KSI; Tajiri mwenye mishe nyingi za kupiga hela
Muktasari:
- Hata hivyo, mbali na mafanikio hayo, gumzo kubwa lilikuwa ni juu ya kiasi kikubwa cha utajiri ambacho staa huyu amejijengea kupitia YouTube, muziki, ndondi, biashara na matangazo.
LONDON, ENGLAND: MWISHONI mwa wiki iliyopita, jina la KSI lilitikisa tena mitandao baada ya kampuni yake ya vinywaji, PRIME Hydration, kutajwa kama moja ya bidhaa za vinywaji zinazobamba sana Ulaya na Marekani.
Hata hivyo, mbali na mafanikio hayo, gumzo kubwa lilikuwa ni juu ya kiasi kikubwa cha utajiri ambacho staa huyu amejijengea kupitia YouTube, muziki, ndondi, biashara na matangazo.
KSI, jina lake halisi likiwa Olajide Olatunji, alianza safari yake kama mtengenezaji wa video za michezo ya FIFA YouTube, lakini leo hii ni miongoni mwa wasanii na wajasiriamali vijana matajiri zaidi duniani. Je, anapigaje pesa? Msome hapa.
ANAPIGAJE PESA
Kwa sasa, utajiri wa KSI unakadiriwa kufikia zaidi ya Dola 100 hadi 120 milioni, uliotokana na vyanzo mbalimbali.
Kwanza ni kupitia YouTube ambapo ana zaidi ya wafuasi milioni 40 na kwa mwaka alikuwa na uwezo wa kukunja takribani Dola 10 milioni kwa mwaka. Hiyo ni pamoja na matangazo binafsi na yale ya YouTube.
Vilevile jamaa ameshatoa albamu kadhaa zilizofanya vizuri kama Dissimulation na All Over The Place, ambapo nyimbo zake zimepata mamilioni ya wasikilizaji kupitia majukwaa kama Spotify na Apple Music ambako analipwa mkwanja wa maana.
Kupitia mapambano makubwa ya ndondi kama ya Logan Paul, Tommy Fury na wapinzani wengine, KSI amepata pesa nyingi na wastani wa kila pambano alikunja takribani Dola 40 milioni.
Kwa asilimia kubwa utajiri wake pia unachangiwa na kampuni ya vinywaji ya PRIME Hydration ambayo inamilikiwa pia na mwana mtandao mwenzake Logan Paul.
Kwa sasa kampuni hii inakadiriwa kuingiza mauzo ya hadi Dola 3 milioni kwa mwaka ikiwa ni inazidi kuongezeka kila uchao.
Jamaa pia ana kampuni yake ya Misifit Boxing ambayo inafanya kazi ya kuandaa mapambano mbalimbali barani Ulaya.
Vilevile ni balozi wa kampuni mbalimbali kama Adidas, G Fuel, EA Sports. Huku anapata Dola 10 milioni kwa mwaka.
Mwaka 2023, jarida la Forbes lilimtaja kama mmoja wa vijana waliotengeneza fedha nyingi zaidi kupitia mitandao ya kijamii.
MIJENGO
KSI anaishi katika nyumba ya kifahari jijini London yenye thamani ya zaidi ya Dola 10 milioni, yenye:
Gym binafsi, studio ya muziki, sinema ya ndani, bwawa la kuogelea na bustani ya kisasa.
Pia anamiliki mali nyingine England na baadhi ya nchi za Ulaya kwa ajili ya biashara.
NDINGA
Lamborghini Aventador – Dola 450,000
Rolls Royce Wraith – Dola 330,000
Porsche 911 Turbo S – Dola 220,000
BMW i8 – Dola 150,000
Mercedes-Benz G-Wagon – Dola 200,000
Audi R8
Mbali na hayo, anapenda pia pikipiki za bei kubwa.
MSAADA KWA JAMII
Kupitia taasisi na kampeni mbalimbali, KSI amekuwa akichangia, gharama za elimu kwa vijana wasio na uwezo wa kujisomesha, misaada kwa waathirika wa majanga na kusaidia vipaji vya vijana kwenye muziki na michezo mengine.
Mwaka 2022, alichangia zaidi ya Dola 500,000 kusaidia miradi ya vijana barani Afrika na Ulaya.
FAMILIA NA MAISHA BINAFSI
KSI amekuwa akiweka sana maisha yake binafsi mbali na macho ya watu, lakini mwenyewe amethibitisha kuwa yupo katika uhusiano, lakini hataki kumweka hadharani mpenzi wake na inasemekana wapo pamoja kwa mwaka wa nane sasa.
Inaelezwa kuwa, mbali na kazi, KSI hupenda kutumia muda wake kufanya mazoezi, kuandika muziki, kusafiri na kuendeleza biashara zake.