Hongera Mayele japo DR Congo imetolewa
Muktasari:
- Hapa kijiweni tulishapata matumaini DR Congo ingevuka hasa baada ya kutangulia kufunga bao mapema kipindi cha kwanza na kucheza kwa muda mrefu bila kuruhusu bao la wapinzani.
SAFARI ya DR Congo katika Kombe la Dunia iliishia juzi Jumatano baada ya kuchapwa mabao 2-1 na England katika hatua ya 32 bora.
Hapa kijiweni tulishapata matumaini DR Congo ingevuka hasa baada ya kutangulia kufunga bao mapema kipindi cha kwanza na kucheza kwa muda mrefu bila kuruhusu bao la wapinzani.
Hata hivyo, mabao mawili ya England katika dakika 15 za mwisho yakahitimisha ndoto ya DR Congo na Waafrika wengi kijumla ya timu hiyo kuingia robo fainali.
Hata hivyo, jambo ambalo limetufurahisha hapa kijiweni ni kuona mshambuliaji Fiston Mayele akipata fursa ya kucheza katika mashindano hayo makubwa na yenye thamani na mvuto zaidi duniani.
Mayele hachezi hapa nchini kwa sasa na yupo Misri anakoichezea Klabu ya Pyramids FC lakini kabla ya kwenda huko alipita hapa na akacheza kwenye ligi yetu na aliitumikia Yanga.
Jambo la kufurahisha zaidi, jamaa amemaliza mashindano hayo akiwa amefunga moja kati ya mabao manne ambayo DR Congo imeyapata katika fainali hizo mwaka huu huku mengine yakipachikwa na Yoane Wissa.
Hili ni jambo kubwa sana kwa sababu kila Mayele anavyopata mafanikio kisoka, inakuwa ni rahisi kwa Tanzania kutajwa na kuhusishwa kwa vile hapa ndio palikuwa daraja la yeye kufika alipo hivi sasa.
Pongezi nyingi kwa Mayele kwa kushiriki Kombe la Dunia na kufunga bao kwani sio mafanikio rahisi kwa mchezaji kuyafikia hasa kwa anayecheza ligi za Afrika.