Fatema; Ukimsikiliza utauona mwanzo mpya wa safari ya maisha yako
Muktasari:
- Ni mwanamke anayetumia muda mwingi kujifunza vitu na kubuni kipi kifanyike, anajitoa kusaidia vijana na wanawake kuzifikia ndoto zao kwa kuwasapoti kipesa na kuwapa elimu.
HUENDA kuna mwanamke sehemu anayepitia nyakati mgumu, anajiona thamani yake imeshuka, hana mchango katika jamii na amezikatia tamaa ndoto zake. Hata hivyo, kama akibahatika kukutana na alichozungumza mlezi wa Simba Queens na mjumbe wa bodi ya Singida Black Stars, Fatema Dewji, atapata mwanzo mpya wa safari yake.
Mwanaspoti lilifunga safari kutoka Tabata Mwananchi kwenda kufanya mahojiano maalumu na Fatema katika ofisi zake zilizopo Posta, jijini Dar es Salaam na miongoni mwa mambo muhimu aliyoyazungumzia ni mwanamke kuzigeuza changamoto kuwa fursa.
Waandishi wa makala haya walipokelewa kwa tabasamu la ukarimu, unyenyekevu na upendo mkubwa, utambulisho ukafanyika kisha yakaanza mahojiano, yanayolenga kutambua nguvu ya mwanamke katika jamii.
Ni mwanamke anayetumia muda mwingi kujifunza vitu na kubuni kipi kifanyike, anajitoa kusaidia vijana na wanawake kuzifikia ndoto zao kwa kuwasapoti kipesa na kuwapa elimu.
Fatema aliyesoma Shule ya Sekondari ya International School of Tanzania na Chuo cha Georgetown kilichopo Washington DC, Marekani, anatoa somo kwa wanawake kutumia muda mwingi kujishughulisha, kujijali, kujitunza na kujifunza kila siku badala ya kupoteza muda kwa vitu visivyo na maana.
Alisomea masuala ya fedha (finance) na teolojia katika chuo hicho, kabla ya kurejea Tanzania na majukumu kutokana na taaluma hiyo ikiwamo kusomea mambo ya masoko.
"Wakati nafanya kazi ya mambo ya fedha nilikuwa nakaa muda mwingi ofisini, hilo sikulipenda nilitamani nifanye kazi ya kunikutanisha na watu mara kwa mara ili kuendelea kujifunza vitu vingi kuhusu jamii, hivyo nilikuwa natumia muda wa Chakula cha mchana 'lunch' kwenda kuzungumza na wauza maduka, wafanya biashara mbalimbali, lengo nilitaka nijue soko la Afrika linahitaji vitu gani, maana chuo nilichosoma wanafundisha mambo ya Ulaya zaidi," anasema Fatema na kuongeza;
"Baada ya kufanya utafiti huo kwa muda mrefu pia nilikuwa nazungumza na baba yangu mara kwa mara kujua uzoefu wake kwa muda aliyofanya biashara, basi nikaenda kusomea mambo ya masoko ya Afrika ndipo nikaanza kufanya kazi hiyo.
"Nilianza kufanya kazi na mtu mmoja anaitwa Robert, bado yupo, ila kwa sasa nafanya kazi na watu 200 ambao wamepata ajira, ukiacha hilo, pia nina shule ninayowafundisha watoto kuhusu mambo ya AIA, natambua baada ya miaka 10 kila kitu kitakuwa huko, sayansi na teknolojia ndivyo vinavyoshika dunia."
RATIBA ZAKE
Anasema angalau kwa sasa anapata muda kidogo wa kupumzika, tofauti na nyuma pumzika yake ilikuwa ni wakati anakwenda (kufanya ibada) kuswali.
"Familia yangu wananiambia unapaswa kupumzika, unafanya sana kazi. Nipo katika biashara, mlezi Simba Queens nipo Singida Black Stars (SBS), nina vipindi ninavyofundisha wanawake kujua thamani na urembo wa asili walionao, namna wanavyotakiwa kuzungumza mbele ya watu kwa kutumia sauti ya ushawishi, kutumia muda mwingi kujifunza vitu vipya badala ya kukaa kuzungumzia watu mambo ambayo hayawezi kubadilisha kitu chochote katika maisha yao," anasema Fatema na kuongeza;
"Mwanamke ili ajiamini lazima awe na mpangilio wa ratiba, asipende kupoteza muda wake na vitu visivyo vya maana, badala yake atumie muda huo kufuatilia vitu vitakavyomfunza. Mfano mimi nilikuwa natembea madukani, masokoni ili kufanya tafiti ya kipi naweza nikakifanya.
"Pia lazima mwanamke ajipende kimwonekano, kusali kila mtu kwa imani yake, kujua anakula nini ili kulinda afya ya mwili, kufanya mazoezi baada ya kuamka, kuamka mapema na kupangilia vitu, asiiache haiba ya kuwa mwanamke, kwa kutumia sauti nyororo anapozungumza na watu hata kama ana kazi nzuri kiasi gani haiwezi kumbadilisha asiwe mwanamke, pia ajue kupika, anayezingatia hayo lazima thamani yake iwe juu, maana muujiza wa kwanza ni uhai tulio nao na kuamka kila siku siyo jambo jepesi," anasema Fatema.
Ukiachana na majukumu hayo pia anasema alianza kucheza gofu tangu akiwa na miaka sita na kila siku alikuwa anapiga mipira 200 hadi kuna kipindi alikuwa anaona kama baba yake anamsumbua, ila faida anayopata anampa maua yake mzee Gullam.
"Mzee ni mtu mwenye nidhamu ya juu katika kufanya vitu vyake, anafokasi na mambo yake, ana bidii, watoto wake wote ametulea kwa staili hiyo, nimepata nafasi ya kusomeshwa chuo kikubwa duniani, naamini anajivunia mimi kwani nafanya kile alichotamani kukiona kwangu," anasema.
Fatema anasema anacheza michezo mbalimbali miongoni mwa hiyo ni tenisi na gofu na ana 'handcup' tisa na aliwahi kufika tatu, amechukua tuzo zaidi ya 200 katika mashindano ya nje na ndani.
MAJUKUMU YAKE SIMBA QUEENS
Ukiachana na jukumu la kutafuta wadhamini, anahakikisha wachezaji wanapata lishe nzuri, kuelewa matumizi ya mitandao ili kujipatia kipato, kuwafunza kuhusu uwekezaji wa maisha yao ya baadaye.
"Awali ilikuwa ngumu kupata wadhamini, lakini kwa sasa wanatupigia simu wao wenyewe, pia inatokana na ushawishi tulioutengeneza, awali wakati najiunga na Simba Queens tulikuwa tunakuta mashabiki wawili au watatu, ila kwa sasa wanakwenda wengi," anasema Fatema na kuongeza;
"Pia mitandao ya Simba Queens ya kijamii ina wafuasi wengi, tofauti na mwanzo pia tunawafundisha jinsi ya kujipenda na kukaa katika mwonekano wa kike, haijalishi wanacheza mpira wa miguu, ile ni kazi.
"Ninawaomba mashabiki wa mpira wa miguu Tanzania wazisapoti timu zote za wanawake na isiwe Simba Queens pekee, kwani wanapofanikiwa wanakuwa wamemwinua mtoto wa kike."
Anasema kabla ya kujikita na Simba Queens alikuwa shabiki wa Arsenal, ila kwa sasa ameiweka pembeni na wala hafuatilii kwa sababu hataki kuongeza presha: "Simba Queens inapocheza nakuwa na presha kubwa hata Simba ya wanaume, ndiyo maana sishabikii tena Arsenal, sitaki presha zingine."
SIKU YA WANAWAKE
Kitu alichokipanga kukifanya kuadhimisha siku ya wanawake duniani, anasema amewachagua wanawake 10 na atawapa zawadi kubwa ya kuendeleza biashara zao pamoja na mafunzo ya kipi wakifanye ili wasonge mbele.
"Hao wanawake 10 wanilitafuta mtandaoni wakanielezea changamoto zilizowakwamisha biashara zao, nitawashika mkono na kuwapa elimu ya kipi wakifanye, itakuwa zawadi kubwa na wataifurahia," anasema.
SIRI YA MWILI WAKE
"Nafanya mazoezi, nazingatia ulaji wa chakula sahihi, kuhusu urembo ni kujiamini na kujipenda hakuna vitu vingine, siamini katika kutumia mavitu mengi, siyo mtu wa kujaribisha nguo nyingi, ninayochukua kuvaa ndiyo hiyo hiyo, maana napenda kwenda na muda, napenda vitu vya fasheni na huku mbeleni nitaanzisha brandi yangu ya nguo," anasema na kuongeza;
"Nisisitize mwanamke ukitumia muda kujitunza kwa kufanya usafi wa mwili kama inavyotakiwa, utajiamini, pia afya yako ya akili itakuwa nzuri, maana muda mwingi utatumia kuwaza vitu vya maana na siyo ambavyo haviongezi chochote maishani mwako, wasome vitu vyenye manufaa kila wakati itawasaidia."
MWANDISHI WA VITABU
Anasema kutokana na utafiti aliokuwa anaufanya na kujifunza maisha ya watu kila siku katika jamii hadi sasa ameandika vitabu 10 na anatarajia kuendelea kuandika na anapenda pia kusoma vya wengine.
"Kitabu cha kwanza nimeandika kuhusu masoko ya Afrika na ndani yake kuna stori ya maisha yangu. Kinaonyesha nilivyokuwa naenda masokoni kuzungumza na watu, kuzungumza na baba kila kitu kipo mle, kuna kitabu kinachohusu kuzungumzia vizuri biashara unayofanya, kingine mtu anavyotakiwa kujibrandi, kipo cha kuyajua masoko na namna mtu anavyoweza kuanza na mtaji mdogo hadi akawa bilionea, vipo vingi na nawaza kuandika kitabu cha maisha yangu na Simba Queens," anasema na kuongeza;
"Kutokana na soka nimekutana na watu tofauti, wanaofikiria vitu kwa ukubwa, bado naendelea kuwaza kufanya mengi zaidi hasa kusaidia vijana na wanawake."
STORI ZA FAMILIA ZA KITAJIRI
Fatema anasema wanapokusanyika familia nzima kwa chakula cha pamoja, asilimia kubwa ya stori wanazozungumza ni kuhusu biashara na michezo.
"Tunatumia muda tunaokutana katika chakula cha pamoja kuzungumzia biashara na mpira, maana kwa asilimia kubwa tumekuwa katika misingi hiyo, hivyo tunajikuta hatuna stori nyingi, ndiyo maana ni vigumu mimi ukanikuta natoka na marafiki kwenda kuangalia move ingawa ni kitu kizuri, lakini kwa upande wangu naona napoteza muda," anasema.
Mbali na hilo anasema mama yake mzazi aliwajenga katika nidhamu hakutaka waje wapotee:
"Mama na baba wametusaidia sana kutujengea nidhamu, ndiyo maana katika familia yetu kila mtu anapambana kwa kadri anavyoweza."
BONDI YAKE NA MO DEWJI
Anasema ni binti wa mwisho kuzaliwa kati ya watoto sita, hivyo kila mtu anamtazama kama mtu wa kipekee, lakini bondi yake na mwekezaji wa klabu ya Simba na mfanyabiashara, Mohammed Dewji 'Mo Dewji' ni kubwa kutokana na mambo ya mpira wa miguu.
"Kwanza nimejifunza utoaji wake kwa jamii, ni mtu anayependa kuona vijana wanafikia malengo na kujikwamua na umaskini, hilo linanipa nguvu na wakati mwingine ananiambia naona bidii yako, endelea kusonga mbele, lakini na wengine wote wananipa moyo sana," anasema.