Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachoifanya Dabi ya K'koo kuwa ndani ya 10 bora Afrika


MASHABIKI na wapenzi wa soka nchini kwa sasa wanahesabu saa tu kuanzia sasa kabla ya macho na masikio kuwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar ambao utatumika kwa pambano la watani za jadi wa soka Tanzania, Simba na Yanga.


Wababe hao wa soka nchini watavaana Jumapili hii kuanzia saa 2:15 usiku katika pambano la  kwanza la Ligi Kuu Bara kwa msimu huu, lakini likiwa la 115 kwa timu hizo katika Ligi Bara tangu 1965. Hii ina maana kuanzia leo Alhamisi, zimebaki kama siku tatu ikiwa ni sawa na saa 72 kabla ya mechi hiyo kupigwa visiwani humo.

Hata hivyo, hilo litakuwa pambano la pili kwa timu hizo kwa msimu huu baada ya awali kuvaana katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Septemba  16, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na Simba kulala kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Pacome Zouzoua dakika ya 54.

Tayari tambo na majigambo kutoka kwa viongozi, wanachama, wapenzi na mashabiki wa klabu hizo kongwe nchini zimeanza mapema, kabla ya dakika 90 za pambano hilo zitakapomaliza ubishi wa kujua kama Simba itafuta uteja mbele ya watani wao hao au itaendelea unyonge.

Kama umesahau ni kwamba katika mechi sita mfululizo zilizopita za mashindano mbalimbali, Simba haijapata ushindi na mechi ya mwisho iliyofungia msimu wa 2024-2025 iliyopigwa Juni 15 mwaka jana, Simba ilikubali kichapo cha mabao 2-0 na kuipa Yanga taji la msimu wa nne mfululizo.

Mechi ya Jumapili itakuwa ya kwanza kwa  Ligi Kuu kwa vigogo hivyo kukutana visiwani Zanzibar, lakini kabla ya hapo zilishacheza mechi kadhaa zikiwamo za Kombe la Mapinduzi na hata Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) mara mbili visiwani humo 1975 na 1992.

Wakati mashabiki na wapenzi wakisubiri kwa hamu pambano hilo litakalokuwa la kwanza kwa Dabi kwa makocha Steve Barker wa Simba na Pedro Goncalves na pia la kwanza kukutana wenyewe kwa wenyewe katika Ligi Kuu Bara kwani wote waliingia mwishoni mwa mwaka jana.

Kama hujui ni kwamba, Dabi ya Kariakoo ni kati ya mechi za dabi zenye mvuto na bora barani Afrika ikitajwa kushika nafasi ya nne.

Usibishe! Hapa chini ni orodha ya Dabi 10 Bora kwa klabu barani Afrika kwa mujibu wa mitandao, huku Dabi ya Cairo, Misri ikishika nafasi ya kwanza kwa mvuto na kukubalika.


CAIRO DERBY

Hii ndio inayotajwa kuwa dabi kali zaidi Afrika na miongoni mwa dabi bora na zenye mvuto duniani. Inajulikana pia kwa jina la Arab Classico na iliasisiwa rasmi mwaka Februari 9, 1917 ambapo Al Ahly ilishinda kwa bao 1-0 na imedumu na kuwa na msisimko mkubwa hadi leo.

Dabi hii uhusisha klabu za Al Ahly dhidi ya Zamalek, kwani mechi baina ya timu hizo huwa sio mchezo na hii imetajwa kutokana na historia kubwa ya mvutano wa kijamii, kisiasa na kihistoria kwa timu hizo zenye mafanikio makubwa nchini humo na Afrika kwa ujumla.


CASABLANCA DERBY

Hii ni dabi ya Morocco, inayotajwa ni ya pili kwa ukubwa na mvuto kwa klabu Afrika nyuma ya ile ya Cairo, ikiwa imeasisiwa mwaka 1957.

Casablanca Derby inatajwa kama moja ya dabi zenye mvuto na msisimko mkubwa duniani ikifutiliwa hadi na UEFA na inazihusisha klabu za Raja Casablanca na mahasimu wao, Wydad Casablanca.

Mara ya kwanza kwa Dabi hiyo kupigwa ilikuwa ni Februari 10, 1957 ambapo Raja ilishinda kwa bao 1-0 na mara ya mwisho kukutana ilikuwa Oktoba 29 mwaka jana bila kutmbiana kwa kutoka suluhu.


SOWETO DERBY

Utasema nini juu ya dabi hii ya Soweto iliyoasisiwa Januari 24, 1970? Hii ni mechi inayohusisha klabu za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates za Afrika Kusini, ikitajwa kushika nafasi ya tatu Afrika kwa msisimko wake. Dabi hii huvuta maelfu kila mwaka, ikiwa na historia ya ubaguzi na mapambano ya uhuru nyuma yake.

Soweto Derby ikipigwa huwa sio mchezo kuanzia nje hadi ndani ya uwanja kutokana na upinzani mkubwa uliopo baina ya timu hizo zikihusisha mashabiki wengi zaidi.

Ingawa Afrika Kusini kuna dabi nyingine kadhaa ikiwamo inayoelezwa kama ndio asilia ya Soweto baina ya Orlando dhidi ya Moroka Swallows, lakini hii ndio kiboko yao kwa sasa ambapo timu hizo zilikutana mara ya kwanza Januari 24, 1970 na Pirates kushinda 1-0 na mara ya mwisho kuvaana ilikuwa Mei 10, mwaka jana na Kaizer Chiefs kushinda 2-1.

Kwa sasa timu hizo zinajiandaa kukutana Jumamosi hii katika mechi ya Ligi Kuu, Kaizer ikiwa wenyeji.


KARIAKOO DERBY

Pambano hilo la Simba na Yanga lililoasisiwa mwaka 1965, ndilo linalotajwa kushika nafasi ya nne kwa msisimko barani Afrika. Hili ni tofauti la dabi nyingine zilizotangulia, kwani hutajwa zaidi kama la watani na sio mahasimu kutokana na namna mashabiki wanavyolichukulia sio kwa uadui.

Dabi hii ndio maarufu zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa imejaa historia, vituko, msisimko na mvuto unaojengwa na rekodi na tambo baina ya timu hizo zenye asili moja, kwani Simba ilizaliwa baada ya kujimegua kutoka Yanga mwaka 1936.

Mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana enzi hizo Simba ikifahamika kama Sunderland ilikuwa ni Juni 7, 1965  ambapo Yanga ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Mawazo Shomvi dakika ya 15, japo mechi haikumalizika kutokana na giza na Yanga kugoma kurudiana na Simba kupewa ushindi wa mezani na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Bara mwaka huo.


TUNIS DERBY

Hii itatajwa kama Dabi ya tano kwa ubora na mvuto Afrika, japo yenyewe mara kadhaa imekuwa ikiishua kwa kuzuka kwa ghasia kutokana na ushindani mkali, historia ya kisiasa baina ya klabu zinazoiunda dabi hiyo.

Tunis Derby inahusisha klabu za Esperance na Club Africain na ni moja ya Dabi kongwe kwani iliasisiwa Machi 24, 1924 ambapo tmu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza na Club Africain kushinda kwa mabao 3-0 na mara a mwisho kuvaana ilikuwa Novemba 9, 2025 na kutoka suluhu.


MASHEMEJI DERBY

Hili ni pambano la mahasimu wa soka huko Kenya, likibebwa na ushindani na upinzani mkali unaosimamia au kuwakilisha tofauti za kijiografia na kihistoria kwa timu za Gor Mahia na AFC Leopards. Ni dabi maarufu Afrika Mashariki, ikifahamika pia kwa jina lingine la Ingo-Dala Derby zihusisha klabu hizo za jijini Nairobi.

Mara kadhaa dabi hii imekuwa ikiishia kwa fujo hadi mtaani kutokana na upinzani unaohusisha makabila makubwa ya nchi hiyo yanayonasibishwa na klabu hizo zilizokutana na kuasisi dabi hiyo Mei 5, 1968. Mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni Desemba 7, mwka jana na Ingwe kushinda kwa bao 1-0 dhidi ya K’Ogalo na zitakutana tena Aprili 26, mwaka huu AFC ikiwa wenyeji.


ALGIERS DERBY

Hii ni moja ya dabi maarufu na kongwe barani Afrika ikihusisha klabu za MC Alger na USM Alger ikiwa imeasisiwa Novemba 14, 1940.

Ni dabi maarufu kwa ukanda wa Afrika Kaskazini ikiwa imejaa siasa, historia, uzalendo pamoja na vita uwanjani, kwani kama zilivyo dabi za ukanda huo mara kadhaa kimewaka uwanjani kutokana ma mashabiki wa timu hizo kuwa ‘vichaa’ wa soka.

Mara ya kwanza kwa dabi hiyo kupigwa ilikuwa Novemba 14, 1940 na MC Alger kushinda kwa mabao 4-1 na zilikutana mara ya mwisho mapema mwaka huu, Januari 17 katika mechi ya Super Cup na MCA kuendeleza ubabe mbele ya wapinzani wao, USMA.


KITWE DERBY

Dabi hii inafahamika pia kwa jina la El Kopala au Chibwe Derby ikiwa ni ya huko Zambia na imekuwa maarufu barani Afrika kutokana na ushindani na msisimko wake ukihusisha klabu za Nkana FC na Power Dynamo zilizopo Kitwe, ukanda maarufu kwa uchimbaji madini ya Shaba.

Historia inaonyesha Dabi hii ya klabu kutoka Copperbelt hupambana kwa heshima ya mji na fahari ya kihistoria, ikiasisiwa rasmi mwaka 1979 na zilikutana mara ya mwisho April mwaka jana na kutoka sare ya 1-1, huku rekodi ikionyesha tangu 2011 zimekutana mara 32 na Dynamos kushinda 16.


OMDURMAN DERBY

Hii ni dabi ya Sudan ikihusisha klabu zenye mafanikio mkubwa nchini humo na Afrika kwa ujumla, Al Hilal na Al Merrikh.

Japo hakuna rekodi zinazoonyesha dabi hiyo ilianza kukutana lini, lakini moja ya mechi nyenye mvuto na kufuatiliwa kwa ukaribu, japo kwa sasa mambo yamewatibukia kutokana na Sudan kuwa katika mgogoro wa kisiasa na kuzifana timu hizo kucheza katika Ligi za mataifa mengine.

Msimu uliopita ilishiriki Ligi ya Mauritania na huko kiliwaka na safari wapo hapo Rwanda wakikinukisha kama kawaida bilaa kujali kama zinacheza ugenini japo zinakosa mashabiki asilia.


ABIDJAN DERBY

Hii ni dabi ya Ivory Coast ikihusisha klabu kongwe za ASEC Mimosas na Africa Sports zilizo na mafanikio mkubwa nchini humo na Afrika kwa ujumla.

Ni moja ya dabi kali za Ukanda wa Afrika Magharibi (WAFU), lakini likini klabu kongwe na zenye mafanikio makubwa nchini humo na Afrika na mechi yao hujaza mashabiki jijini Abijdan zilipo maskani yao.


NYINGINE

Mbali na dabi hizo, lakini zipo nyingine kali katika mataifa mbalimbali ikiwamo zile za DR Congo za Kinshasa Derby kati ya AS Vita na DC Motema Pembe au Lubumbashi Derby inayohusisha TP Mazembe na FC Lupopo.

Pia kuna dabi ya Kumasi inayohusisha Asante Kotoko dhidi ya Heart of Oak kwa pale Ghana, huku kule Libya kuna dabi tamu maarufu kwa jina la Tripoli Derby ikihusisha klabu za Al Ahli Tripoli dhidi ya Al Ittihad Tripoli.

Kwa majirani zetu wa Rwanda kuna dabi ya Kigali ikihusisha APR dhidi ya Rayon Sports au ile ya miamba ya Nigeria Enyimba dhidi ya Iwuanyanwu Nationale mbali na ile ya Uganda Derby kati ya Jogoo SC Villa dhidi ya Express, japo kwa sasa mziki umehamia kwa Vipers v KCCA.

Zipo pia Yaounde Derby ya pale Cameroon kati ya Canon Yaounde na Tonnerre Yaounde na ile Luanda Derby inayohusisha klabu za Petro de Luanda dhidi ua Primeiro na Zimbabwe kuna Dynamos dhidi ya Caps United.

Kifupi karibu kila nchi kuna mechi za kali za dabi zaidi ya moja, lakini zinazotambulika rasmi na kutajwa sana Afrika orodha ni kama ulivyoicheki hapo juu. Ni muda wa kusubiri Dabi ya Kariakoo.