DONISIA; Miaka 16 ya kibabe soka la wanawake
Muktasari:
- Kuna nyota kama Fatuma Bushiri, Asha Mwalala, Mwanahamisi Omary ambao walifanya makubwa kwenye soka la wanawake lakini kiungo mmoja hivi anayetokea mitaa ya Mapigo na Mwendo, Donisia Minja amejiwekea utawala wake.
KWENYE soka la wanawake, kuna wachezaji wanaokuja na kuondoka kama upepo, na wapo wachache wanaojenga ufalme wao kwenye soka hilo linaloendelea kukua nchini.
Kuna nyota kama Fatuma Bushiri, Asha Mwalala, Mwanahamisi Omary ambao walifanya makubwa kwenye soka la wanawake lakini kiungo mmoja hivi anayetokea mitaa ya Mapigo na Mwendo, Donisia Minja amejiwekea utawala wake.
Tangu aanze soka la ushindani huu unakuwa mwaka wa 16 kiungo huyo fundi kuitumikia JKT Queens akiwa na kiwango kile kile kinachofanya kila makocha waendelee kumtumia.
Amefundishwa na makocha mbalimbali kama Ally Ally, Azishi Kondo ambaye alianza kumfundisha tangu akiwa shuleni hadi sasa, Ester Chabruma na sasa Abdallah Kessy hawajawahi kumuweka benchi Minja.
Ukiwauliza watakuambia mambo mengi, lakini wengi ni nidhamu yake anapokuwa uwanjani anabadilika kulingana na mpango wa kocha, huku anatoa kile unachotaka kwa wakati sahihi.
Ukianza kumchambua Donisia unaweza usimalize maneno kutokana na ubora wake. Anacheza kana kwamba alianza juzi kati. Lakini Mwanaspoti linakuletea miaka 16 ya soka la ushindani na namna alivyoendelea kukomaa na nafasi yake kwenye kikosi cha JKT Queens na Twiga Stars.
SAFARI YAKE
Donisia ni nyota mkongwe kwenye soka la wanawake akiwa alianza kukipiga tangu 2004 akiwa Shule ya Msingi Airwing, Dar es Salaam na 2009 alisajiliwa na Simba Queens hadi 2014 kisha akajiunga na Evergreen na msimu uliofuata alitua JKT Queens ambako ndiko alipo hadi sasa.
Ni miaka 16 sasa ya kiungo huyo mkabaji tangu aanze kucheza soka akiwa na JKT Queens na ndio timu aliyocheza muda mrefu.
Kiungo huyo amekuwa muhimu ndani ya kikosi hicho na amefanikiwa kuisaidia timu hiyo kuchukua mataji manne ya Ligi Kuu ya Wanawake Bara katika misimu ya 2017-18, 2018-19, 2022-23 na 2024-25.
Tangu msimu wa kwanza hajawahi kuchuja na amekuwa na ubora uliomfanya ajiwekee ufalme kwenye eneo hilo ambalo siyo rahisi kukaa benchi kutokana na uwezo wake.
Mbali na kuisaidia JKT Queens eneo la ukabaji, pia ana uwezo wa kufunga na mfano ni 2022/23 alipofunga mabao 17 akitofautiana na Jentrix Shikangwa wa Simba aliyefunga 19 aliyeibuka na kiatu cha ufungaji bora.
Msimu huo chama lake la JKT lilimaliza likiwa na ‘clean sheet’ saba yaani kiufupi ni mzuri kwenye kuzuia, lakini wakati huohuo anafunga na kushindana na washambuliaji kwenye vita ya ufungaji bora.
Kwenye moja ya mahojiano aliwahi kusema, “nafunga sana mabao ya frikiki kwa sababu nayafanyia sana mazoezi. Tukishamaliza mazoezi ya timu kocha ananipa mazoezi maalumu ya kufunga kwa faulo kila siku hivyo nawekewa mipira zaidi ya 10 kufanyia zoezi hilo.”
Kwa kuthibitisha hilo msimu uliopita kwenye mechi ngumu na Yanga Princess na Simba Queens kiungo huyo aliwafunga watani hao wa jadi kila mmoja bao moja la frikiki.
MCHANGO JKT QUEENS
Nyota huyo amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho tangu JKT ianze kushiriki Ligi Kuu ya Wanawake Bara 2017 akiisaidia kunyakua mataji sita hadi sasa - manne ya Ligi Kuu sawa na Simba Queens na mawili ya Ngao ya Jamii kwa wanawake ikiweka rekodi ya kipekee.
Uwepo wake umeifanya JKT Queens kuwa miongoni mwa timu zinazoogopwa WPL. Timu inapokutana na wanajeshi hao, kinachoangaliwa kwanza ni jinsi ya kumzuia Donisia hiyo inaonyesha uzito wake ndani ya mfumo wa timu.
Kwenye eneo analocheza wapo wachezaji wengine kama Janeth Pangamwene, Elizabeth Chenge, Joyce Lema, Fatuma Bushiri lakini bado ameendelea kuchukua nafasi hiyo.
Kipengele kingine cha mchango wake ni kutokuchuja kwa misimu yote aliyoichezea timu hiyo. Kila msimu yupo kwenye kiwango kikubwa. Hii ni nadra wachezaji wengi hupanda na kushuka, lakini Donisia ameendelea kuwa chaguo la kwanza kwa makocha msimu baada ya msimu.
Hii ndiyo sifa inayomfanya awe wa kipekee. Licha ya kuwa mkabaji, Donisia ni mzuri kupiga mashuti ya mbali, free-kick na penati. Msimu uliopita alipachika mabao sita, idadi isiyotegemewa kwa mchezaji wa nafasi yake. Huu ndio ubora uliofanya JKT Queens kuwa na machaguo mawili kumtumia kama mlinzi wa eneo la kati na wakati huo huo akisaidia kufunga.
Donisia si mchezaji wa kupiga mipira ya kubahatisha. Ana uwezo wa kugeuza ulinzi kwenda shambulizi kwa kupiga pasi sahihi, zenye kutengeneza mwelekeo wa mchezo. Huu ndio ufundi unaomtofautisha na viungo wengi wa ukabaji nchini. Ndiyo maana mara nyingi JKT Queens huonekana timu inayocheza kwa utulivu na mpangilio, kwani mipira inapita kwake kabla ya kwenda kwa washambuliaji.
TWIGA STARS.
Mbali na timu pia amekuwa na nafasi yake kwenye kikosi cha timu za taifa tangu vijana U-17, U-20 na hadi sasa Twiga Stars.
Uzoefu alioupata akiwa na kikosi cha JKT kimemfanya kocha wa Twiga Stars, Bakari Shime kuendelea kumuanini kwenye timu hiyo na ameendelea kuonyesha uwezo na uzalendo.
Aliisaidia Twiga Stars kufuzu Wafcon na mashindano ya Kombe la Dunia la Futsala ambalo limetamatika hivi karibuni, Tanzania ikiishia makundi.
MSIKIE MWENYEWE
Akizungumzia kiwango chake Minja alisema “Nafikiri sababu ya kuwa na kiwango bora ni kuepuka mambo mengi mimi nafanya sana mazoezi na muda mwingi nautumia kupumzika na kuepuka mambo ya kuharibu karia yangu.”