Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Familia ya Dewji inavyopitia magumu ndani ya Simba


MWAKA 1986 Simba SC ilifanya uchaguzi mkuu uliowaweka madarakani viongozi wapya, Mwenyekiti Emmanuel Makaidi na Katibu Mkuu Jimmy David Ngonya.


Wakati huo katibu mkuu anachaguliwa na wanachama, hivyo anakuwa na nguvu za kisiasa...Ngonya alikuwa na nguvu kwelikweli hadi akabatizwa jina la utani la Gorbachev, akifananishwa na Rais wa Urusi wa wakati ule, Mikhail Gorbachev.


Lakini bahati mbaya kwao ni kwamba uongozi wao ulikumbwa na ukosefu wa amani klabuni na kusababisha timu kuyumba sana.

Simba ikanusurika kushuka daraja siku ya mwisho ya msimu, kwa misimu mitatu mfululizo ambayo Ngonya na Makaidi walikuwa viongozi.

Misimu hiyo ni 1987, 1988 na 1989. Itakumbukwa kwamba wakati ule msimu ulienda sambamba na kalenda ya kawaida ya mwaka, yaani kuanzia Januari hadi Desemba.


1987

Baada ya kuwa na msimu mbaya, Simba iliingia siku ya mwisho ikiwa ya mwisho kwenye msimamo.

Mechi yao ya mwisho ilikuwa dhidi ya mabingwa watetezi,  Tukuyu Stars ya Mbeya.

Mechi ikaisha kwa sare ya 5-5, Simba kunusurika kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Japo waziri wa michezo wakati huo, Fatma Said Ally, alifuta matokeo haya, na mengine mengi siku hiyo kwa viashiria vya upangaji matokeo...ila Simba ikakwepa aibu ya kushuka daraja.


1988

Huu ulikuwa msimu wa pili mfululizo kwa Simba kunusurika kushuka daraja.

Walienda siku ya mwisho ya msimu wakiwa kwenye orodha ya timu zitakazoshuka.

Ili wasishuke, wanapaswa kushinda mechi yao ya mwisho ambayo ilikuwa ni dhidi ya Yanga.

Yanga wenyewe waliingia kwenye mechi hii wakitafuta sare tu ili wawe mabingwa.

Simba wakashinda 2-1 na kunusurika...Yanga wakakosa ubingwa, ukachukuliwa na Coastal Union.


1989

Simba iliingia siku ya mwisho ya ligi ikihitaji sare tu ili ikwepe kushuka daraja.

Wapinzani wao walikuwa majirani zao, Pilsner, timu iliyokuwa ikimilikiwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL).

Pilsner hiyo ilikuwa na wachezaji wawili wenye damu ya Simba, kipa Idd Pazi 'Father' na beki Jamhuri Kihwelo 'Julio'.

Wachezaji wengine waliobaki walikuwa damu ya Yanga.

Yakatokea yaliyotokea, mechi ikaisha 1-1 na Simba wakanusurika.


UJIO WA KWANZA DEWJI

Baada ya kadhia yote hii, Simba ikapata tajiri wa kuweka pesa ili kuimarisha timu.

Tajiri huyo ni Azim Dewji, mfanyabiashara mzawa mwenye asili ya Asia.

Dewji alipelekwa Simba na katibu mkuu wa muda wa FAT, Leodegar Tenga.

Yeye alitaka kuifadhili timu ya taifa, lakini Tenga akamsihi aende akaifadhili Simba kwani ikiimarika na timu ya taifa itaimarika.

Dewji akaenda Simba mwaka 1990, na kubadilisha kila kitu.

Simba wakashinda ubingwa wao wa kwanza wa ligi baada ya miaka 10.

Mara ya mwisho Simba kushinda ubingwa wa ligi ilikuwa 1980, walikaa eda hadi 1990 alipokuja Azim Dewji.

Yaani Azim Dewji aliikuta Simba inapambana kushuka daraja, akaipa ubingwa kwa kutumia uwekezaji wake.

Haikuishia hapo 1991 na 1992 Simba ikashinda ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, sasa Kombe la Kagame.

1993 ikashinda ubingwa wa ligi ya Muungano na kubwa kuliko zote ni kufika fainali ya Kombe la CAF.

Misimu miwili mfululizo iliyofuata, 1994 na 1995, Simba ilishinda ligi zote mbili, ya bara na Muungano.

Na ikashinda tena Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati 1995 na 1996.

Simba ilikuwa ya moto sana.

Ikaibuka migogoro mikubwa na Dewji kuonekana mtu mbaya Simba.

Mtu ambaye alitumia pesa zake kuijenga upya timu iliyoelekea kushuka daraja hadi kuwa kinara wa Afrika...akaonekana mbaya, akafukuzwa kwa kejeli nyingi sana.


UJIO WA PILI WA DEWJI

Baada ya Azim Dewji kuondoka, Simba ikaelekea kurudi ilikotoka.

Ikaukosa ubingwa wa ligi tangu ilipochukua kwa mara ya mwisho 1995, hadi 2001 alipokuka Dewji mwingine, Mohamed ambaye sasa ni Mo.

Mohamed 'MO' Dewji alianza kuingia Simba 1999 akiikuta ikiwa hoi bin taaban.

Akaanza taratibu kujenga kikosi imara kilichokuja kushinda ubingwa 2001, walipotwaa ligi zote mbili, ya Bara na Muungano.

Pia walitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati.

Wakatwaa tena ubingwa wa Muungano 2002 na wa Bara 2003.

Mwaka 2003 pia Simba chini ya Mo Dewji ikafanya maajabu kwa kuwatoa mabingwa watetezi wa Afrika, Zamalek, kwenye raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa.

Simba wakafuzu hatua ya makundi, na wakafanya vizuri kwani walimaliza katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 7.

Hii ni tofauti na Yanga ambayo ilishika mkia kwenye kundi lake, ilipofuzu hatua kama hiyo mwaka 1998.

Hii iliwezekana tu kwa pesa za Mohamed Dewji.

Wakatwaa tena ubingwa wa bara mwaka 2004.

Mwaka 2005, Mohamed Dewji akaondoka Simba, baada ya maneno maneno mengi yaliyojaa dharau kejeli na dhihaka.

Simba ikarudi kwenye kuunga unga na kubabaisha kiasi cha kuhitaji ufadhili wa Khalid Adam Wilson.

Hiki ni kitu ambacho watu wengi hawakijui. Khalid Adam alikuwa akifanya biashara zake Japan na kujipatia riziki yake.

Rafiki yake mkubwa alikuwa Jamhuri Kihwelo ambaye alikuwa kocha msaidizi katika zile nyakati za unga unga mwana baada ya kuondoka Mo.

Simba ilikuwa na hali mbaya kiuchumi hivyo Khalid akawa anaisaidia kama kumuunga mkono rafiki yake.

Simba ilienda Nigeria kucheza na Enyimba mwaka 2007, yeye akilipia gharama za hoteli kule...na mambo mengine mengi kama posho za wachezaji na kadhalika.

Hii ilipelekea biashara zake kufilisika na mtaji kuanguka.

Miaka mingi baadaye Jamhuri Kihwelo akawa kocha wa Mwadui ya Shinyanga, akamchukua Khalid Adam kumfanya kuwa meneja wa timu.

Akiwa hapo akasomea ukocha na baadaye akawa kocha wa hiyo timu.


UJIO WA TATU WA DEWJI

Maisha ya Simba yakaendelea kuwa ya kuunga unga hadi Mo aliporudi tena 2017. Aliikuta Simba iko hali mbaya ikikosa ubingwa tangu 2012.

Akajenga kikosi imara kilichokuja kutawala mpira wa Tanzania kwa miaka minne mfululizo.

Simba hii ikafungua milango ya Tanzania kuamini Afrika inawezekana. Kucheza hatua ya makundi kukawa jambo la kawaida kwa Simba.

Msimu uliopita Simba imecheza tena fainali ya Afrika, safari hii Kombe la Shirikisho.

Hii yote ni kwa nguvu kubwa ya pesa ya familia ya Dewji, safari hii akiwa ni Mo Dewji.

Lakini licha ya yote hayo, familia hii imekuwa ikiishia kutukanwa, kukashifiwa na kudhihakiwa.

Watu wanaofanya hivyo hata fedha za kumudu familia zao hawana.

Poleni sana kina Dewji!