HISIA ZANGU: Sio bahati mbaya akina Chirwa kucheza soka Tanzania
Muktasari:
Kule Zambia wameshaweka kanuni isiyosomeka kwamba mchezaji yeyote anayekuja kucheza soka la kulipwa Tanzania basi asahau kuchaguliwa timu ya taifa. Jaribu kujikumbusha, kuna mchezaji yeyote wa Zambia aliyewahi kucheza nchini kisha akaitwa timu ya taifa? Jikumbushe kuhusu Davies Mwape na Felix Sunzu.
OBREY Chirwa anajua kweli mpira. Kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita alikuwa akifunga mabao ya video tu. Anajua kwelikweli mpira. Anatumia mguu wa kushoto vizuri. Lakini nahisi hatumii akili yake vizuri katika mambo mengine.
Kule Zambia wameshaweka kanuni isiyosomeka kwamba mchezaji yeyote anayekuja kucheza soka la kulipwa Tanzania basi asahau kuchaguliwa timu ya taifa. Jaribu kujikumbusha, kuna mchezaji yeyote wa Zambia aliyewahi kucheza nchini kisha akaitwa timu ya taifa? Jikumbushe kuhusu Davies Mwape na Felix Sunzu. Walipocheza nchini hawakugusa timu ya taifa ingawa awali walikuwepo.
Pasipoti yake inaonyesha kuwa alizaliwa Februari 12, 1994. Kwa sasa atakuwa na miaka 23 tu, lakini ameamua kutocheza Timu ya Taifa ya Zambia kwa sababu ameamua kuja Tanzania. Anaijua vema kanuni hii. Hautasikia ameitwa labda aende kwingineko ambapo soka lao lipo juu zaidi ya Zambia.
Kwanini Chirwa alimpiga mpigapicha wiki iliyopita? Jibu ni rahisi tu kwamba hayupo hapa kwa bahati mbaya. Kwa kipaji chake angeweza kuwa mbali zaidi ya hapa. Wakati akiwa Zimbabwe aliwahi kwenda Denmark akafuzu majaribio, lakini akarudi Zimbabwe kimyakimya huku klabu yake ikishangaa.
Hayupo hapa nchini kwa bahati mbaya. Yupo sehemu anayostahili. Yupo sehemu ambayo ina wachezaji wengi wazawa ambao hawana sifa ya kuwa wachezaji wa kulipwa. Lakini pia yupo sehemu ambayo tumekuwa tunapokea wachezaji wengi wa kigeni ambao hawana sifa za kuwa wachezaji wa kulipwa kama yeye.
Mchezaji kupigwa picha ni kawaida tu, hasa akiwa mazoezini. Mchezaji kupigwa picha hata akiwa jukwaani ni jambo la kawaida tu. Kitu ambacho sio cha kawaida ni mchezaji kupigwa picha akiwa katika maisha ya faragha.
Lakini naambiwa kuwa Chirwa ana tabia ya kushuku ushirikina kutoka kwa wachezaji wenzake wa Yanga hasa wale wa nyumbani. Naambiwa kuwa hata wachezaji wa Yanga walifurahi kuona mwandishi anakwenda polisi kumshtaki Chirwa. Wenzake inadaiwa kuwa hawazipendi tabia zake.
Ninachowashangaa wenzake ni namna ambavyo wanashindwa kung’amua kuwa mchezaji kama yeye yupo nchini kwa sababu ya tabia hizohizo anazowaonyesha. Mzambia mwenye kipaji cha uhakika ni nadra kuja Tanzania hata kama atapata mshahara mzuri.
Mzambia anayeweza kuja hapa ni yule ambaye labda umri wake umekwenda kama ilivyokuwa kwa Mwape na Sunzu, au yule ambaye hana malengo na Timu ya Taifa ya Zambia, au yule ambaye hana mpango wa kuchuma pesa za nje ya nchi yake katika nchi zilizoendelea kisoka.
Mchezaji anayempiga mpigapicha katika mazingira ya uwanjani hafai kuwa mchezaji wa kulipwa. Lakini hainishangazi sana kwa sababu achilia mbali Chirwa, Tanzania imeendelea kupokea wanasoka wengi wa kigeni ambao wana vipaji, lakini hawajafika hapa kwa bahati mbaya.
Wamefika hapa kwa sababu tabia zao haziwezi kuwapa mafanikio nje ya Tanzania. Hatuwezi kuwataja majina lakini kuna wanasoka wengi wa kigeni ambao wanafika nchini na kujitumbukiza katika anasa. Vipaji vyao vinafia hapa.
Wanafika wakiwa na majina makubwa, lakini kila siku vipaji vyao vinayeyuka kwa kuendekeza starehe. Vipaji vyao vinakwenda kumalizika katika vitanda vyao na baadhi ya mabinti wa Bongo Movie. Ni ukweli ambao viongozi na wanachama maarufu wa klabu hizi wanaujua.
Ulaya kuna wanasoka wa namna hii, lakini wana bahati kwamba wamezaliwa huko na hawalazimiki kufunga safari za kwenda huko. Hawa ndio akina Joey Barton ambao wamebebwa na ukweli kwamba wamezaliwa Ulaya. Kama wangezaliwa Afrika wasingefika Ulaya kwa sababu hawana sifa.
Alichofanya Chirwa kwa mpigapicha wa gazeti ni kitendo tu kinachodhihirisha hakuja hapa kwa bahati mbaya. Amekuja katika tabia za watu wa aina yake. Ndio maana hata kuna viongozi na wanachama wa Yanga wanamtetea. Viongozi hawa na wanachama wamezoea kuishi na wachezaji wa aina ya Chirwa kwa miaka nenda rudi.
Chirwa yupo katika sehemu sahihi kabisa kwa kitendo alichofanya. Mchezaji mwenye kipaji, nidhamu, umri mdogo hawezi kutoka Zimbabwe akaja Tanzania. Lazima kuna jambo. Sio bure kama watu wengi wanavyodhani.