Prime
Kibarua kigumu kocha mpya Simba
NDANI ya misimu minne ya mateso kwa Simba kuanzia 2021/22 hadi 2024/25 wamepita makocha watano ambao wameshindwa kurejesha heshima ya timu hiyo huku watani zao, Yanga wakitesa kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mfululizo ‘back to back’.
Wakati Simba ikiwa na imani kuwa huu huenda ukawa msimu wao wa mafanikio chini ya Fadlu Davids baada ya msimu uliopita kuweka msingi mzuri katika mradi huo huku akipewa uhuru wa kusajili wachezaji ambao aliwahitaji kulingana na mipango yake.
Kocha huyo wa Afrika Kusini aliamua kuachana na miamba hiyo ikiwa ni baada ya mechi ya mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya Gaborone United huko Botswana na kushinda kwa bao 1-0 katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni siku chache tu tangu mechi ya ufungizi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga. Mnyama alipoteza kwa bao 1-0.
Licha ya kukosa ubingwa wa ndani msimu uliopita, Fadlu aliifanya Simba kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ilikuwa ni historia kwao baada ya miaka 31 tangu kucheza fainali ya mwisho katika michuano ya CAF. Kwa miaka mingi chini ya makocha tofauti, Simba ilikuwa ikiishia hatua ya robo fainali.
Fadlu ambaye alidumu Simba kwa siku 444, amewaachia kibarua cha kufanya viongozi wa timu hiyo ambao kwa sasa wanahaha kuhakikisha wanapata mrithi wake huku wakitekeleza mkakati wa muda mfupi kwa kumpa kazi ya muda kocha wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ ambaye atasaidiana na Seleman Matola.
Katika kipindi hicho cha miaka minne, benchi la ufundi la Simba limepita mikononi mwa makocha tofauti mbali na Fadlu wengine ni Pablo Franco (siku 204), Zoran Manojlovic (siku 67), Robertinho (siku 310) na Abdelhak Benchikha (siku 149).
Wote waliishi kwa matumaini, walijaribu kupandisha kiwango cha timu, lakini mwishowe walijikuta wakiacha nafasi yao ikiwa bado na mapengo yale yale, kushindwa kuleta ubingwa wa ndani mbele ya Yanga.
PRESHA YA HESHIMA
Kwa sasa, Simba imebaki kuwa kivuli. Yanga imetawala, jambo ambalo si pigo tu kwa mashabiki wa Simba bali pia limeibua mjadala juu ya uwezo wa viongozi katika kusimamia miradi ya makocha.
Kibarua kikubwa cha kocha mpya atakayekabidhiwa timu hiyo ni kuikomesha kasi ya Yanga. Kuanzia msimu wa 2021/22, Yanga wameonyesha kiwango cha juu, wakisajili makocha wenye dira na kuwa na mfumo wa benchi la ufundi ulio imara. Hata pale walipopoteza baadhi ya nyota, walibaki na muundo unaofanya kikosi chao kuendelea kuwa tishio.
Kwa Simba, changamoto kubwa si tu kushinda mechi za kawaida za ligi, bali ni kuhakikisha wanakuwa na mfumo wa kupambana na Yanga kwenye mechi za moja kwa moja (dabi). Hii ndiyo nguzo kuu ya heshima Tanzania. Kocha mpya atalazimika kuonesha uwezo wake mapema kupitia mechi hizo ambazo kimsingi ndizo zinazoamua mustakabali wa msimu.
FADLU NA CHANGAMOTO ALIZOACHA
Fadlu aliingia Simba akipewa nafasi kubwa ya kuamua sera za usajili na mfumo wa uchezaji. Alijaribu kuleta mabadiliko na kwa hakika alifanikiwa kuifikisha Simba fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kitu ambacho hakijawahi kufanywa kwa zaidi ya miaka 30. Huo ulikuwa mwanzo wa matumaini mapya.
Kocha huyo, aliondoka akiwa amefanikisha mambo kadhaa, lakini amewaachia warithi wake mzigo mkubwa wa kuhakikisha matunda ya msingi aliouacha yanageuzwa kuwa ubingwa wa ndani na mafanikio kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
JAMBO LA KUFANYA
Kocha mpya atakayekuja Simba anakabidhiwa timu yenye vipaji, lakini yenye changamoto kubwa za kimuundo. Miongoni mwa masuala yanayohitaji uangalizi ni usajili wa kimkakati, kivipi? Simba imekuwa na historia ya kusajili wachezaji kwa wingi, mara nyingine bila mpangilio.
Kocha mpya atalazimika kushirikiana kwa karibu na viongozi kuhakikisha kila usajili una mantiki ndani ya mfumo wake.
Jambo lingine ni kuimarisha ukuta, katika misimu mitatu iliyopita, Simba imekuwa ikihangaika katika safu ya ulinzi, hasa katika mechi kubwa. Kocha mpya atahitajika kuunda kikosi cha mabeki kinachoaminika na kuondoa makosa madogo yanayoigharimu timu.
NDOTO ZA AFRIKA
Mashabiki wa Simba wanatamani kuona klabu yao ikifika mbali zaidi ya fainali za Kombe la Shirikisho. Ndoto kubwa ni kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo ambalo linaonekana gumu kutokana na ushindani wa klabu za Kaskazini mwa Afrika na Afrika Magharibi.
Kibarua hiki si rahisi. Ili kufanikisha, kocha mpya atalazimika kufanya yafuatayo, kuinua kiwango cha wachezaji wa ndani na kuhakikisha wanashindana bega kwa bega na nyota wa kigeni. Kuunda mfumo wa kiufundi unaoweza kupambana na klabu za Kaskazini, ambazo mara nyingi hucheza soka lenye nguvu, kasi na mbinu.
USHIRIKIANO NA VIONGOZI
Mojawapo ya changamoto kubwa kwa makocha waliopita ni uhusiano wao na viongozi wa klabu. Kwa mfano, mara nyingine maamuzi ya usajili hayakuwa yakilingana na mipango ya kiufundi ya kocha. Hili limekuwa kikwazo kikubwa kwa Simba kujenga kikosi cha kudumu.
Kocha mpya anapaswa kuhakikisha anakuwa sehemu ya maamuzi makubwa ya kikosi na kuwa na sauti inayosikilizwa. Bila hivyo, historia ya makocha waliopita huenda ikajirudia.
MSIKIE FADLU
Aliyekuwa kocha Simba, Fadlu anasema: “Simba ni klabu kubwa yenye historia na matarajio makubwa kila msimu. Nilipokuwa hapa, niliona jinsi mashabiki wanavyopenda klabu yao na wanavyohitaji kuona heshima ya timu ikirejea ndani na nje ya nchi,”
“Niliamini katika mradi niliouanzisha, niliamini katika wachezaji na niliona mwanga wa mafanikio mbele. Tulifikia fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Huo ulikuwa mwanzo mzuri, lakini bado kulikuwa na kazi kubwa ya kufanya.”
“Changamoto kubwa kwa kocha ajaye ni namna ya kuishinda Yanga. Si kazi rahisi, kwa sababu Yanga imekuwa bora kwa muda mrefu. Lakini ninaamini Simba bado ina kila kitu kinachohitajika, vipaji, mashabiki na rasilimali kurejea kwenye nafasi yake ya juu. Kocha mpya akipata msaada sahihi wa viongozi anaweza kuleta mabadiliko makubwa.”