John Bocco anasogea mdogomdogo
Muktasari:
- Hii ni taarifa njema sana imepokelewa hapa kijiweni kwa sababu Bocco ni miongoni mwa wachezaji ambao wamefanya vizuri sana katika soka letu kabla ya kuhamua kustaafu na baadae kuanza kufundisha soka la vijana.
JUZI tumeona mashambuliaji wa zamani wa Simba na Azam, John Bocco maarufu kama Adebayor, akiwa miongoni mwa wahitimu wa kozi ya ukocha wa soka leseni B.
Hii ni taarifa njema sana imepokelewa hapa kijiweni kwa sababu Bocco ni miongoni mwa wachezaji ambao wamefanya vizuri sana katika soka letu kabla ya kuhamua kustaafu na baadae kuanza kufundisha soka la vijana.
Tunapomwona Bocco anahitimu leseni B inatupa imani kubwa hapa kijiweni tunakwenda kumpata miongoni mwa makocha bora baadae katika nchi yetu.
Bocco ana heshima kubwa katika soka letu. Ni mtu ambaye ana nidhamu kubwa ambayo ameionyesha kabla na baada ya kuataafu kucheza soka.
Pia tangu anacheza, alionyesha dalili atakuja kuwa kocha mzuri na hilo linajidhihirisha katika timu za vijana za Simba ambazo anazifundisha hivi sasa.
Zinacheza soka la kufundishwa, soka la mipango na mbinu na zinaonyesha ni timu ambazo zimepitia katika mafunzo sahihi ya mtu sahihi.
Lakini kitu kingine ambacho tunaamini kitambeba Bocco katika ukocha siku za usoni ni ile heshima ambayo ameijengea kutokana na mafanikio aliyoyapata akiwa mchezaji.
Ameshinda mataji yote makubwa ya soka ya ngazi ya klabu ndani ya nchi hii tena akiwa nahodha, pia ameshinda taji akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Kijiwe kinamtakia kila la heri John Bocco katika maisha yake ya ukocha. Kinaamini ataongeza elimu zaidi na siku moja atakuwa kocha mkuu wa timu ya Ligi Kuu.