Jake Paul, tajiri aliyebondwa na tajiri mwenzake
Muktasari:
- Katika pambano hilo ambalo Paul alipoteza raundi ya sita mbali ya kushuhudiwa kwa burudani ya kurushiana ngumi, nje ya ulingo pia kulikuwa na vita ya kifedha.
CALIFORNIA, MAREKANI: WAKATI mwaka huu ukienda kumalizika moja kati ya matukio yaliyotokea Desemba hii ilikuwa ni pambano kati ya Jake Pual na Anthony Joshua lililofanyika kule Marekani.
Katika pambano hilo ambalo Paul alipoteza raundi ya sita mbali ya kushuhudiwa kwa burudani ya kurushiana ngumi, nje ya ulingo pia kulikuwa na vita ya kifedha.
Paul na Joshua ni miongoni mwa mabondia matajiri kwa sasa duniani na hiyo imetokana na malipo ya pesa za mapambano pamoja na madili mengine waliyonayo.
Leo, tumekusogezea ATM ya Paul aliyepokea kichapo, undani wa utajiri wake na mali anazomiliki.
ANAPIGAJE PESA
Asilimia kubwa ya mapato yake kwa sasa inatokana na mapambano mbalimbali anayopigana. Utajiri wake unakadiriwa kufikia Dola 100 milioni.
Kupitia ngumi amekuwa akivunja rekodi za mapato yanayokusanywa akiingiza kati ya Dola 20 hadi 40 milioni kama malipo yake.
Mapambano ambayo yaliwahi kumwingizia pesa nyingi ukiondoa hili la Anthony Joshua lililompa Dola 90 milioni, mengine ni dhidi ya majina makubwa kama Tyron Woodley, Anderson Silva, Nate Diaz na Mike Tyson.
Paul pia bado anaendelea kukunja mpunga wa kutosha kupitia Youtube ambako ana chaneli yake yenye wafuasi milioni 20.
Vilevile ana biashara zake binafsi ambazo ni pamoja na kampuni ya Most Valuable Promotions (MVP), ambayo imekuwa ikisimamia mabondia na matukio ya mapambano mbalimbali.
Kampuni hiyo ina mabondia wa kiume na kiume akiwemo Amanda Serrano. Jane pia ana hisa za katika kampuni za Celsius Energy Drinks, DraftKings, Meta Quest na Experian. Kwa ujumla kwa mwaka anaingiza zaidi ya Dola 100 milioni kupitia sehemu zote.
NYUMBA
Jake Paul anamiliki mijengo kadhaa ya kifahari huko Marekani. Aliwahi kumiliki nyumba kubwa maeneo ya Calabasas, California, iliyojulikana kama Team 10 Mansion, yenye thamani ya zaidi ya Dola 7 milioni ambayo baadaye aliiuza.
Kwa sasa anaishi Puerto Rico ambako amenunua nyumba ya kifahari inayokadiriwa kuwa na thamani ya Dola 16 milioni. Vilvile ana nyumba nyingine jijini Los Angeles.
NDINGA
Ferrari SF90 Stradale (Dola 600,000)
Lamborghini Huracan (Dola 250,000)
Rolls-Royce Cullinan (Dola 350,000)
Tesla Cybertruck (Dola 100,000)
Mercedes-Benz G-Wagon (Dola 200,000)
MSAADA KWA JAMII
Staa huyo ni mmoja kati ya waanzilishi wa taasisi ya Boxing Bullies Foundation iliyoanzishwa 2021 ambayo kazi yake kubwa ni kusaidia vijana wanaohitaji kucheza ndondi na pia imejikita katika kuleta usawa kwenye mchezo huo.
Mara kadhaa pia amekuwa akishiriki kampeni mbalimbali za ukusanyaji pesa kwa ajili ya kusaidia watu wasiojiweza.
MAISHA NA BATA
Jake Paul yupo katika uhusiano wa kimapenzi na mrembo kutoka Uholanzi, Jutta Leerdam, ambaye ni mwanamichezo wa kuteleza kwenye barafu.
Alishinda medali ya Olimpiki katika mashindano yaliyofanyika Beijing 2022. Alimvisha pete ya uchumba 2023. Kwa sasa anaonekana kupunguza zaidi kula bata ikichangiwa na kujiandaa kwake kwa ajili ya mapambano mbalimbali.