Straika Mashujaa kutimkia Kagera Sugar
Muktasari:
- Nyota huyo aliyejiunga na Mashujaa, Julai 29, 2025, akitokea Mbeya City, amefikia makubaliano ya awali na Kagera Sugar kwa ajili ya kukichezea kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027, huku akiwekewa mkataba wa miaka miwili.
BAADA ya Kagera Sugar kukata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2026-2027, mabosi wa timu hiyo wanasuka upya kikosi hicho na sasa wako katika hatua za mwisho za kumsajili aliyekuwa nyota wa Mashujaa FC, Mudathir Said.
Nyota huyo aliyejiunga na Mashujaa, Julai 29, 2025, akitokea Mbeya City, amefikia makubaliano ya awali na Kagera Sugar kwa ajili ya kukichezea kikosi hicho kwa msimu wa 2026-2027, huku akiwekewa mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Kagera Sugar, Bernard Samson Sikira, alisema uongozi wa timu hiyo umeshakamilisha baadhi ya sajili za wachezaji wapya, ambapo muda wowote kuanza sasa wataanza kuwatambulisha rasmi kwa mashabiki zao.
“Tumebakisha baadhi ya taratibu ndogo kwa ajili ya kuweka hadharani kikosi chetu cha msimu wa 2026-2027, usajili wetu umezingatia mapendekezo ya benchi la ufundi na malengo tuliyojiwekea ya kufanya vizuri na kuleta ushindani,” alisema.
Mwanaspoti linatambua Mudathir aliamua kuvunja mkataba wa mwaka mmoja Mashujaa ili kujiunga na Kagera Sugar, ambayo imemuwekea kiasi kikubwa cha fedha.
Mshambuliaji huyo licha ya kuchezea Mbeya City na Mashujaa, pia amecheza Coastal Union na Pamba Jiji akiungana na nyota wapya ambao ni beki wa kushoto anayemudu kucheza beki ya kati, Boniface Onyango kutoka Kakamega Homeboyz ya Kenya.
Nyota wengine waliosajiliwa na Kagera Sugar ni washambuliaji, Collins Maina aliyetoka Fortune Sacco FC ya Kenya na Naku James akitoka Polisi Tanzania, sambamba na viungo, Said Ndemla kutoka JKT Tanzania na Daudi Milandu kutokea Dodoma Jiji.
Kagera Sugar imemrejesha tena beki wa kulia wa kikosi hicho, Dickson Mhilu aliyeondoka Dodoma Jiji.