikapu ya NBA ya Memphis Grizzlies na mkurugenzi mtendaji wa Ubiquiti Networks akiongoza kwa ongezeko la asilimia 145.
Wamiliki watatu kati ya 25 yaani Ballmer, Francois Pinault wa Stade Rennais ya Ufaransa na Mat Ishbia wa Phoenix Suns ya Marekani walishuhudia mali zao zikishuka thamani. Kwa mwaka wa pili mfululizo, mpira wa kikapu unatawala orodha hii ukiwa na timu 13 (11 kutoka NBA na mbili WNBA), ilhali soka timu 12 (sita kutoka Ulaya, nne za MLS na mbili Ligi Kuu ya Wanawake England zikifuatiwa na soka la Kimarekani (NFL nane) na NHL ziko nne. Steve Cohen ndiye mmiliki pekee wa timu ya MLB aliyejumuishwa kwenye orodha.Hii hapa orodha ya wamiliki 25 tajiri zaidi 2025 wa timu duniani:
1. Steve Ballmer
Utajiri: Dola 118 bilioni
Timu: Los Angeles Clippers
Chanzo cha utajiri: Microsoft
Uraia: Marekani
Ballmer kwa muda mrefu alitaka kuhamishia Clippers kwenye uwanja binafsi badala ya kushirikiana na Los Angeles Lakers na Sacramento Kings. Ndoto yake ilitimia mwaka jana baada ya kufunguliwa Intuit Dome huko Inglewood.
Uwanja huo wa teknolojia ya kisasa umekuwa ukifanya kazi kwa kuandaa zaidi ya matukio 100 (ikiwemo matamasha na michezo ya kikapu) na kuvutia mashabiki zaidi ya milioni moja.
2. Rob Walton & familia
Utajiri: Dola 110 bilioni
Timu: Denver Broncos
Chanzo cha Utajiri: Walmart
Uraia: Marekani
Walton alilipa bei ya rekodi kuingia NFL 2022, lakini uwekezaji wake tayari unaonyesha faida. Forbes inakadiria Broncos ambapo mmiliki rasmi wa udhibiti ni mkwewe, Greg Penner kwa sasa inathaminiwa kwa Dola 5.5 bilioni ikiwa ni ongezeko la asilimia 18 tangu alipoinunua.
Lakini ongezeko hilo bado ni dogo ukilinganisha na kupanda kwa hisa za Walmart ambazo zimeongezeka zaidi ya mara mbili katika kipindi hicho.
3. Miriam Adelson & familia
Utajiri: Dola 32.1 bilioni
Timu: Dallas Mavericks
Chanzo cha utajiri: Kasino
Uraia: Marekani
Adelson mwenye umri wa miaka 79 ni mjane wa aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Las Vegas Sands, Sheldon Adelson aliyefariki 2021, aliyeinunua Mavericks Desemba 2023.
Lakini mwanzo wake kama mmiliki ulikumbwa na changamoto pale alipoidhinisha uhamisho wa nyota Luka Doncic kwenda Los Angeles Lakers mwaka huu. Baada ya mwaka uliopita kufika fainali za NBA, mwaka huu Dallas haikufuzu hata mchujo (playoffs).
Pamoja na hayo, timu ilitangaza bei za juu zaidi za tiketi za msimu ujao jambo lililoongeza msuguano na mashabiki.
4. Daniel Gilbert
Utajiri: Dola 27.8 bilioni
Timu: Cleveland Cavaliers
Chanzo cha utajiri: Mikopo ya nyumba
Uraia: Marekani
Kampuni ya Gilbert, Rocket Companies ilipitia misukosuko mwaka uliopita. Hisa zilipanda zaidi ya Dola 20 Septemba, zikashuka chini ya Dola 11 Januari. Baadaye zilipanda tena na kufunga kwa Dola 15.77 Machi 7, siku ambayo Forbes ilirekodi thamani ya mabilionea 2025. Gilbert mwenye miaka 63 ameshuhudia pia Cavaliers ikipanda thamani hadi kufikia Dola 3.95 bilioni.
5. Idan Ofer
Utajiri: Dola 22.5 bilioni
Timu: FC Famalicao (Ureno)
Chanzo cha utajiri: Usafirishaji
Uraia: Israel
Ofer, mtoto wa pili wa tajiri wa usafirishaji hayati Sammy Ofer aliyefariki 2011, alipata udhibiti mkubwa wa Famalicao 2018, mwaka mmoja baada ya kununua hisa ndogo Atletico Madrid ya Hispania. Famalicao ilipanda daraja hadi Ligi Kuu Ureno 2019 na imebaki hapo tangu wakati huo, ingawa bado haijawahi kumaliza ligi katika nafasi za juu kuliko ya sita.
6. François Pinault & familia
Utajiri: Dola 21.7 bilioni
Timu: Stade Rennais
Chanzo cha utajiri: Bidhaa za kifahari
Uraia: Ufaransa
Katika miaka 27 ambayo Pinault (mwenyekiti wa heshima wa kundi la bidhaa za kifahari Kering), amemiliki Stade Rennais, timu hiyo haijawahi kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Ufaransa. Mwaka huu pia hali huenda haitabadilika.
7 Steve Cohen
Utajiri: Dola 21.3 bilioni
Timu: New York Mets
Chanzo cha utajiri: Hedge Funds
Uraia: Marekani
Cohen mwenye miaka 68 ni mwanzilishi wa Point72 Asset Management, aliyekumbusha ulimwengu wa mpira wa mangongo kwamba hana hofu ya kutumia fedha.
Majira ya baridi alimsaini supastaa Juan Soto kwa mkataba wa miaka 15 wenye thamani ya Dola 765 milioni. Nje ya uwanja, mipango yake ya kujenga kasino huko Queens ilipiga hatua Februari baada ya City Planning Commission kuidhinisha mabadiliko muhimu ya sheria za upangaji wa ardhi.
7 David Tepper
Utajiri: Dola 21.3 bilioni
Timu: Carolina Panthers na Charlotte FC
Chanzo cha utajiri: Hedge funds
Uraia: Marekani
Tangu Tepper (miaka 67), ni mwanzilishi wa Appaloosa Management aliyeinunua timu ya soka la Kimarekani, Panthers 2018 kwa Dola 2.275 bilioni. Timu hiyo haijawahi kufuzu mchujo wa NFL.
Malalamiko hayaji tu kutoka kwa mashabiki kwani katika uchambuzi wa hivi karibuni wa wachezaji wa NFL (NFLPA survey), Tepper alipata alama ya D, ikiwa ni ya pili mbaya zaidi miongoni mwa wamiliki 32. Lakini katika kandanda anakomilikia timu inayoshirikia Ligi Kuu Marekani (MLS), Charlotte FC imefanya vyema zaidi.
Timu hiyo imetinga hatua ya mtoano kwa miaka miwili mfululizo na imekuwa ya pili kwa mahudhurio ya mashabiki wa msimu wa kawaida 2022, 2023 na 2024 (kwa mujibu wa Transfermarkt).
9. Henry Samueli
Utajiri: Dola 19.7 bilioni
Timu: Anaheim Ducks
Chanzo cha utajiri: Semiconductors
Uraia: Marekani
Mabadiliko makubwa aliyoyafanya Samueli, 70, mwanzilishi mwenza wa Broadcom kwenye timu ya Anaheim Ducks yamefanya wengine waanze kujiuliza iwapo anaweza pia kuokoa timu nyingine ya Orange County na Los Angeles Angels ambayo mmiliki wake Arturo Moreno aliwahi kuiweka sokoni kwa muda mfupi 2022. Kwa uwezo wake kifedha, Samueli anaweza.
Kampuni yake ya teknolojia ya chip ilifanya vizuri mwaka huu ikipandisha utajiri wake kwa karibu asilimia 40 na kuambulia faida mara sita miongoni mwa wamiliki 25 wa klabu duniani.
10. Stephen Ross
Utajiri: Dola 18.4 bilioni
Timu: Miami Dolphins
Chanzo cha utajiri: Mali isiyohamishika
Uraia: Marekani
Baada ya wamiliki wa Ligi ya Soka la Kimarekani (NFL) kupiga kura Agosti kuruhusu wawekezaji wa taasisi kununua hisa kwenye timu, Ross alikuwa wa kwanza kutumia fursa hiyo. Desemba, mwanzilishi wa Related Companies mwenye miaka 84, aliuza asilimia 10 ya Dolphins (pamoja na Uwanja wa Hard Rock na mashindano ya Formula 1 Miami Grand Prix) kwa Ares Management, kwa thamani ya Dola 8.1 bilioni. Forbes inakadiria thamani ya Dolphins pekee (bila mali nyingine) kuwa na thamani ya Dola 6.2 bilioni hadi mwaka jana.
11. Shahid Khan
Utajiri: Dola 17.3 bilioni
Timu: Jacksonville Jaguars, Fulham na All Elite Wrestling
Chanzo cha utajiri: Vipuri vya magari
Uraia: Marekani
Khan mwenye umri wa miaka 74 ni miongoni mwa wamiliki wachache wa timu kubwa za michezo wenye asili ya nje ya Marekani. Alizaliwa Pakistan na alihamia Marekani akiwa kijana. Jaguars ilifuzu mchujo wa NFL mara mbili katika misimu mitatu iliyopita.
Klabu yake ya England, Fulham imedumu kwenye Ligi Kuu England tangu 2022. Nje ya soka na kandanda, Khan ni mmiliki mwenza wa taasisi inayosimamia mchezo wa mieleka All Elite Wrestling (AEW), mpinzani mkuu wa WWE ambayo sasa ni sehemu ya TKO Group.
12. Arthur Blank
Utajiri: Dola 16.7 bilioni
Timu: Atlanta Falcons na Atlanta United
Chanzo cha utajiri: Home Depot
Uraia: Marekani
Blank, 82, ni mwanzilishi mwenza wa Home Depot akiwa na historia ya muda mrefu ya kusaidia jamii kupitia hisani. Anaendelea kufadhili miradi ya kijamii huko Atlanta wakati timu zake mbili — Falcons (NFL) na Atlanta United (MLS) zinaendelea kukua. Atlanta United ambayo aliianzisha 2014 tayari imeshinda ubingwa wa MLS (2018) na inajulikana kwa kuvutia mashabiki wengi zaidi ya timu nyingine yoyote ya ligi hiyo.
13. Jan Koum
Utajiri: Dola 16.5 bilioni
Timu: Dinamo Kyiv
Chanzo cha utajiri: WhatsApp
Uraia: Marekani
Koum, mwanzilishi mwenza wa WhatsApp (aliyouza kwa Facebook 2014 kwa Dola 19 bilioni), ni mmiliki wa klabu ya nyumbani kwao Ukraine, Dynamo Kyiv. Klabu hiyo ni moja ya timu maarufu zaidi katika historia ya Ukraine ikiwa na mataji zaidi ya 15 ya ligi. Hata hivyo, vita inayoendelea nchini humo imeathiri vibaya klabu na ligi nzima ikiwemo kuhamisha mechi nyingi mbali na mji wa Kyiv.
14. Stanley Kroenke
Utajiri: Dola 16.2 bilioni
Timu: Arsenal, Los Angeles Rams, Denver Nuggets, Colorado Avalanche, Colorado Rapids na Colorado Mammoth
Chanzo cha Utajiri: Mali isiyohamishika, michezo, ndoa na familia ya Walmart
Uraia: Marekani
Kroenke, 78, ana moja ya falme kubwa zaidi za michezo duniani. Timu yake Rams ilishinda Super Bowl 2022, Nuggets NBA na 2023 na Avalanche ikaondoka na Stanley Cup 2022. Timu yake ya kandanda, Arsenal, iko kileleni mwa Ligi Kuu England na hushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya mara kwa mata. Pia anamiliki Uwanja wa Emirates na SoFi, moja ya viwanja vya gharama kubwa zaidi duniani.
15. Robert Kraft
Utajiri: Dola 15.5 bilioni
Timu: New England Patriots na New England Revolution
Chanzo cha utajiri: Uwekezaji, karatasi na ufungashaji
Uraia: Marekani
Kraft mwenye miaka 83 alijizolea sifa kubwa kwa kuiongoza vyema Patriots enzi zake NFL akiwa na Tom Brady na Bill Belichick. Tangu Brady aondoke 2020 timu imekuwa ikiporomoka na ilimaliza msimu uliopita ikiwa na rekodi mbaya zaidi katika enzi ya Belichick. Hata hivyo, Kraft bado ni mmoja wa wamiliki wenye heshima kubwa NFL na anamiliki pia timu ya New England Revolution kwenye MLS.
16. John Henry
Utajiri: Dola 14.3 bilioni
Timu: Boston Red Sox, Liverpool, Pittsburgh Penguins na RFK Racing
Chanzo cha utajiri: Uwekezaji
Uraia: Marekani
Henry (miaka 76), ndiye kiongozi wa Fenway Sports Group (FSG), moja ya kampuni kubwa za michezo duniani. Red Sox ilishinda World Series mara nne tangu ainunue 2002. Liverpool pia imeshinda Ligi ya Mabingwa Ulaya (2019) na Ligi Kuu England (2020). Henry na FSG pia wanamiliki Penguins ya mchezo wa Ligi Kuu ya Mangongo Marekani (NHL) na timu ya mbio za NASCAR na RFK Racing.
17. Mark Cuban
Utajiri: Dola 13.5 bilioni
Timu: Dallas Mavericks (hisa ndogo)
Chanzo cha Utajiri: Teknolojia, uwekezaji
Uraia: Marekani
Cuban ana miaka 67, aliuza sehemu kubwa ya Mavericks kwa familia ya Adelson 2023, lakini alibaki na hisa chache na ushawishi katika uamuzi wa michezo. Alinunua Mavericks 2000 kwa Dola milioni 285 na kuiongoza hadi ubingwa wa NBA 2011. Pamoja na kushuka thamani ya hisa zake, Cuban bado ni mmoja wa wamiliki maarufu na anaendelea kushiriki kwenye miradi ya teknolojia na televisheni akiwa pia kama jaji wa kipindi cha Shark Tank.
18. Larry Tanenbaum
Utajiri: Dola 13.2 bilioni
Timu: Toronto Maple Leafs, Toronto Raptors na Toronto FC
Chanzo cha Utajiri: Ujenzi, uwekezaji
Uraia: Canada
Tanenbaum (miaka 79), ni mwenyekiti wa Maple Leaf Sports & Entertainment (MLSE), kampuni inayomiliki Raptors (NBA), Maple Leafs (NHL) na Toronto FC (MLS). Wakati Raptors ilishinda NBA 2019, Leafs bado inahangaika kuvunja ukame wa zaidi ya nusu karne bila Stanley Cup. Tanenbaum pia ni mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa NBA akiwakilisha maslahi ya wamiliki wa timu zote.
19. Jerry Jones
Utajiri: Dola 13 bilioni
Timu: Dallas Cowboys
Chanzo cha Utajiri: Mafuta na gesi na mali isiyohamishika
Uraia: Marekani
Akiwa na miaka 82 hivi sasa, Jones alinunua Cowboys 1989 kwa Dola 150 milioni na sasa ni mojawapo ya klabu za michezo zenye thamani kubwa zaidi duniani ikikadiriwa zaidi ya Dola 9 bilioni. Cowboys mara nyingi hujulikana kama “America’s Team” na licha ya kutochukua Super Bowl tangu 1995 ina mapato na mashabiki wengi zaidi katika NFL.
20. Ann Walton Kroenke
Utajiri: Dola 12.6 bilioni
Timu: Denver Nuggets, Colorado Avalanche, Colorado Rapids na Colorado Mammoth
Chanzo cha Utajiri: Walmart
Uraia: Marekani
Ann (miaka 76), ni mke wa Stan Kroenke na mrithi wa utajiri wa Walmart. Kupitia ndoa na uwekezaji wa familia ana ushawishi mkubwa katika kampuni ya Kroenke Sports & Entertainment. Hii inajumuisha timu za NBA, NHL, MLS na Lacrosse. Ingawa mumewe ndiye anayejulikana zaidi kama uso wa umiliki, sehemu ya utajiri na timu zipo pia chini ya jina lake.
21. Gayle Benson
Utajiri: Dola bilioni 11.7
Timu: New Orleans Saints na New Orleans Pelicans
Chanzo cha Utajiri: Urithi na uwekezaji
Uraia: Marekani
Gayle, 78, alirithi timu baada ya kifo cha mumewe Tom Benson 2018. Ameahidi kwamba mara baada ya kifo chake Saints (NFL) na Pelicans (NBA) zitauzwa na mapato yote kuelekezwa kwenye misingi ya hisani huko New Orleans. Hadi wakati huu anaendelea kuongoza timu hizo huku akisisitiza juu ya kujenga urithi wa kijamii katika jiji hilo.
23. Micky Arison
Utajiri: Dola 11.5 bilioni
Timu: Miami Heat
Chanzo cha Utajiri: Carnival Cruise Lines
Uraia: Marekani
Arison, 76, amekuwa mmiliki wa Heat tangu 1995. Katika kipindi chake timu imeshinda mataji matatu ya NBA (2006, 2012, 2013). Ingawa haina tena nyota kama LeBron James, Heat imeendelea kubaki kuwa washindani hasa chini ya kocha Erik Spoelstra. Nje ya mpira wa kikapu, Arison ni mwenyekiti wa kampuni kubwa ya meli za kitalii duniani, Carnival Corporation.
24. Tilman Fertitta
Utajiri: Dola bilioni 11.2
Timu: Houston Rockets
Chanzo cha Utajiri: Mikahawa, hoteli na kamari
Uraia: Marekani
Fertitta (miaka 67), alinunua Rockets 2017 kwa Dola 2.2 bilioni. Tangu wakati huo timu hiyo imekuwa katika kipindi cha kujengwa upya ikijaribu kutengeneza kizazi kipya cha nyota baada ya kuondoka kwa James Harden 2021. Fertitta pia anamiliki kasino, hoteli na migahawa mingi kupitia kampuni ya Landry’s Inc.
25. Paul Tudor Jones II
Utajiri: Dola bilioni 11
Timu: Memphis Grizzlies
Chanzo cha utajiri: Hedge Funds
Uraia: Marekani
Jones, 71, ni mfanyabiashara maarufu wa Wall Street na mwanzilishi wa Tudor Investment Corporation. Pia ni mmoja wa wamiliki wenza wa Memphis Grizzlies akijiunga na kundi la wawekezaji waliowekeza kwenye timu hiyo. Licha ya kushikilia hisa chache anabaki kuwa sehemu ya wamiliki tajiri zaidi NBA.