Prime
Kipa aishi na risasi mgongoni miaka 13

INAWEZEKANA wengi wamesahau, lakini ukweli ni kwamba Januari mwakani itatimia miaka 14 tangu tukio la kushambuliwa kwa msafara wa Timu ya Taifa ya Togo uliyokuwa ukiingia Angola kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2010.
Timu ya Togo, ilishambuliwa na waasi katika Jimbo la Cabinda, Angola wakati ikiwa mpakani ikiingia ikitokea kambi ya mazoezi iliyokuwa nchi jirani ya Congo Brazzaville baada ya basi la timu hiyo kuvamiwa na kutekwa na waasi hao waliodaiwa walikuwa tisa wakiwa na silaha kali zikiwamo bunduki aina ya AK 47.
Katika tukio hilo, watu watatu walipoteza maisha akiwamo dereva wa basi hilo, Mario Adjoua, Kocha msaidizi wa timu hiyo, Amelete Abalo na Mtangazaji na Mwandishi wa Habari wa Televisheni ya Taifa ya Togo, Stanislas Ocloo ambao walifariki siku moja baada ya tukio hilo la Janauri 8, 2010.
Mbali na watatu hao waliouwawa, pia watu wengine wanane wakiwamo wachezaji walijeruhiwa baadhi wakipata majeraha makubwa yaliyotokana na risasi za waasi hao akiwamo beki Serge Akakpo, Kocha Hubert Velud, daktari wa timu, Tadafame Wadja, Wake Nibombe, Elista Kodjo Lano, Kocha wa Viungo, Divinelae Amevor na kipa Kodjovi Obilale ambaye aliyepigwa risasi ya mgongoni iliyodumu hadi leo.
Ukisikia ule usemi wa kwanza kama kifo chako hakijafikia, huwezi kufa ndivyo ilivyo kwa kipa huyo ambaye kwa miaka karibu 14 sasa anaishi na risasi kutokana na madaktari wa Afrika Kusini kusema wakimfanyia upasuaji wangehatarisha zaidi maisha yake kuliko kuendelea risasi kuwa sehemu ya mwili wake.
Mwanaspoti limewaletea mkasa wa kipa huyo na tukio zima la shambulizi hilo kwa kikosi hicho cha Togo ambacho enzi hizo kilikuwa chini ya nahodha, Emmanuel Adebayor aliyetoa simulizi zima la mkasa huo uliolitia aibu soka la Afrika kipindi hicho mbele ya macho ya wanamichezo duniani.

TUKIO LENYEWE
Ilikuwa Januari 8, 2010 basi la timu ya Taifa ya Togo lililokuwa njiani maeneo ya Cabinda, Angola ikienda kushiriki michuano ya AFCON lilishambuliwa na waasi wa 15 FLEC, Gari hiyo ilikuwa ndio limevuka tu kwenye mpaka baina ya Congo na Angola lilimiminiwa na risasi kwa muda usiopungua dakika 30.
Dereva wa gari Mario Adjoua alikuwa mmoja ya watu wa kwanza kuuawa kwenye shambulio hilo, hivyo gari haikuweza kwenda na wachezaji wakalazimika kulala chini ya vitu kwa ajili ya kuokoa maisha yao.
Timu ya maaskari 10 waliokuwa wanasindikiza msafara huu walijaribu kupambana vilivyo Serge Akakpo ambaye kwa wakati huo alikuwa akiichezea FC Vaslui alipigwa risasi za kutosha na kupoteza damu nyingi.
Mchezaji wa zamani wa Tottenham, Arsenal na Real Madrid ambaye alikuwa ndiye kapteni wa timu kwa wakati huo anasimulia tukio kwa kina kupitia kwenye moja ya mahojiano kwenye chaneli yake ya Youtube.
Adebayor anasema baada ya kambi ya wiki mbili na kuanza safari kuelekea Angola kushiriki mashindano hayo.
“Tulikuwa tumeweka kambi kwenye moja ya hoteli nzuri sana, hapo tulifanya mazoezi kwa wiki mbili na kiukweli maisha yalikuwa mazuri sana, kocha alitupa mapumziko mchana na usiku. Nakumbuka asubuhi ya siku ya tukio husika nilikuwa nawaharakisha wachezaji wenzangu kwamba wafanye haraka ili tuwahi kuondoka kwenda kwenye kambi ambayo tulipangiwa kukaa wakati wote wa mashindano,” anasema Adebayor na kuelezea kwamba kila mtu aliwahi kwa wakati na wakapanda basi.
“Tukiwa kwenye basi kila mtu alikuwa na furaha kama unavyojua sio jambo dogo kuwa sehemu ya timu kwenye michuano ya AFCON, tulikuwa na malengo yetu kama timu na wachezaji binafsi, kwahiyo tupanda basi na tukaanza safari hadi mpakani ili kuingia Angola kutoka Congo, tulipofika hapo tukakuta walinzi kibao, wengi walikuwa wamebeba bunduki, wengine walikuwa wamevalia mabomu.
“Kama wachezaji tulikuwa tunafurahi tu kuwaona, tukawa tunaonyeshana bunduki, umeona kile, umeona hiki, ilikuwa ni furaha tu na tukawa tunacheka na kuinjoi, mimi ndiye niliyechelewesha msafara pale mpakani kwa sababu kadi yangu ya manjano haikuwa inaonekana, kwahivyo niliitafuta na mwisho ikabidi nipate chanjo nyingine, ilichukua kama dakika 30, kumaliza hilo zoezi kisha nikaruhusiwa, kila mtu alikuwa ameshavuka mpaka na walikuwa wananisubiri, kwahiyo nikavuka na hapo nikajiona kwamba rasmi sasa nimeingia kwenye AFCON.
“Kwa sababu nimefika sehemu husika, kulikuwa na mabasi mawili moja ni kwa ajili ya vifaa (chakula, maji, jezi, nk) na lingine ndio tulipanda sisi.”
Adebayor anasema sasa kwenye hayo mabasi mawili ambayo ndio waliandaliwa na CAF kwa ajili ya kuwasafirisha kutoka mpakani hadi kwenye hoteli watakayofikia, kwa bahati mbaya lile ambalo wachezaji walikuwa wamepanda halikuwa na kiyoyozi, na kulifanyika makosa kwa sababu basi ambalo ilitakiwa wapande ni lile waliloweka mizigo.
Anaongeza hakukuwa na namna ikabidi waendelee tu kupanda basi hilo hilo lakini ilibidi wafungue vioo kwa ajili ya kupunguza joto.
“Wachezaji karibia wote walikuwa wamevua mashati, gari likatembea kwa mwendo wa kama dakika 15 hivi, sasa ikiwa imechanganya kitu pekee tulichosikia ilikuwa ni mlipuko na kwa sababu kilikuwa ni kipindi cha Januari, tukaamini huenda bado watu wanafurahia sikukuu za mwisho wa mwaka, lakini tuliposikia mlio huo wa mlipuko tulichanganyikiwa kwa sababu nilikuwa kwenye siti za nyuma kabisa sikuwa nimeona kitu zaidi ya moshi na sauti za watu wakisema lala chini lala chini, baada ya hapo hakuna nilichosikia zaidi ya milio ya risasi na sio milio tu ni milio iliyotoka kwenye bunduki ya ‘mashine gun’, ilikuwa kama sinema.”
Staa huyu anasema kilichoendelea baada ya hapo ni kwamba, vioo vya gari vilivunjika na mmoja kati ya wachezaji akawa anamwambia dereva endelea kuendesha.
“Unajua kulikuwa kimya hivyo baada ya jamaa kusema dereva aendelee kwenda tukasikia sauti ikituambia kwamba dereva amefariki hapo ndio tukajua kwamba sasa mambo yameharibika zaidi, muda huo golikipa wetu namba tatu Kodjovi Obilale nilimsikia akisema “Mguu wangu, mgongo wangu,” lakini sisi tulimzoea kama mmoja kati ya watu wanaopenda sana utani, yaani linapokuja suala la kuchekesha yeye ndiye aliyekuwa mtu pekee wa kufanya hivyo, hivyo kila mtu akajua jamaa anatania, kila mtu akawa anamwambia acha utani, lakini tulikuja kujua kwamba alikuwa hatanii baada ya yeye kujikongoja na kuvua singland yake ya ndani hapo ndo tukaona kwamba kuanzia mgongoni hadi miguuni mwake kulikuwa na damu tu.”
Kwa upande wa wale maaskari waliokuwa wanasindikiza Adebayor anasema ilibidi waende mbali kwanza kisha baada ya hapo wakarudi wakiwa na gari aina ya Toyota Pickup zisizopungua nne walipofika wakasogea hadi karibu ya gari lao kisha wakaanza kurudisha mashambulizi kwa wale waliokuwa wakilishambulia gari la wachezaji.
“Kwa kweli ilikuwa ni kama sinema, unajua tulikuwa tunazisikia bunduki kwa ukaribu kabisa, yaani sikuwa naamini kinachotokea, hapo nilitoa simu nikampigia mke wangu ambaye kwa wakati huo alikuwa na mimba nikamwambia kama atajifungua mtoto wa kiume amuite Emmanuel Juniro na kama wa kike Princess Emmanuela.
‘’Akanambia nini kinaendelea, sikumwambia lakini alisikia milio ya risasi na watu wakiwa wanalia, baada ya hapo tukaona mtu akiwa na bunduki ameingia kwenye gari yetu, hatukujua kama anakuja kutumaliza kabisa ama anakuja kutusaidia, baada ya kuingia akatuambia tutokea twende kwenye zile pickup ambazo walikuja nazo, wachezaji wakaanza kutambaa kutoka nje ya basi na mwisho kabisa nilibakia mimi na Kossi Agassa, tukawa tumeshikana mikono. Yule askari aliyeingia ndani ya basi alivyoona tumeshikana mikono na hatutaki kutoka akatumia bunduki yake kutuachanisha mikono.
“Yule askari akaniuliza wewe ni Adebayor, nikamwambia ndio, akamwambia Agassa aondoke kwenye gari na baada ya hapo akavua nguo yake ya kuzuia risasi na kofia yake ya chuma kisha akanipa na kuniambia nivae, baada ya hapo akanambia shikilia mguu wangu, nikamwambia hapana nataka kusimama sasa wakati naendelea kumbishia ghafla kwenye eneo nililosimama nikasikia bunduki, kuanzia hapo nikaacha ubishi na nikaanza kumsikiliza, akawa anarusha risasi hadi tukafika kwenye moja magari na tukapanda kuondoka eneo hilo. Kiasi kama cha saa moja na dakika 13 tukawa tumefika hospitali.
Walipofika hospitali mmoja kati ya viongozi wa timu ambaye ndiye aliyekuwa msemaji alikuwa akilalamika kwamba ana maumivu na kadiri muda ulivyozidi kwenda ndio alizidi kuwa na hali mbaya walipofika wakamuwahisha haraka kwenye chumba cha matibabu na Adebayor anasema jamaa alikuwa na risasi zisizopungua tatu na mbaya zaidi kulikuwa na tundu moja limeingia risasi tatu.
Haikuchukua muda baada ya kufika hospitalini kiongozi huyo alipoteza maisha, baada ya hapo kocha wao msaidizi naye alipoteza maisha.
“Tulikuwa tunashauriana ikiwa tucheze mashindano ama turudi nyumbani lakini akili zetu hazikuwa sawa hivyo tukaamua tu kurudi nyumbani, tukiwa kwenye ndege ilikuwa ni huzuni sana kwa sababu wenzetu wawili ambao tulikuja nao kwa muda huo walikuwa kwenye eneo la mizigo kama maiti, kwakweli ilikuwa huzuni tangu hapo nilijisemea kwamba kitu chochote nitakachokifanya nikiwa naamini kwamba kitanipa furaha daima nitakifanya.”

NANI ALIWASHAMBULIA
Walishambuliwa na Kikundi cha Front for the Liberation of the Enclave of Cabinda ‘FLEC’ ambacho kimekuwa kikiendesha vita ya msituni dhidi ya Serikali ya Angola tangu mwaka 1975, shauku yao kubwa ikiwa ni kutaka uhuru wa eneo la Cabinda wakiamini eneo hilo halipaswi kuwa sehemu ya Angola na badala yake inabidi liwe eneo huru lenye serikali yake na kila kitu chake.
Baada ya shambulio hilo, walitoa taarifa kupitia katibu wao mkuu iliyosema kwamba “Hili operesheni ndio kwanza imeanza na kutakuwa na matukio mengi kama haya ambayo yatatokea kwenye eneo hili la Cabinda.”
OBILALE NA MIAKA 13 NA RISASI
Baada ya tukio hili Kodjovi Obilale naye alifikishwa hospitalini, baada ya uchunguzi daktari alisema staa huyu amepigwa risasi iliyokaa kwenye mgongo na kama wakiitoa inaweza kumsababishia madhara zaidi hivyo bora iendelee kuwepo, aishi nayo.

Tangu hapo safari ya soka ya Obilale ambaye kwa wakati huo alikuwa akiichezea GSI Pontivy ya Ufaransa iliisitishwa rasmi na amekuwa akitembelea kiti cha matairi mawili ikiwa ni miaka 12 baada ya tukio hilo kwani hawezi tena kutembea kwa miguu yake miwili.
Taarifa kutoka tovuti mbalimbali zinadai kuwa staa huyu amejiendeleza kwa kusoma masuala ya matibabu kwa watoto wenye ulemavu ambapo ameajiriwa kwenye taasisi ya Lorient Association Remise en Jeu.
BAADA YA SHAMBULIO
Baada ya shambulio hilo taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kwamba Polisi wa Angola waliwakamata washukiwa wawili Januari 10, 2010. kisha baada ya uchunguzi zaidi watu tisa wengine walikamatwa.
Waziri wa serikali ya Angola kwa wakati huo, Antonio Bento Bembe aliita tukio kama ni ‘kitendo cha kigaidi’ na akatoa amri ya ulinzi mkali kuzidishwa katika maeneo yote yanayohusiana na mashindano, Martin O’Neill aliyekuwa kocha wa Moustapha Salifou aliyekuwa anaichezea Aston Villa, alionyesha kushtushwa na tukio hilo katika mahojiano aliyofanya na tovuti ya Villa.
Klabu kama Manchester City na Portsmouth zilionyesha wasiwasi wao kuhusu usalama wa wachezaji wao ambao walikuwa wakicheza kwenye mataifa mengine. Mastaa wa soka Benni McCarthy na Momo Sissoko, walilaani shambulizi hilo. kitaifa.
“Serikali imeweka siku tatu za maombolezo nchini kote, ambayo yalianza Jumatatu Januari 11, 2010,” Houngbo alisema kwenye televisheni ya serikali.

MICHUANO ILIKUWAJE?
Katika mashindano ambapo Togo ilipangwa kwenye Kundi B, lililokuwa na wababe kama Ivory Coast, Ghana na Burkina Faso.
Hata hivyo, timu hiyo iliamua kujitoa kutokana na tukio hilo la simanzi lililowavunja nguvu nyota wa timu hiyo, hivyo kundi hilo kusaliwa na timu tatu ambapo, Ivory Coast ilimaliza kinara kwa pointi nne, lakini ikaenda kutolewa kwenye robo fainali dhidi ya Algeria katika mchezo ambao ulienda dakika 30 za ziada baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare.
Ghana ilimaliza ya pili ilisonga mbele hadi fainali na kwenda kufungwa na waliobeba ubingwa, Misri, huku mfungaji bora wa michuano alikuwa ni Mohamed Nagy Ismail Afash (Gedo) aliyefunga mabao matano na mchezaji bora alikuwa ni Ahmed Hassan, wote wakiwa ni raia wa Misri.