Prime
Dube, Depu Yanga imejilipua!
YANGA imeingia kwenye msimu mpya ikiwa imefanya maamuzi makubwa ya kukibadili kikosi chake, lakini hakuna uamuzi unaozungumzwa zaidi kuliko kuondoka kwa washambuliaji Laurindo Depu na Prince Dube.
Ni wachezaji waliobeba sehemu kubwa ya mabao ya timu katika misimu iliyopita, hivyo kuondoka kwao kunafungua mjadala mkubwa kama mabingwa hao wamefanya uamuzi wa kimkakati wa kuanza ukurasa mpya au wamejitengenezea tatizo litakalowagharimu katika Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Depu alitua Yanga akitokea Radomiak Radom ya Poland akiwa na matarajio makubwa. Ingawa alicheza kwa kipindi kifupi baada ya kusajiliwa dirisha dogo, alianza kuonyesha dalili za kuzoea mazingira na mfumo wa timu.
Kwa upande wa Prince Dube, alitokea Azam FC akiwa tayari ni mshambuliaji aliyefahamu mazingira ya soka la Tanzania. Ndani ya miaka miwili aliyokaa Jangwani, alijijengea heshima kubwa kutokana na mabao na mchango wake katika mafanikio ya timu.
Swali kubwa linaloulizwa sasa si kama Yanga ilikuwa na uwezo wa kuwapata washambuliaji wapya, bali kama ulikuwa wakati sahihi wa kuondokana na wachezaji wawili waliokuwa tayari wamejenga uelewano na kikosi.
MABAO YAO YALIIBEBA YANGA
Kwa misimu miwili iliyopita, Dube alikuwa mmoja wa washambuliaji walioibeba Yanga kwenye mechi nyingi muhimu. Alifunga katika Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho na michuano ya CAF huku akitoa mchango mkubwa wa pasi za mwisho.
Laurindo Depu naye, licha ya kucheza nusu msimu, alionyesha ubora wake kwa haraka. Alikuwa miongoni mwa wachezaji waliobadili taswira ya safu ya ushambuliaji kutokana na kasi yake, uwezo wa kutafuta nafasi na utulivu mbele ya lango.
Kilichowafanya wawe muhimu hakikuwa idadi ya mabao pekee, bali uwezo wao wa kuamua mechi. Mara nyingi walikuwa wakitumia nafasi chache kuzalisha matokeo makubwa, jambo ambalo si rahisi kulipata kwa kila mshambuliaji.
DUBE ALIKUWA MSHAMBULIAJI WA MECHI KUBWA
Dube alijenga sifa ya kuwa mshambuliaji wa mechi zenye presha. Alikuwa akitumia nguvu zake, uimara wa mwili na uwezo wa kushinda mipira ya juu kuwatesa mabeki.
Mbali na kufunga, alikuwa akivuta mabeki wawili au watatu jambo lililowapa nafasi viungo washambuliaji na mawinga kuingia kwenye maeneo hatari. Hiyo ndiyo sababu hata siku ambazo hakufunga, bado alikuwa na mchango mkubwa katika mfumo wa timu.
DEPU ALIKUWA SILAHA YA KASI
Depu alikuwa na sifa tofauti kabisa. Alikuwa na kasi, uwezo wa kupenya katikati ya mabeki na kutengeneza nafasi mwenyewe.
Mchezaji huyo alikuwa na uwezo wa kubadili matokeo ndani ya dakika chache. Aliweza kuisumbua safu ya ulinzi kwa harakati zake bila mpira na alikuwa miongoni mwa washambuliaji waliokuwa wanaipa Yanga mbinu tofauti za kushambulia.
Ndani ya muda mfupi alionyesha kuwa angeweza kuwa tegemeo kubwa zaidi kama asingepata majeraha au angeendelea kubaki kikosini.
REKODI ZAO
Kwa pamoja Dube na Depu walichangia mabao 46 pamoja na pasi 16 za mabao. Dube alifunga mabao 32, huku Depu akifunga 14.
Hizi si takwimu ndogo kwa timu inayoshindania mataji ndani na nje ya nchi. Maana yake ni Yanga imeondokewa na sehemu kubwa ya mchango wa mabao iliyokuwa ikiitegemea katika mechi nyingi.
Sasa jukumu hilo linahamia kwa Peter Shalulile, Cheikh Touré pamoja na washambuliaji wengine wapya ambao bado wanahitaji muda wa kuonyesha uwezo wao.
JE, WANAWEZA KUZIBA PENGO?
Historia ya Ligi Kuu Bara inaonyesha si kila mshambuliaji mkubwa anafanikiwa mara moja.
Msimu uliopita Yanga ilimsajili Balla Conte pamoja na Celestine Ecua, lakini hawakuweza kuwa na mchango mkubwa kama ulivyotarajiwa.
Hiyo inaonyesha ubora wa mchezaji pekee hautoshi. Lazima aelewe mfumo wa kocha, aina ya viungo anaocheza nao na mazingira ya ushindani wa ligi.
Ndiyo maana mashabiki wengi bado wana wasiwasi kama Shalulile na Touré wataweza kuanza kufunga mapema au watahitaji muda mrefu wa kuzoea.
HATARI IKO HAPA
Mashindano ya CAF hayatoi nafasi nyingi za kufunga.Mara nyingi timu hupata nafasi mbili au tatu tu ndani ya dakika 90. Hapo ndipo umuhimu wa mshambuliaji mwenye uzoefu unapojitokeza.
Iwapo washambuliaji wapya watashindwa kutumia nafasi hizo mapema, Yanga inaweza kujikuta ikitawala mchezo lakini ikashindwa kupata ushindi.
Pia mzigo mkubwa unaweza kuhamia kwa viungo washambuliaji kama Allan Okello kutengeneza na wakati mwingine kufunga mabao, jambo ambalo linaweza kuathiri uwiano wa timu.
Zaidi ya hilo, ukitazama washambuliaji wapya utagundua kuwa Peter Shalulile ndiye mwenye uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, huku Cheikh Touré akitokea Saudi Arabia akiwa bado hajapata uzoefu mkubwa wa mashindano ya CAF.
MTIHANI WA MAKOCHA
Benchi jipya la ufundi chini ya Manqoba Mngqithi linaanza kazi likiwa tayari limepoteza washambuliaji wawili waliokuwa wamezoea mfumo wa timu.
Kocha atalazimika kujenga upya safu ya ushambuliaji huku akihakikisha washambuliaji wapya wanaingia haraka kwenye mfumo wa timu.
Si kazi ya kufundisha pekee, bali pia kujenga maelewano kati ya washambuliaji, viungo na mawinga kwa muda mfupi kabla ya mechi muhimu za Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na CAF hazijaanza.
UAMUZI UTAHUKUMIWA UWANJANI
Katika soka, maamuzi ya usajili hayahukumiwi siku yanapofanyika bali yanahukumiwa uwanjani.
Kama Shalulile, Touré na washambuliaji wengine watafunga mabao mengi na kuendelea kuipa Yanga mataji, viongozi watapongezwa kwa maamuzi yao.
Lakini kama safu ya ushambuliaji itaanza kusuasua, mashabiki hawatasita kulinganisha kila mechi na mchango uliokuwa unatolewa na Dube na Depu.
Kwa sasa Yanga imechagua kuanza ukurasa mpya. Swali linalosubiriwa kujibiwa ni kama ukurasa huo mpya utakuwa bora kuliko ule uliomalizika au kuondoka kwa Dube na Depu kutageuka kuwa moja ya maamuzi yatakayojadiliwa kwa muda mrefu ndani ya klabu hiyo.
WASIKIE WADAU
Mchezaji wa zamani Simba Dua Said anasema hawezi kumzungumzia sanaa Dube kwa sababu alishafanya kazi yake ndani ya miaka miwili na mkataba wake ukamalizika.
"Shida kubwa naiyona kwa Depu ni mchezaji ambae ameingia dirisha dogo kwa hiyo haikuwa sawa kwa Yanga kumwondoa kwa sababu alishaanza kuzoea mazingira na huenda angewaka sana.
"Yanga imefanya matumizi mabaya ya fedha, kusajili wachezaji wapya wakati wapo ambao tayari wameshafahamu ligi yetu ilivyo ni kama wanacheza karata au kamari hujui matokeo yatakavyokuwa.
"Mzize bado sio uhakika sana kutokana na majeraha ila Depu alikuwa fiti kabisa na alishaanza mazoezi, hesabu walizopiga Yanga zinawaweka njia panda kwa sababu sio rahisi kupata wachezaji watakaowaka haraka kama Allan Okello."
Mkongwe Abdallah Kibadeni anaamini viongozi wa Yanga wameamua kubadili safu ya ushambuliaji kwa kuangalia muda mrefu, lakini anaonya kuwa mabadiliko hayo yanaweza kuwa na gharama katika mechi za mwanzo wa msimu.
"Ukibadili washambuliaji wote kwa wakati mmoja unakuwa umechukua hatari. Washambuliaji wapya wanahitaji muda wa kuzoea wachezaji wenzao na mfumo wa kocha. Ndiyo maana mechi za mwanzo zinaweza kuwa ngumu kabla hawajapata maelewano."
Shabiki wa Yanga Juma Abdallah anasema wao kama mashabiki wanachotaka ni kuiona timu yao inapata ushindi bila kujali nani ametoka kwa sababu wanaamini macho ya viongozi wao yanaona mbali.
"Sio kila mchezaji anauwezo wa kuwaka ila shida inakuja kwa mashabiki ambao tunataka matokeo na kiukweli shauku yetu kubwa ni ushindi isiwe kama timu pinzani msimu mzima wanacheza na mtu mmoja mbele.
Mchambuzi Charles Abel anasema ujio wa Shalulile umeongeza nguvu kubwa sana Yanga hasa kwenye eneo hilo la mbele, pia kuuzwa kwa Depu ni hesabu nzuri.
"Alikuja Depu akakliki mapema tu, pia Dube sio kwamba hakuhitajiwa na Yanga ila wakati wa mazungumzo yeye akaamua kuondoka kwa hiyo hayo sio maamuzi ya Yanga.
"Yanga imepata faida ya kumuuza Depu kwa sababu timu imepata pesa nyingi msimu mzima kwa klabu kama Yanga kunahitaji matumizi makubwa ya pesa, hivyo kuwapa imani na wale waliopo nadhani ndio jambo jema zaidi.
"Ni mapema sana kusemea uamuzi wa Yanga kwa sasa kwani msimu bado haujaanza ukizingatia wapo wazoefu wengi kama Okello ambao wakiunganika pale na wageni hao basi unapata picha ya ushindani mkubwa wa Ligi Kuu Bara na ushindi wa Yanga."