HISIA ZANGU: Ugonjwa wa kumlaumu Mbwana Samatta utakwisha lini?

Summary

MARA baada ya kumalizika kwa pambano kati ya Tanzania dhidi ya Berlin pale Uwanja wa Mkapa- Temeke, mwandishi mmoja asiyejitambua alimfuata Mbwana Samatta na kumuuliza swali. “Mashabiki wamekuwa wakisema wewe hauna mchango mkubwa ukirudi nyumbani tofauti na Ulaya.”

MARA baada ya kumalizika kwa pambano kati ya Tanzania dhidi ya Berlin pale Uwanja wa Mkapa- Temeke, mwandishi mmoja asiyejitambua alimfuata Mbwana Samatta na kumuuliza swali. “Mashabiki wamekuwa wakisema wewe hauna mchango mkubwa ukirudi nyumbani tofauti na Ulaya.”

Kudai kwamba mwandishi asiyejitambua ni kitu sahihi zaidi. Huyu alikuwa mwandishi wa michezo au alikuwa mwandishi wa siasa? Huyu alikuwa mwandishi wa masuala ya jamii au alikuwa mwandishi wa masuala ya mazingira?

Kama Mwandishi ni wa michezo anapaswa kuufahamu mchezo wenyewe. Anapaswa kuwa na mtazamo wake binafsi kuhusu anachokiona kwa Samatta na timu kwa ujumla. Hapaswi kuongozwa na hisia za mashabiki au kuchukua maneno ya mashabiki ya mtaani.

Kama ingekuwa kuna kashfa ya Samatta mtaani kwake basi Mwandishi angeweza kuuliza ‘watu wanasema’. Kama Samatta angekuwa amefanya jambo la hisani mtaani mwandishi angeweza kuanza kwa kusema ‘watu wanasema.’ Lakini hii ilikuwa ni mechi ya soka ambayo Mwandishi alikuwepo uwanjani.

Mwandishi hana maoni yoyote ya maana licha ya kuutazama mpira kwa dakika tisini. Wakati yeye ndiye ambaye alipaswa kutoa mwongozo kwa mashabiki, bahati mbaya yeye ndiye ambaye anapewa mwongozo na mashabiki. Kama angekuwa ameutazama mpira huo ni kwamba Samatta hakufunga tu lakini alishafanya mambo mengi sahihi. Ni kama pia ilivyokuwa katika pambano la juzi pale Benin.

Samatta anacheza vizuri akiwa na Stars ingawa kwa sasa hajafunga sana. Akiwa na Stars anacheza chini. Anachukua mipira, anakokota, anapiga pasi za kuunganisha timu ëLink upî. Inawezekana anafanya haya kwa sababu ya timu yetu ilivyo.

Alipokuwa kule Genk aliwahi kuniambia kwamba kocha wake alimtaka asimame katikati tu na kufunga. Ni tofauti na mpira alioondoka nao akiwa Simba ambapo alikuwa anakokota kwa muda mrefu na kufunga. Kule walikuwepo kina Leon Bailey wa kumfanyia kazi hizi. Yeye alihitajika kusimama pale katikati tu.

Huku Tanzania Samatta anacheza ule mpira wake wa zamani. Kuna akina nani zaidi wa kumfanyia kazi? Anacheza na wachezaji wa kawaida tu. inabidi pia ajifanyie kazi nyingi ambazo Ulaya huwa anafanyiwa zaidi na kujikuta akiwa mviziaji.

Mwandishi hawezi kuliona hili kwa sababu kila mtu anasubiri Samatta afunge tu basi. Samatta asipofunga anabebeshwa mzigo wa lawama mitaani na katika mitandao ya kijamii. Ni kitu cha kawaida kwa sababu amekuwa mhanga wa ukubwa wake. Na hasa linapokua suala kwamba yeye ni Mtanzania.

Watanzania wamezoea lawama. Hawawapendi watu wao ambao wamekuwa wakubwa. Samatta anastahili heshima kubwa nchi hii. ameamsha ndoto za vijana wengi ambao waliona kuna baadhi ya mambo hayawezekani.

Kuna watu wa aina mbili ambao huwa wanamlaumu sana Samatta. Kuna wale ambao hawaelewi mchezo wenye ulivyo kama huyu Mwandishi. Na Kuna watu pia ni wasahaulifu wa kujua ni namna gani Samatta ni shujaa wetu.

Katika hili la pili, ukweli ni kwamba leo hii Samatta asipoitwa katika timu ya taifa bado anastahili kupewa heshima kubwa kuliko hao wachezaji walioitwa kikosini.

Leo hii Samatta hata akiisha na kujikuta anachezea Ruvu Shooting ya Massau Bwire bado anastahili heshima kubwa kuliko wachezaji wote wa Tanzania wanaocheza ndani na nje ya nchi.

Ukihesabu mambo ambayo amejifanyia mwenyewe na ameifanyia nchi ni mengi. Ukihesabu rekodi nyingi ambazo ameweka na ambazo kila mahala zinatufanya tuandike kuwa ‘Ni Mtanzania wa kwanza.’ Basi Samatta anastahili kupewa heshima kubwa na sio mwandishi mmoja kubeba kipaza sauti na kuzungumza maneno ya mitaani huku mpira wenyewe akiwa hauelewi.

Kabla haujamlaumu Samatta unapaswa kujikumbusha kwamba ni Mtanzania wa kwanza kuchukua ubingwa wa Afrika, Mtanzania wa kwanza kuwa mfungaji bora Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Mtanzania wa kwanza kuwa mwanasoka bora wa ndani Afrika, Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu Ubelgiji, Mtanzania wa kwanza kufunga mabao mengi Ubelgiji, Mtanzania wa kwanza kuuzwa pesa nyingi Ulaya, Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya England.

Mtanzania wa kwanza kufunga bao Ligi Kuu ya England, Mtanzania wa kwanza kuzifunga Liverpool na Manchester City, Mtanzania wa kwanza kucheza katika klabu kubwa Uturuki. Kuna rekodi nyingi ambazo hazitafutwa.

Kabla ya kuhoji uzalendo wa Samatta lazima tujiulize ni lini aligoma kuja kuichezea timu ya taifa tangu akiwa na TP Mazembe, Genk, Aston Villa, Fenerbahce na sasa Royal Antwerp ya Ubelgiji. Mara zote amekuwa akipatikana. Unajua anatumia saa ngapi hewani kwa mwaka kurudi kuichezea timu ya taifa au kuifuata popote ilipo?

Tatizo kubwa wachezaji wazuri au wakubwa wanaocheza timu zetu za Afrika wamekuwa wakiingia katika matatizo kama haya kwa sababu mashabiki wanaamini kwamba wao ni malaika waliokuja kutukomboa. Hawaamini kama wao ni binadamu wa kawaida.

Katika pambano dhidi ya Benin pale Temeke, mastaa wetu wengine Simon Msuva na John Bocco walikosa mabao ya wazi. Kama mabao hayo yangekuwa yamekoswa na Samatta nadhani angelaumiwa mara mbili ya zile lawama zilizokwenda kwa Msuva na Bocco.

Kama angekosa Samatta lazima tungeambiwa tu kwamba ìPale Msuva hakukosiî. Bahati nzuri kwa Msuva ni kwamba kwanza anacheza na Samatta katika timu moja, lakini pili amekuwa na mwenendo mzuri wa kufunga katika siku za karibuni akiwa na kikosi cha Stars.

Kama Samatta asingekuwepo nchi hii ina maana mzigo wote mzito ungekuwa unaangukia kwake. Kwa sababu anacheza Waydad Casablanca ya Morocco na kwa sababu ingekuwa timu kubwa zaidi miongoni mwa timu za wachezaji wetu basi Msuva naye angekuwa anabebeshwa mzigo huu wa lawama.

Kama hili unabisha basi jikumbushe tu kwamba Samatta ana mabao mengi katika kikosi cha Stars kuliko Msuva. Lakini hapo hapo kama Samatta asingekuwa Mtanzania basi sasa hivi Msuva angekuwa analaumiwa sana licha ya mabao yake ambayo yamekuwa yakitusaidia siku za karibuni.

Watanzania tujifunze kuacha lawama za kijinga. Haipo kwa Samatta tu. Watanzania wanawasakama akina Diamond Platinumz na Hassan Mwakinyo kutokana na kuwa wahanga wa mafanikio yao. Diamond alipoteuliwa kuwania tuzo fulani miezi ya karibuni kuna watanzania walimsapoti msanii kutoka Nigeria ili Diamond ashindwe.