Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kipaji kilivyomjenga darasani na uwanjani

Muktasari:

  • Mtazamo huo umewafanya baadhi ya watu kuamini kuwa michezo na elimu haviwezi kwenda sambamba na wengine wakenda mbali zaidi kuwa ni chanzo cha uhuni.

KWA miaka mingi kumekuwepo na dhana ya kwamba wanamichezo wengi hufeli masomo kutokana na kutumia muda wao mwingi mazoezini.

Mtazamo huo umewafanya baadhi ya watu kuamini kuwa michezo na elimu haviwezi kwenda sambamba na wengine wakenda mbali zaidi kuwa ni chanzo cha uhuni.

Hata hivyo, dhana hiyo si sahihi kwa kuwa wapo wanamichezo ambao wamefanikiwa kufanya vizuri darasani huku wakiendelea kung’ara kwenye taaluma zao za michezo.

Kwa uhalisia, mafanikio ya mwanafunzi katika masomo hutegemea nidhamu, usimamizi mzuri wa muda na kujituma wala sio ushiriki katika michezo pekee.

Kwa kawaida michezo huchangia kujenga umakini, nidhamu, uwezo wa kufanya kazi kwa timu na kuhimili changamoto, sifa ambazo husaidia katika masomo.

Jamii inapaswa kutambua kuwa badala ya kuwakatisha tamaa wanafunzi wenye ndoto za kuwa wanamichezo, ni wakati wa kuwapa mazingira yatakayowawezesha kufanikiwa katika elimu na michezo kwa wakati mmoja.

Mwanapoti ilipata nafasi ya kuzungumza mchezaji wa Mpira wa Mikono Zanzibar, Yassir Juma Iddi ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Ndijani Unguja.

Ukiachana na mambo mengine, mchezaji huyo amesema michezo imekuwa miongoni mwa sababu mojawapo inayomfanya kufaulu vizuri masomo yake.

Mchezaji huyo, amesema dhana hiyo imekatisha vijana wengi ndoto zao za michezo na hatimaye kuishia katika mambo wasioyatarajia.

“Michezo ndio sababu kubwa ya wanafunzi kufaulu, kwani hata mimi nisingefanikiwa kufika kidato cha tatu kama ingekuwa hivyo, naisihi jamii iache kuwa na dhana hizo zenye kuzima ndoto za vijana,” amesema


WALIOGUNDUA KIPAJI CHAKE

Yassir anasema, Mwalimu Daudi Martin Samson na Kocha Kombo Ali Kombo hawa ndio waliofanikiwa kuibua kipaji chake na kuanza kumfundisha sheria na mbinu za mchezo huo.

Ingawaje mchezo huo ni urithi kutoka kwa familia yake kwani alikuwa anaushuhudia kwa kaka yake na ndio sababu ya kuvutiwa nao na kujifunza.

“Baada ya kugundua kipaji changu makocha hao wamenifundisha mengi kuhusu mchezo huu hadi kufikia hatua hii na bado wao ndio wanaonisimamia,” anasema


ANACHOJIVUNIA

Mchezaji huyo anasema anajivunia kutwaa tuzo ya mchezaji bora mara mbili mfululizo katika mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (Umitashumta) mwaka 2022 na 2023 wakati akiwa shule ya Msingi Ndijani.

Yassir anasema tuzo hizo zimekuwa kumbukumbu nzuri na zenye historia katika maisha yake tangu aanze kucheza mpira wa mikono.

Anasema kushinda tuzo hizo zimezidi kumpa heshima nyumbani, shuleni na  nguvu ya kufanya mazoezi kwa bidii kwani awali hakuwahi kufikiria kuwa yatatokea hayo.

Pia, anasema tuzo hizo zimemuongezea nguvu ya kupambana na kujiamini kuwa kama atafanya makubwa zaidi ya alivyo sasa.


SIRI YA KUFANYA VIZURI

Yassir amesema siri ya mafanikio yake ni kufanya mazoezi kwa bidii na kufuata maelekezo ya makocha wake, Kombo Ali Kombo na Daudi Martin Samson hao ndio msaada wa kufanya vizuri.

Jambo jengine, anasema ni kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja, jambo ambalo linamsaidia kuwa bora zaidi kila hatua.

Vilevile, Yassir amesema anapenda mpira wa mikono kwa sababu anafurahia namna unavyochezwa na umemsaidia kuwa imara katika masomo yake.


CHANGAMOTO

Anasema, wakati mwengine muda wa masomo na mazoezi vinaingiliana kwahivyo humlazimu kuacha mazoezi na kusoma baada yahapo ndio anafanya binafsi.

Si hilo tu, Yassir anasema changamoto nyengine anasema watu wengi wanadhani mchezo huo huu ni kwa ajili ya wanawake pekee kwa sababu unachezwa kwa mikono kwa maana hiyo anakutana na maneno yasio mazuri.

Yassir amesema, mchezo huo unakabiliwa na changamoto wa vifaa vya kutumia wakati wa mchezo jambo ambalo linakwamisha ndoto zake.


MALENGO YAKE

Anasema, malengo yake ni kufika mbali zaidi katika mchezo huo ili kuwa mchezaji mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.


MECHI DHIDI YA DODOMA ILIKUWA HATARI

Yassir anasema, mchezo wao dhidi ya Dodoma mwaka 2023 katika mashindano yaliyofanyika Mkoa wa Tabora hawezi kuusahau kwa sababu ulikuwa ni kutafuta bingwa wa jumla wa michuano.

Anasema, mchezo huo ulikuwa mgumu upande wao kwakukutana na watu wakubwa wenye nguvu sana ukizingatia umbile lake ni dogo ingawaje walishinda lakini cha moto walikiona.


WACHEZAJI WANAOMVUTIA

Anasema kwa Tanzania anamkubali sana Edward Mbonea na nje ya Tanzania ni Gidsel kutoka Denmark.

Yassir anasema anatumia muda mwingi kuangalia clip zao na kujifunza ili kuongeza ujuzi wake kupitia wachezaji hao.

Mchezaji huyo anasema yapo mabadiliko  ya kimwili na kiakili kama vile kukua, kujitambua na ufahamu kuongezeka baada ya kukutana na watu tofauti.


USHAURI

“Ushauri wangu kwa wahusika wa michezo ni kuwekeza mashuleni kuanzia msingi hadi Sekondari kwa kuandaa mashindano mengi na programu maalum za kufundisha mchezo huu itasaidia kupiga hatua,” anasema.