Falconets; Wakongwe wanaorudi kusaka taji
Muktasari:
- Nigeria inaingia Poland 2026 ikiwa imefuzu kwa mara ya 12, jambo linaloifanya kuwa moja ya timu zenye uzoefu mkubwa katika historia ya mashindano hayo.
NIGERIA ni moja ya timu ambazo zimejijengea jina kubwa kwenye mashindano ya Kombe la Dunia kwa wanawake U-20. Timu hiyo inayofahamika kwa jina la Falconets imetengeneza heshima kubwa kwenye mashindano hayo na sasa inarudi tena kwenye jukwaa la dunia ikiwa na kiu ya kuvuka hatua ambayo imekuwa ikiwakosesha usingizi kwa muda mrefu.
Nigeria inaingia Poland 2026 ikiwa imefuzu kwa mara ya 12, jambo linaloifanya kuwa moja ya timu zenye uzoefu mkubwa katika historia ya mashindano hayo.
Licha ya kuwa na historia kubwa duniani, kuna kitu kimoja ambacho Nigeria bado inakitafuta ambalo ni taji ililolikosa kwa miaka 12 iliyoshiriki.
FALCONETS WAMEWAHI KUFIKA FAINALI MBILI
Nigeria imewahi kucheza fainali mbili, mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2010, walipofika hatua ya mwisho na kukutana na Germany, Safari yao iliishia kwenye medali ya fedha baada ya kupoteza mchezo huo.
Miaka minne baadaye, mwaka 2014, Falconets walifika fainali lakini wakakutana tena na Ujerumani na kuishia kushindwa, kwa hiyo mara mbili ambazo Nigeria imefika fainali, imeondoka ikiwa mshindi wa pili.
Hawaendi Poland kwa ajili ya kuongeza tu idadi ya ushiriki wao bali wanaenda wakitaka kuandika ukurasa mpya na ikiwezekana kurudi Nigeria na Kombe la Dunia.
Kwa ujumla, Nigeria ni moja ya timu zilizofanya vizuri zaidi kutoka Afrika kwenye mashindano haya na historia yao ya kufika fainali mara mbili ndiyo inayowafanya kila wanapoingia kwenye Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 20 kupewa heshima na wapinzani.
NJIA YA KWENDA POLAND HAIKUWA RAHISI
Safari ya Nigeria kuelekea Poland haikuwa ya kawaida Falconets walikutana na Rwanda katika hatua ya pili ya kufuzu na walionyesha ubora kwa kushinda kwa jumla ya mabao 5-0.
Baada ya hapo wakakutana na Senegal ambako walifanikiwa kusonga mbele baada ya kushinda kwa jumla ya 3-1,hatua ya mwisho ikawapeleka Malawi, na huko safari haikuwa rahisi kama hatua zilizotangulia.
Nigeria ilishinda mchezo wa kwanza 2-0, lakini kwenye mchezo wa marudiano Malawi ilipata ushindi wa 2-1, Pamoja na kipigo hicho, Nigeria ilisonga mbele kwa jumla ya mabao 3-2 na kufunga tiketi ya kwenda Poland. Nigeria ya mwaka huu ni timu ambayo inayoweza kushinda, lakini pia imeonyesha kwamba inaweza kulazimika kupambana hadi dakika za mwisho.
UZOEFU WA MASHINDANO
Silaha kubwa ya Nigeria ni uzoefu, Timu hii haijafika Poland kwa bahati kwani imefuzu mara 12 na imewahi kufika fainali mara mbili.
Uzoefu huo unaweza kuwa na thamani kubwa kwenye mashindano ambayo wakati mwingine mechi moja tu inaweza kuamua kama timu inaendelea au inarudi nyumbani.
Mbali na uzoefu, maandalizi ya Falconets yamejikita katika kujenga timu yenye nidhamu, utimamu wa mwili, uelewa wa mbinu na mshikamano.
Kocha Moses Aduku amekuwa akisisitiza umuhimu wa maandalizi ya kimwili na kiakili, huku akitaka wachezaji wake waingie kwenye mashindano wakiwa tayari kupambania ubingwa.
Shirikisho la Soka la Nigeria, NFF, pia limeeleza kuwa maandalizi ya timu yalihusisha kazi ya kiufundi, utekelezaji wa mbinu, utimamu wa mwili na kujenga mshikamano ndani ya kikosi.
UDHAIFU WA NIGERIA
Kinachowapa nguvu kinaweza pia kuwa chanzo cha presha, Nigeria ina historia kubwa kwenye mashindano haya, lakini historia hiyo inakuja na matarajio makubwa.
Baada ya kufika fainali mara mbili na kushindwa, kila kizazi kipya cha Falconets kinapopelekwa Kombe la Dunia hujikuta kikikabiliwa na swali lilelile Je, huu ndiyo mwaka wa Nigeria kubeba kombe? Presha hiyo inaweza kuwa kubwa hasa kwenye hatua ya mtoano, ambapo kosa moja linaweza kumaliza safari ya timu nzima.
Safari ya kufuzu pia imeonyesha kuwa Nigeria haiwezi kucheza kwa mazoea, Ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi uliwapa faida nzuri kabla ya mchezo wa marudiano, lakini Malawi walifanikiwa kushinda 2-1.
MOSES ADUKU ABEBA MATUMAINI
Mbele ya jukumu hilo yupo Moses Aduku, kocha aliyepewa kazi ya kuiongoza Nigeria kwenye kampeni ya Poland 2026, Aduku amesisitiza maandalizi, nidhamu na umakini. Wakati wa safari ya kufuzu, alitaka wachezaji wake wawe tayari kimwili na kiakili, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kama timu moja na kazi yake kubwa ni kubadilisha uzoefu huo wote kuwa matokeo.
Nigeria ina historia ina vipaji na uzoefu, Kinachohitajika sasa ni kuunganisha vitu hivyo na kupata matokeo uwanjani.
SURA YA KUNDI F
Nigeria imepangwa Kundi F pamoja na Hispania, China na New Caledonia.
Hapa ndipo kazi halisi inaanzia kwani Spain ni timu inayojulikana kwa mchezo wa pasi, umiliki wa mpira na ubora wa kiufundi.
China nayo inarudi kwenye mashindano baada ya kukosa matoleo yaliyopita, ikiwa na historia ya kuwa mabingwa wa dunia.
New Caledonia, kwa upande mwingine, inaingia kwenye mashindano haya ikiwa ni moja ya timu zitakazokuwa zikifanya historia ya kwanza kwenye Kombe la Dunia la U-20 la Wanawake.
Kwa Nigeria, jambo la kwanza ni kuvuka hatua ya makundi lakini kwa historia waliyonayo, mashabiki wao watataka zaidi ya hapo.
NINI WANACHOHITAJI KUFIKA FAINALI?
Nigeria inahitaji kutumia uzoefu wake bila kubebwa na historia inahitaji kuwa makini inapokuwa mbele, kuwa na nidhamu inapokuwa ikishambuliwa na kutumia nafasi inapozipata.
Pia, Falconets wanahitaji kuhakikisha mechi ambazo wanaonekana kuzimiliki hazigeuki kuwa vita dakika za mwisho. Mchezo wa Malawi kwenye kufuzu ni mfano mzuri wa hilo, Walikuwa na faida ya 2-0, lakini wakaruhusu Malawi kupata ushindi wa 2-1 kwenye mchezo wa pili, walivuka, lakini walijifunza.
SAFARI YA 12
Wameingia Mara 12 kwenye Kombe la Dunia na kucheza fainali mbili ambazo zote wamepoteza, lakini bado kuna kitu kimoja ambacho hakipo kwenye kabati la Falconets ambacho ni ubingwa wa michuano hiyo.
Hii inaweza kuwa nafasi nyingine ya kujaribu kuandika historia hiyo na Nigeria hawaendi Poland kujifunza namna Kombe la Dunia linavyochezwa tayari wanajua na wana uzoefu wa kutosha.