Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kamati ya Saa 72 sasa iheshimu FVS

ZENGWE Pict


BODI ya Ligi Tanzania Bara (TPLB), imeanza kutumia teknolojia ya msaada wa video (Football Video Support, FVS) katika mechi zake kwa ajili ya kuwasaidia waamuzi angalau wawe na uhakika mkubwa kabla ya kufanya uamuzi.


Teknolojia hiyo hutumia kamera za mrushaji wa matangazo kwa njia ya televisheni kwa ajili ya kupata marudio ya matukio tata ambayo makocha wataona hayakufanyiwa uamuzi sahihi.


Kwa mujibu wa protokali za teknolojia hiyo, kila kocha atapewa nafasi mbili au kadi mbili za kuomba tukio alilo na wasiwasi nalo liangaliwe vizuri na mwamuzi kwa kwenda pembeni ya uwanja ambako kunakuwa na waendeshaji video wawili.

Kocha hutakiwa kunyoosha kidole kwa mwamuzi wa akiba na baadaye hupewa kadi. Iwapo tukio alilotaka liangaliwe kwa makini litasababisha refa abadili uamuzi wake, kocha huyo atarudishiwa kadi na hivyo kuendelea kuwa na nafasi mbili.

ZENG 05

Iwapo refa ataendelea kushikilia uamuzi wake, kocha huyo atakuwa amepoteza nafasi moja na kubakiwa na moja.

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), liliamua kuruhusu teknolojia hiyo baada ya kuona baadhi ya mataifa hayawezi kumudu gharama za teknolojia nyingine ya mwamuzi msaidizi wa video (VAR), ambayo haitumii kamera za mrushaji wa matangazo.

Matukio yanayohusika katika teknolojia hii ni yale ya makosa ya wazi na dhahiri katika uamuzi kuhusu uwezekano wa kufungwa bao, uwezekano wa penati, uwezekano wa kadi nyekundu ya moja kwa moja au refa kumuonyesha kadi mchezaji ambaye hakustahili.

Na protokali hizo zinasema uamuzi wa refa ni wa mwisho. Ujio wa matumizi ya teknolojia hiyo angalau unashusha pumzi kwa waamuzi ambao kwa takriban misimu minne wamekuwa gumzo katika mijadala inayohusu uamuzi mbovu na makosa ya kibinadamu.

ZENG 02

Angalau yale makosa yaliyoanza kuota sugu, maarufu kama makosa ya kibinadamu yatapungua na ubishani kuhusu makosa ya waamuzi utapungua. Ni muhimu sasa kwa Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi maarufu kwa jina la Kamati ya Saa 72 ikaheshimu protokali za FVS kwa kuanza kuwatafutia makosa  waamuzi na kuwafungia.

Ni matumaini kuwa kamati hiyo itaheshimu uamuzi wa waamuzi kama teknolojia hiyo inavyotaka kuwa uamuzi wa refa ni wa mwisho na kuepuka kuhalalisha mijadala ya redioni na kwenye mitandao ya kijamii kwa kuwafungia waamuzi watakaolalamikiwa hata baada ya kutumia teknolojia hii.

Mijadala ilishaanza baada ya tukio la Peter Shelulile kuokoa mpira kwa mguu ndani ya eneo la penalti wakati mshambuliaji wa Simba alitaka kuupiga mpira huo kwa kichwa wakati wa mechi ya ufunguzi wa msimu kati ya Yanga na Simba.

ZENG 04

Baada ya kuombwa kwenda kuangalia tukio vizuri, mwamuzi Ahmed Arajiga aliridhika kuwa hakukuwa na mchezo wa hatari katika tukio hilo.

Na kama protokali zinavyotaka refa huyo aliutangazia umma kuwa mchezaji aliyekuwa timu iliyokuwa inalinda lango aliupiga mpira na hivyo hakukuwa na faulo. Wengi walianza kuponda mitandaoni kuwa Arajiga hakuwa sahihi kwa sababu lilikuwa tukio la hatari lililohusisha kichwa na mguu na hivyo ilikuwa ni lazima aamue iwe penalti.

ZENG 01

Lakini, sasa zilezile kamera ambazo Kamati ya Saa 72 ilikuwa inatumia kuadhibu waamuzi ndizo hizohizo ambazo marefa watatumia kuondoa utata katika uamuzi. Maana yake ni kwamba matukio yote tata na ya dhahiri yataombewa kuangaliwa upya na wahusika, na hivyo hakutakuwa na haja tena ya kuangalia yale ambayo hayakurudiwa na kutumia kuadhibu waamuzi.

Kwa njia moja au nyingine, Kamati ya Saa 72 ilichangia sana kushusha hadhi ya waamuzi wetu kwa kubeba mijadala ya redioni, kwenye televisheni na mitandaoni kuhusu matukio tata na kuamua kama mijadala ilivyotaka. Hii haikuwa sahihi kwa sababu waliokaa kurudia matukio walitumia teknolojia kupata sehemu fulani ya usahihi, wakati waliofanya uamuzi hawakutumia teknolojia yoyote kuwasaidia kuamua.

Ilikuwa ni kama kuwaambia watu ni kweli waamuzi walikuwa wakifanya makosa makubwa na wakati mwingine kuthibitisha tuhuma kuwa walikuwa wanataka kuibeba timu moja. Hii iliwaweka waamuzi kwenye hali ngumu kiasi kwamba ilionekana kama ni sahihi kuleta waamuzi kutoka nje eti kuchezesha mechi za watani wa jadi badala ya kutafuta suluhisho.

ZENG 03

Hilo pia lilishusha hadhi ya waamuzi wetu na kuwaondolea kujiamini katika majukwaa makubwa. Siyo ajabu kwamba huwa hatuna waamuzi katika mashindano makubwa si tu ya dunia, bali hata Afrika kwa sababu hali ya kujiamini inakuwa haipo na ni rahisi hilo kuonekana.

Pamoja na kuingia kwa teknolojia hiyo, bado kunahitajika juhudi kubwa za kukuza viwango vya waamuzi wetu na kuwaongezea hali ya kujiamini. Ni muhimu pia masuala ya waamuzi yakashughulikiwa na waamuzi wenyewe kwa kutoa taarifa ya matukio tata yaliyofanyika kwenye raundi moja ili kuwapa elimu zaidi mashabiki, waandishi wa habari na wachambuzi.