Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Fainali za Kombe la Dunia la Klabu zilivyoacha utamu

DUNIA Pict

Muktasari:

  • Mabao ya Cole Palmer, aliyefunga mara mbili na la kuchopu la Joao Pedro yalitosha kuipa Chelsea ushindi muhimu, wakiichapa PSG katika kipute kilichofanyika kwenye Uwanja wa MetLife.

NEW JERSEY, MAREKANI: FAINALI za Kombe la Dunia la Klabu zimehitimishwa kwa Chelsea kuichapa Paris Saint-Germain 3-0 na kubeba taji hilo kibabe.

Mabao ya Cole Palmer, aliyefunga mara mbili na la kuchopu la Joao Pedro yalitosha kuipa Chelsea ushindi muhimu, wakiichapa PSG katika kipute kilichofanyika kwenye Uwanja wa MetLife.

Palmer alikuwa staa wa mchezo huo wa fainali ya Kombe la Dunia la Klabu, lakini kiungo huyo mshambuliaji wa kimataifa wa England, anafichua kwamba mambo yote yamewezekana kutokana na mpango kazi matata wa kocha Enzo Maresca.

Palmer, ambaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo, akishinda pia tuzo ya kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo (MVP), alisema Chelsea ilikuwa bora uwanjani kutokana na mpango kazi madhubuti wa kocha Maresca, ambaye anaonekana aliwasoma vyema PSG.

Palmer alisema: “Kocha alikuwa na mpango kazi matata. Alijua nafasi ambazo PSG watakwenda kuziacha uwanjani. Alinifanya niwe huru uwanjani kwa kadri inavyowezekana na nilichofanya ni kumlipa mabao.”

Kwa ujumla wake, Palmer alikuwa kwenye kiwango bora kabisa katika michuano hiyo yote, lakini hakuwa staa pekee wa Chelsea, aliyetamba huko Marekani. Staa mpya aliyesajiliwa katika dirisha hili, Joao Pedro, naye alikuwa moto, akifunga mara tatu, ikiwamo bao la kuchopu dhidi ya kipa hodari kabisa, Gianluigi Donnarumma kwenye mechi ya fainali.

DUNI 02

Baada ya ubingwa huo wa Kombe la Dunia la Klabu na Conference League, Palmer anaamini Maresca atatengeneza kitu matata sana katika kikosi cha Chelsea kuanzia sasa, akisema: “Kuna kitu spesho kinajengwa.”

Hayo ni ya kwenye fainali, lakini swali linaloulizwa na wengi kwa sasa, je, mashindano hayo ya Kombe la Dunia la Klabu yamefanikiwa?

Rais wa Fifa, Gianni Infantino alisema kabla ya mechi ya fainali: "Tunachoweza kusema kwa usahihi hizi fainali za Kombe la Dunia la Klabu zimekuwa na mafanikio makubwa sana."

Huko nyuma, michuano hiyo ilikuwa ikifanyika kwenye kipindi cha majira ya baridi, ikijumuisha mabingwa sita wa mabara pamoja na timu moja mwenyeji, lakini sasa imetumia mfumo mpya kabisa, unaolingana na ule wa Kombe la Dunia kwa timu za taifa.

Timu 32 kutoka kweye mabara yote, zilichuana kwenye mechi 63, ikiwamo fainali katika michuano hiyo iliyofanyika Marekani.

Ukosoaji mkubwa wa michuano hiyo iliibuliwa na aliyekuwa kocha wa zamani wa Liverpool, Jurgen Klopp, ambaye alipinga uanzishwaji wa mashindano hayo kwenye soka, akipingana na Infantino.

Hilo lilionekana kupata sapoti baada ya idadi ndogo ya mashabiki waliokuwa wakijitokeza uwanjani, hali mbaya ya hewa na uchovu wa wachezaji, kwamba ni kati ya vitu vilivyoweka doa katika fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu huko Marekani.

"Yamekuwa na mafanikio makubwa. Nimekuwapo kila mahali na hakika yamekuwa mashindano mazuri kuyatazama," alisema Michael Brown, ambaye ni mtangazaji wa Dazn, aliyekuwa akiripoti mashindano hayo.

Kutokana na hilo, mjadala uliopo mezani kwa sasa ni kuhusu uchambuzi wa mashindano hayo ya Kombe la Dunia la Klabu kama zilikuwa fainali za mafanikio au zilichemsha.

DUNI 01

Mashabiki uwanjani

Mengi yamezungumzwa juu ya uchache wa mashabiki waliojitokeza viwanjani kwa baadhi ya mechi. Kuna mechi nne zilishindwa kufikisha mashabiki 10,000 viwanjani, huku idadi ndogo zaidi ya mashabiki kuingia kwenye mechi ilikuwa ile ya 3,412, iliyoshuhudia mechi ya Mamelodi Sundowns ilipowachapa Ulsan HD 1-0.

Lakini, kulikuwa na mechi 15 zilizohudhuriwa na mashabiki 60,000 au zaidi, huku mechi iliyoshuhudiwa na mashabiki wengi zaidi, 80,619, ni iliyoshuhudiwa PSG iliichapa Atletico Madrid 4-0 huko Pasadena.

Mechi zilizokuwa na mashabiki wengi uwanjani ni zile zilizokuwa zikihusisha PSG au Real Madrid, huku idadi kubwa ya mechi hizo ni zile za hatua ya mtoano, ambazo mashabiki wengi walihitaji kwenda kuona kinachotokea uwanjani.

Kwa maana hiyo, wastani wa mashabiki waliohudhuria kwenye viwanja ilikuwa 38,369 ikiwa ni kiwango cha chini kwenye Kombe la Dunia lolote lililowahi kufanyika tangu Chile mwaka 1962.

Sababu kadhaa zilitolewa kuhusiana na uchache wa mashabiki kwenye viwanja kuwa ni muda wa kuanza mechi, bei ya tiketi, hali ya hewa na ishu ya uhamiaji ambapo zilikuwa zinavuruga mashabiki wa kutoka eneo moja kwenda jingine kunakofanyika mechi.


1. Mechi za mashabiki wachache

Ulsan HD 0-1 Mamelodi Sundowns, 3,412

Pachuca 1-2 Salzburg, 5,282

Benfica 6-0 Auckland City, 6,730

Borussia Dortmund 1-0 Ulsan HD, 8,239

Wydad AC 1-2 Al Ain, 10,785

2. Mechi za mashabiki wengi

Chelsea 3-0 PSG, 81,118

PSG 4-0 Atletico Madrid, 80,619

PSG 4-0 Real Madrid, 77,542

Real Madrid 3-2 Borussia Dortmund, 76,611

Fluminense 0-2 Chelsea, 70,556

DUNI 06

Bei za tiketi

Baada ya kuelezwa kwamba moja ya sababu za mashabiki kuwa wachache kwenye mechi ni bei ya tiketi kuwa juu, Fifa ilikuja na utaratibu wa kushusha bei ya tiketi hizo, ambapo mchezo wa nusu fainali kati ya Chelsea na Fluminense, bei ya tiketi iliripotiwa kushuka kutoka karibu Pauni 350 hadi chini ya Pauni 10.

Tiketi za robo fainali baina ya Chelsea na Palmeiras zilikuwa Pauni 8, ambapo mashabiki walalamika huko nyuma walilipa zaidi ya Pauni 250, tiketi ambazo zilitangulia kuuzwa kabla ya punguzo.


Ushindani wa timu umekuwaje?

Kilichovutia kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia la Klabu ni kwamba kila timu ilikuwa inapambana kushinda mechi na hilo lilifanya kuwapo na ushindani mkubwa, huku chanzo kikubwa kikielezwa ni zawadi ya pesa iliyokuwa ikishindaniwa.

Timu zilikuwa na nafasi ya kuvuna hadi Pauni 91 milioni kwa ile ambayo itakwenda hadi kwenye hatua ya kunyakua ubingwa, huku timu iliyokomea kwenye hatua ya 16 bora, kama ilivyotokea kwa Manchester City iliweka kibindoni Pauni 38 milioni.

Chelsea baada ya kutinga tu fainali, tayari ilikuwa imejihakikishia Pauni 80 milioni kwenye akaunti ya benki, ambapo staa wao mpya, Joao Pedro alilipa pesa yao waliyomsajili kwa kufunga mara mbili kwenye mechi ya nusu fainali dhidi ya Fluminense.

DUNI 05

Mgawo wa pesa ulivyokuwa unaongezeka

-Kushiriki tu, Pauni 27.9 milioni

-Hatua makundi: Imeongezeka Pauni 4.4milioni

-Hatua 16 bora: Imeongezeka Pauni 5.5milioni

-Robo fainali: Imeongezeka Pauni 9.6milioni

-Nusu fainali: Imeongezeka Pauni 15.3milioni

-Fainali: Imeongezeka Pauni 21.9milioni

-Bingwa: Imeongezeka Pauni 7.3milioni


Kingine kitamu kuhusu bingwa wa mashindano hayo ataruhusiwa kuvaa beji ya Kombe la Dunia la Klabu ya ubingwa kwenye jezi hadi majira ya kiangazi 2029, wakati fainali nyingine zitakapofanyika.


Sababu za kimpira

Kwenye upande wa soka, mashindano hayo yanahesabika kuwa yenye mafanikio makubwa. Hatua ya makundi ya mashindano hayo ilianza kwa kasi ndogo na wengi walionekana kama ushindani utakuwa hafifu baada ya Bayern Munich 10-0 dhidi ya Auckland City.

Lakini, kulikuwa na mechi nyingine pia zilizokuwa na mabao mengi na kufanya kuwapo na wastani wa mabao matatu kwa kila mechi. Kuna matokeo ya kushtua pia, ikiwamo Man City kuchapwa na Al-Hilal kwa mabao 4-3 baada ya dakika 120.

Benfica nayo ilipambana na Chelsea hadi kwenye dakika za ziada kabla ya The Blues kushinda 4-1. Chelsea ilifunga bao la ushindi kwenye dakika za mwishoni dhidi ya Palmeiras kwenye hatua ya robo fainali, ambapo Estevao Willian, ambaye atajiunga na timu hiyo ya London baadaye mwezi huu, alifunga dhidi ya timu yake tarajiwa.

Lionel Messi alifunga bao matata kabisa kwa mpira wa frii-kiki, timu ya soka la ridhaa Auckland City ikipata pointi mbele ya Boca Juniors, baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza kwa jumla ya mabao 16-0, na kulikuwa na mechi zilizokuwa na matokeo ya 4-4, 4-3, 4-2 na 5-2.

PSG, ambayo ilikuwa kwenye kiwango bora kabla ya kuchapwa fainali, ilizichapa Atletico Madrid, Real Madrid na Inter Miami kwa mabao 4-0. PSG iliichapa Bayern 2-0 licha ya kubakiwa na wachezaji tisa uwanjani  na kulikuwa na mabao matatu ya dakika za majeruhi na kadi nyekundu, wakati Real Madrid ilipoichapa Borussia Dortmund 3-2.

DUNI 04

Mashabiki wa nje ya Marekani wamependa?

Ni takwimu ngumu kuzikusanya, lakini kwa namna fulani fainali hizo zimevutia mashabiki wengi duniani kote waliokuwa wakifuatilia kupitia luninga. Kwa mfano mechi ya Chelsea dhidi ya Los Angeles FC ilitazamwa na mashabiki 1.6 milioni huko Uingereza, wakati Real Madrid na Al-Hilal ilivutia mashabiki 1.1 milioni.

Huko Saudi Arabia zaidi ya mashabiki 1.5 milioni walitazama mechi ya kipigo cha Man City kwenye raundi ya 16 bora, licha ya mechi hiyo kuchezwa saa 10:00 alfajiri kwa saa za huko kwao.

Mashabiki wa Brazil waliripotiwa kuvutiwa zaidi na fainali hizo kwa sababu timu zote zote nne zilitinga kwenye hatua ya mtoano, hivyo kwa wingi wao walikuwa wakifuatilia fainali hizo, ambapo kwenye Uwanja wa Copacabana mashabiki walikuwa wakijaa kutazama mechi.


Uchovu na majeraha kwa mashabiki

Hiki litahitaji muda kiasi kufahamu uchovu wa wachezaji walioshiriki kwenye fainali hizo, ukiweka kando wale waliopata majeraha ya moja kwa moja kama ilivyo kwa Jamal Musiala wa Bayern Munich. Wachezaji waliokwenda kwenye fainali hizo hawakuwa na mapumziko ya kutosha, kwa sababu walitokea tu kwenye mikikimikiki ya ligi na kwenda kwenye michuano mikubwa. Na pengine hadi kufikia Desemba au Januari uchovu wa mastaa mbalimbali utaanza kuonekana.


DUNI 03

Ubunifu

Kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu kulikuwa na ubunifu uliokuwa tofauti kabisa na utamaduni uliozoeleka kwa miaka mingi kwenye mchezo wa soka. Mchezaji Bora wa Mechi badala yake aliitwa ‘Superior Player of the Match.” Kitu kingine, wachezaji 22 walikuwa wakiitwa mmoja baada ya mwingine kwa sauti kubwa uwanjani wakati wa kuingia kwenye mechi, tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo wachezaji wote wamekuwa wakipanga mstari na kuingia.

Kulikuwa na kuhesabu dakika kabla ya mechi kuanza na muziki ulipigwa kwenye kila mapumziko ya kupoza mwili kwa kupata maji. Mwamuzi msaidizi wa video (VAR) uamuzi wake ulikuwa ukionyeshwa uwanjani kupitia kamera iliyokuwa ikikubaliwa na mwamuzi, huku refa akiweka bayana kosa la mchezaji kabla ya kuchukua uamuzi wake.